Ishu ya Saido Yanga iko hivi

YANGA imeanza kuwaongeza mikataba wachezaji wake ikiwa ni maandalizi ya msimu ujao kitaifa na kimataifa lakini hatima ya nyota wake Said Ntibanzokiza ‘Saido’ kubaki au kuondoka kikosini hapo haijafikiwa.

Saido alijiunga Yanga mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Vital’O ya Burundi mkataba ambao umefika tamati mwezi huu lakini licha ya mazungumzo kuhusu hatima yake ndani ya chama hilo kufanyika baina ya pande zote mbili kwa zaidi ya mara tatu lakini jibu la mwisho halijafikiwa.

Mwanaspoti linajua kuwa ishu yake inashindwa kumalizika kutokana na kuwa na malumbano ya hoja kati ya viongozi wa Yanga wakiwepo wanaotaka nyota huyo abaki na wengine wakitaka aondoke na kusajili mashine nyingine.

Taarifa zinaeleza kuwa licha ya Saido kuhusika kwenye mabao 11 hadi sasa kati ya 35 iliyofunga Yanga akitupia mara sita na asisti matano lakini bado baadhi ya viongozi wa Yanga wametosheka na huduma yake na sasa wanataka wachezaji wengine wapya.

Hata hivyo, uhusiano wa Saido na viongozi wa juu wa timu hiyo pamoja na wadhamini wa Yanga (GSM) ni kati ya mambo yanayoweza kumbakiza Jangwani kwa msimu ujao kwani wanaamini kwa uzoefu wake kwenye michuano mbalimbali akicheza kwenye Ligi Kuu za Uholanzi, Poland, Uturuki, Kazakhstan na Ufaransa utaisaidia Yanga msimu ujao kwenye Ligi Mabingwa Afrika.

Akizungumzia mkataba wake kwenye moja ya mahojiano aliyoyafanya na Mwanaspoti hili, Saido alifunguka kuwa kwa sasa nafasi kubwa ameipa Yanga na kama mambo yataenda tofauti basi ataweka wazi wapi anaenda.

“Haya ni mambo ya kimkataba ambayo siwezi kuyaweka wazi lakini mimi bado nipo Yanga na ndio timu nimeipa nafasi kubwa kubaki, mengine hayo tusubiri kwanza kuona itakuwaje,” alisema Saido.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa alisema usajili wa Yanga unafanywa kwa weledi na wachezaji wote wanaohitajika na benchi la ufundi watahakikisha wanawabakiza Yanga na kuongeza vifaa vingine.

“Sio kwa Saido tu, wachezaji wote watakaoongezewa mikataba watapitishwa na Benchi la Ufundi,” alisema Senzo akisisitiza kuwa mambo yote ya mikataba yanaendelea ndani kwa ndani na klabu ina utaratibu wa kumalizana na wachezaji kupitia matakwa ya benchi la ufundi.

MWAMNYETO, KIBWANA

Juzi Yanga imewaongezea mikataba wa miaka miwili beki Kibwana Shomari pamoja na nahodha Bakari Mwamnyeto.

Mwamnyeto ambaye aliingia kwenye rada za Simba kwa kumshawishi akaitumikie msimu ujao amefanya uamuzi wa kusalia Jangwani hadi 2024.

Uongozi wa Yanga ambao awali ulizungumzia mipango ya kuwaongeza mikataba mastaa hao baada ya msimu kumalizika, umethibitisha kuwa umeshtuka na kuamua kumalizana nao ili kuwaongezea morari katika michezo saba iliyobaki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shomari alisema; “Nina uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza nimeaminiwa hadi kubadilishwa namba, sijaona sababu ya kuondoka na kwenda sehemu nyingine na naamini bado nitaendelea kuwa bora kutokana na kukutana na wachezaji wazoefu nimekuwa nikijifunza kutoka kwao.”