Fiston aongeza mzuka Yanga, kuwasili Jumamosi

Dar es Salaam. Usajili wa mshambuliaji mpya wa Yanga, Fiston Abdulrazak umewapa mzuka mashabiki wa timu hiyo, ambao wanaamini utamrahisishia kazi kocha Kaze Cedric.

Fiston raia wa Burundi anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa na Jumatatu ijayo atafanya mazoezi ya pamoja na wenzake kwenye kambi ya timu hiyo, Kigamboni, Dar es Salaam.

Akizungumza jana, kocha Kaze alisema kesho mchezaji huyo atakuwa katika harakati za safari ya kuja nchini kujiunga na timu yake mpya ya Yanga.

“Nafikiri atawasili Jumamosi, ila mazoezi rasmi tutaanza Jumatatu,” alisema kocha Kaze ambaye ana ndoto ya kuipa Yanga ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu kadhaa mfululizo.

Akizungumzia ubora wa mchezaji huyo, Kaze alisema Wanayanga ashushe presha, wasubiri kuhesabu mabao.

“Ni mchezaji mzuri, si yeye tu, wachezaji wote wa Yanga wana kiwango bora, naamini tutafanya vizuri zaidi, tusubiri kuanza mazoezi” alisema.

Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe alisema timu itaanza kambi rasmi Jumatatu, hivyo kila mchezaji anatakiwa kuwepo kwenye mazoezi ya Asubuhi ya siku hiyo.

Wakati Yanga wakijiandaa na kambi hiyo, mashabiki wao wameshusha presha na kuwa na matarajio makubwa na kikosi chao msimu huu hasa baada ya kukiboresha kwenye usajili wa dirisha dogo hivi karibuni.

“Kwa aina ya wachezaji tulionao na ubora wa kocha, sioni cha kutukosesha ubingwa msimu huu, kuna timu itapigwa 10-0 mzunguko huu wa pili,” alijinasibu mwenyekiti wa wakali wa Terminal, Mohammed Abdallah ‘Muddy Yanga.

Katika hatua nyingine, mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ya Yanga utaendelea tena kesho kwa kikao cha mabadiliko ya katiba.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema baada ya kikao hicho, watapeleka rasimu hiyo Serikalini, kisha TFF na baadaye kwa wanachama na wadau wao kabla ya kupelekwa kwenye mkutano mkuu ili kuipitisha.