Gwambina yamchomoa Zahera

WAKATI tetesi zikidai kuwa huenda Mwinyi Zahera akapewa mikoba rasmi kuinoa Gwambina FC, uongozi wa Klabu hiyo umesema ni suala gumu kutokana na Mkongo huyo kuwa na majukumu kwenye timu yake ya Taifa.

Hivi karibuni Gwambina FC iliwatimua Makocha wake, Fulgence Novatus na msaidizi wake, Athuman Bilal ‘Billo’ ambapo kwa sasa inasimamiwa na Hassan Salum aliyekuwa timu B na Seleman Kisend kocha wa viungo.

Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Daniel Kirai alisema Zahera licha ya kuwa na vigezo vyote vya kuifundisha timu, lakini kigezo cha kuwa na timu yake ya Taifa, kinawapa ugumu kumpa jukumu.

Alisema “Hata kama Zahera ni kocha msaidizi wa timu yao ya Taifa, lakini inaweza kutokea dharula akahitajika sasa tutabakije? Alihoji na kufafanua kuwa “Kuna makocha tunaendelea nao kuzungumza naamini hivi karibuni tutaweka sawa.”

Katibu huyo aliongeza kwa sasa wachezaji bado hawajarejea kambini, hivyo huwenda watakaporipoti wakakuta kila kitu kimekaa sawa.