Job ana rekodi tamu Yanga

Dar es Salaam. Licha ya kuwa na nyota wengi kwenye eneo la beki wa kati, Dickson Job amejihakikishia namba na kutengeneza rekodi ya kuwa beki pekee aliyecheza dakika nyingi kuliko yeyote msimu huu.

Hadi sasa, Yanga imecheza mechi 11 na Job amecheza michezo 10 mfululizo, huku nyota wengine kwenye eneo hilo Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ na Yannick Bangala wakicheza kwa kubadilishana, lakini wote hawajamfikia Job kwa dakika na mechi alizocheza.

Msimu huu, Job amecheza dakika 810 ambapo ametumia dakika 90 kwenye mechi nane na dakika 45 katika mechi dhidi ya Azam FC, ambayo alishindwa kumaliza baada ya kuumia na kuingia Djuma Shaban na dakika 45 nyingine kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold akimpisha Bangala.

Katika mechi hizo Job amecheza na Bakari Mwamnyeto, Bacca na Bangala, huku timu hiyo ikiwa haijapoteza mchezo wowote.

Akizungumzia kuwa kwake kwenye kikosi cha Yanga mfululizo, Job alisema ni kutokana na kuaminiwa na benchi la ufundi kwa kutimiza majukumu yake vizuri.

Alisema kama mchezaji kijana atahakikisha anatumia vizuri kila nafasi ambayo anapewa na lengo ni kuisaidia timu kuzidi kufanya vizuri.

“Nashukuru benchi la ufundi limekuwa likiniamini na kunipa nafasi kila wakati hata inapotokea nakosea, lakini wanaendelea kuniamini na kunipa moyo,” alisema Job.

“Ni bora kwangu kuaminiwa. Kunanijengea kujiamini na kuwa mzoefu, lakini yote kwa yote nabebwa na ujasiri wangu, kujituma mazoezini na kiu yangu ya kufanya makubwa ili nifike mbali.”

Akimzungumzia mchezaji huyo, nyota wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema Job ni mchezaji ambaye amekuwa anapanda kiwango siku hadi siku tangu alipokuwa Mtibwa Sugar.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hery Morris alisema: “Job anajituma na anajitunza na siyo mtu wa starehe.”