Dah! ni wao

Dah! ni wao

Muktasari:

  • Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya timu zilizopiga pesa ndefu kutokana na mauzo ya mastaa wake kwa kuanzia msimu wa 2009-10. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Transfermarkt.

LONDON, ENGLAND. BENFICA imeweka kibindoni mkwanja mrefu, Pauni 1 bilioni kupitia mauzo ya mastaa wake kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Dirisha la usajili wa wachezaji limezidi kuwa maarufu na klabu kubwa duniani zimekuwa zikipata shida katika kuonyesha jeuri yao kwenye matumizi hasa baada ya uchumi wao kuathiriwa kiasi kikubwa na janga la virusi vya corona. Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, klabu kadhaa zilifungua milango ya kuwapiga bei mastaa wao ili kunusuru hali ya mambo.

Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya timu zilizopiga pesa ndefu kutokana na mauzo ya mastaa wake kwa kuanzia msimu wa 2009-10. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Transfermarkt.

1.Benfica-Pauni 1 bilioni

Miamba hiyo ya Ureno si tu kwamba wamepiga pesa ndefu kwenye mauzo ya wachezaji wake, lakini pia imeonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja baada ya kubeba mataji sita ya ligi ndani ya muda huo.

Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi walimpiga bei Ruben Dias kwenda Manchester City kwa ada ya Pauni 64 milioni, huku kabla ya hapo iliwauza Ederson (Pauni 35milioni) na Joao Felix (Pauni 101milioni). Nemanja Matic (Pauni 21milioni), Axel Witsel (Pauni 34milioni) na Victor Lindelof (Pauni 32milioni) huku mauzo hayo yakiwaingizia faida ya Pauni 539 milioni.

2.Atletico Madrid - Pauni 953 milioni

Moja ya klabu iliyopatwa na msongo wa mawazo kutokana na janga la virusi vya corona kuathiri uchumi wao ni Atletico Madrid. katika kuhakikisha wanaweka hesabu zao sawa, Alvaro Morata, Santiago Arias na Thomas Partey ni mastaa waliopigwa bei kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi na hakukuwa na usajili mkubwa kwa maana ya wachezaji waliokuja badala yao. Kwenye mauzo ya mastaa hao, pamoja na yale ya mastaa Antoine Griezmann (Pauni 107milioni), Diego Costa (Pauni 32milioni) na Radamel Falcao (Pauni 51milioni) yamewafanya Atletico Madrid kuingiza Pauni 953 milioni kwenye mauzo ya wachezaji.

3.Juventus - Pauni 900 milioni

Hakuna timu nyingine kwenye orodha hii iliyouza wachezaji wengi kuzidi Juventus. Ndani ya kipindi cha miaka 10, wachezaji 582 wameuzwa na timu hiyo, wakati 591 waliwasili kwenye kikosi, huku wengi wao wakiibuliwa kwenye akademia ya miamba hiyo ya Turin. Staa wao, Paul Pogba alivunja rekodi ya uhamisho duniani wakati aliponaswa na Manchester United kwa ada ya Pauni 89 milioni mwaka 2016. Leonardo Bonucci aliuzwa Pauni 37 milioni, Arturo Vidal (Pauni 35 milioni) na Moise Kean (Pauni 24 milioni) hao ikiwa ni baadhi tu walioingizia pesa nyingi mabingwa hao wa Serie A.

4.Chelsea -Pauni 886 milioni

Adhabu ya kufungiwa na Fifa kufanya usajili ilimshuhudia kocha Frank Lampard akiamua kuweka imani yake kwa wachezaji makinda zaidi kwenye kikosi chake cha Chelsea kwa msimu uliopita kabla ya kufungulia pochi kwenye dirisha lililopita kunasa mastaa. Kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2019 iliishuhudia The Blues ikiingiza Pauni 113 milioni, ikiwa ni rekodi tangu Roman Abramovich alipoinunua klabu hiyo. Eden Hazard bado anaendelea kuwa mchezaji aliyeuzwa kwa pesa nyingi zaidi, Pauni 150 milioni, wakati wachezaji wengine waliouzwa pesa ndefu ni Oscar (Pauni 52milioni) na Diego Costa (Pauni 50milioni). Hata hivyo, ndani ya muongo huo mmoja, Chelsea imetumia Pauni 1.45 bilioni.

5.Monaco - Pauni 868 milioni

Mamilioni ya Dmitry Rybolovlev yaliifanya Monaco kuwa wababe kiuchumi kwa muda fulani mwaka miaka ya 2010. Baada ya hapo, timu hiyo ilifanya biashara ya pesa ndefu kwa kuwauza mastaa kadhaa akiwamo Kylian Mbappe, Thomas Lemar, James Rodriguez na Anthony Martial - wote hao waliingizia pesa za kutosha timu hiyo. Mastaa hao wanne wameingizia Monaco mkwanja wa Pauni 316 milioni. Monaco ni timu nyingine iliyopiga faida kubwa kutokana na mauzo ya mastaa wake ndani ya muda huo licha ya misimu ya karibuni imekuwa haina maajabu kwa kumaliza nafasi za chini kwenye Ligue 1.

6.Barcelona - Pauni 862 milioni

Ubora dhidi ya wingi ni kitu kinachozingatiwa zaidi kwenye klabu za Barcelona na Real Madrid, wababe wakubwa hao kwenye mikimimikiki ya La Liga. Kutokana na hilo limeifanya Barcelona kuwa moja ya timu zilizopiga pesa nyingi kwa kuwauza mastaa wake. Miamba hiyo imeingiza Pauni 862 milioni kwenye mauzo ya mastaa wake, ambapo ndani ya muda huo wachezaji waliouzwa ni 148, huku ikiwa imebeba mataji saba ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Paris Saint-Germain ilimsajili Neymar kwa bei ghali zaiid duniani na kuvunja rekodi ilipomnasa kwa Pauni 198 milioni kutoka Barcelona mwaka 2017. Hata hivyo, ndani ya muda huo, Barcelona imepata hasara ya Pauni 613 milioni.

7.Real Madrid - Pauni 823 milioni

Kama ilivyo kwa wapinzani wao wa El Clasico, Real Madrid haikufanya usajili wa staa yeyote kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu ili kukabiliana na ukata uliosababishwa na janga la virusi vya corona. Zaidi ya hilo, kitu ambacho imefanya timu hiyo ni kuwapiga bei mastaa wake, akiwamo Achraf Hakimi (Pauni 36milioni), Sergio Reguilon (Pauni 27milioni) na Oscar Rodriguez (Pauni 12milioni) wote hao waliondoka. Los Blancos iliwauza pia Cristiano Ronaldo (Pauni 89 milioni) na Angel Di Maria (Pauni 59.7 milioni), ikiwa ni wachezaji iliyowaingizia pesa ndefu. Pesa hiyo Pauni 823 milioni imevunwa kwenye mauzo ya wachezaji 138, wakati yenyewe imenunua mastaa 141 ndani ya muda huo.

8.AS Roma - Pauni 788 milioni

Ukitaja kufahamu ubora wa wachezaji waliopita kwenye uwanja wa Stadio Olimpico miaka ya karibuni, basi tazama kwenye kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England. Liverpool isingeweza kubeba ubingwa huo kama isingekuwa na huduma ya mastaa kipa Alisson Becker na mshambuliaji Mohamed Salah, ambao wote waliigharimu timu hiyo Pauni 92 milioni ilipowasajili kutoka AS Roma.

Miamba hiyo ya Italia, iliwauza pia Radja Nainggolan (Pauni 34 milioni) na Kostas Manolas (Pauni 32 milioni) ikiwa ni wachezaji waliowaingizia faida kubwa kwenye mauzo yao. Ndani ya muda huo, Roma imeshinda Coppa Italia mara mbili tu, huku ikipata hasara ya Pauni 39 milioni.

9.FC Porto - Pauni 785 milioni

FC Porto imezidi kudhihirisha kwamba soka la Ureno limekuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha mastaa wa maana huku yenyewe ikipata vipaji hivyo kutoka America Kusini. Kuanzia kwa Eder Militao iliyowauza (Pauni 44.5 milioni), James Rodriguez (Pauni 42 milioni), Hulk (Pauni 35 milioni) na Eliaquim Mangala (Pauni 32 milioni) ikiwa wachezaji wote iliwasajili kwa pesa kidogo sana wakiwa vijana na kuwauza bei kubwa. Ni miamba mingine pamoja na Benfica waliotengeneza faida kwenye mauzo ya wachezaji baada ya FC Porto yenyewe kuingiza Pauni 393 milioni ikiwa ni faida ndani ya misimu hiyo 10. Porto pia ndani ya muda huo imebeba ubingwa wa ligi mara tano na Europa League.

10.Liverpool - Pauni 730 milioni

Mafanikio ya kocha Jurgen Klopp kwenye kikosi cha Liverpool yalikuja baada ya timu hiyo kubadili sera kutoka kwenye kuwa timu inayouza tu mastaa wake na kuwa timu inayonunua wakali wenye vipaji. Kocha huyo Mjerumani, alitumia pesa alizopata kwenye mauzo ya mastaa Philippe Coutinho (Pauni 130 milioni), Luis Suarez (Pauni 72 milioni) na Raheem Sterling (Pauni 57 milioni) kujenga kikosi cha kibingwa.

Pesa nyingine Liverpool ilivuna kwenye mauzo ya mastaa Rhian Brewster (Pauni 18 milioni) na Dejan Lovren (Pauni 11 milioni) waliouzwa kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Licha ya kuingiza pesa nyingi kwa kuuza wachezaji, Liverpool pia ilifanya usajili wa kuboresha kikosi chao na jambo hilo limewafanya kupata hasara ya Pauni 294 milioni kwenye soko la usajili.