Gomes: Bado moja tu

Muktasari:

  • Simba ilijiwekea mikakati ya kuhakikisha inashinda michezo yote mitatu Kanda ya Ziwa ambayo itazidi kuwaweka katika nafasi nzuri za kutetea taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa nne mfululizo

BADO moja!! ndivyo naweza kusema kwa Simba wakiwa kanda ya ziwa kukamilisha ratiba yao ya kusaka pointi tisa kuelekea kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne mfululizo.

Simba ilitinga kanda ya ziwa ikiwa na vibarua vitatu vya kuwakabili Mwadui ambao walifungwa bao 1-0, Kagera Sugar bao 2-0 na sasa Gwambina Aprili 24 ikiwa ni mchezo wa kiporo baada ya Simba kuwa katika majukumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa mujibu wa Kocha wa kikosi hicho Didier Gomes walienda kutafuta ushindi katika kila mchezo ambao wanakutana nao huko kanda ya ziwa ili kuzidi kusogea katika msimamo ya ligi na sasa wamesalia na mchezo mmoja.

Simba jana ilifikisha pointi 55 katika mechi 23 wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Yanga wenye pointi 57 wakiwa tayari wamecheza mechi 26.

Gomes amesema katika michezo miwili iliyopita wamekumbana na ushindani mkubwa lakini cha kumshukuru Mungu ni matokeo ya pointi tatu ambayo wameyapata katika mechi hizo.

Amesema kwa sasa wamebakiza mchezo mmoja Jumamosi ambao na wenyewe anahitaji pointi tatu kama ambavyo alipanga toka awali licha ya kukubali ushindani ni mkubwa.

"Ushindani ni mkubwa sana sasa, kila timu ambayo nakutana nayo mimi ni kama fainali, na ndio maana nawataka wachezaji wangu wapambane tupate matokeo na tutimize malengo yetu,"amesema Gomes.