Ishu ya Tambwe, Kichuya yazipasua kichwa Simba, Yanga

SAKATA la nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Shiza Kichuya na Amissi Tambwe kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeendelea kuzipasua klabu hizo.

Fifa ilimfungia Kichuya kutojihusisha na soka kwa miezi sita, huku ikiitangwa Simba faini ya Dola 130,000 kwa kumsajili mchezaji huyo kinyemela akiwa ni mali ya Pharco ya Misri iliyomnunua kutoka Msimbazi 2018/19.

Upande wa Tambwe, Fifa iliitaka Yanga imlipe malimbukizo ya usajili na mshahara wake zipatazo Dola 20,802 na klabu hizo zilipewa siku 45 kulipa, japo Simba ilieleza kuomba kufanya marejeo ya kesi hiyo.

Tambwe alisema jana kuwa: “Mwanasheria wangu ameniletea fomu ya kusaini ili kuirudisha Fifa kuwapa mrejesho wa nini kinaendelea juu ya malipo yangu, nimeisaini jana hivyo nasubiri Fifa watakachonijibu.”

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoulizwa alisema suala hilo analifuatilia, huku Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hawezi kulizungumzia sakata la Kichuya.