Kigogo TFF ataja mrithi wa Sven

HABARI za uhakika ni kwamba Jumatatu mchana Simba itakuwa na kocha mkuu mpya raia wa kigeni. Ingawa wanafanya siri kubwa aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Madadi ametaja sifa za kocha mkuu ajaye wa klabu hiyo.

Sven Vandebroeck aliyekuwa kocha mkuu wa mabingwa hao watetezi wa ligi, aliachana na klabu hiyo hivi karibuni ikiwa ni siku chache tangu alipoiongoza kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Wakati uongozi wa Simba inayonolewa na kocha msaidizi, Seleman Matola ukiwa kwenye harakati za kupata kocha mkuu, Madadi ambaye ni Mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), amesema klabu hiyo inahitaji kocha mwenye sifa kuu tano.

“Kwanza awe na uwezo na rekodi bora ya ukocha kimataifa bila kujali ni mzawa au kocha wa kigeni,” alisema Madadi.

Alisema kocha mpya anatapaswa kuwa tayari kukopi na falsafa ya klabu, pia awe na sifa ya utawala bora na uhusiano mzuri kwa umma.

“Hii sio kwa Simba tu, makocha wote wanapaswa kuwa na uhusiano mzuri, ni muhimu sana katika kazi yao, kama Simba itafanikiwa kupata kocha mwenye sifa hizo, naamini watafanikiwa,” alisema.

Madadi aliyewahi kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo alisema, nchini wapo makocha wenye sifa za kuinoa timu hiyo.

“Siwezi kuwataja, ila wapo na wanajulikana, japo uamuzi ni wa klabu kuajiri mzawa au kocha wa kigeni,” alisema.