Atiki: Niombeeni, Kucheza NCAA si rahisi

Muktasari:

  • Akiwa nchini, Atiki amewahi kucheza timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 18, Academy ya JMK Elite Training, klabu ya Yellow Jackets na klabu ya Vijana ‘City Bulls', kabla ya kwenda Canada mwaka 2018.

Baada ya kuingia mkataba wa miaka minne na chuo kikuu cha Brigham Young University (BYU) ambacho timu yake inashiriki Ligi daraja la kwanza ya mpira wa kikapu nchini Marekani (NCAA Division I), Mtanzania, Atiki Ally amesema hatua aliyofika ni ngumu zaidi kuliko alikotoka.

Atiki ambaye amepata ofa ya kimasomo kwenye chuo hicho baada ya kufanya vizuri nchini Canada alipokuwa high scchool, kwenye shule ya  Thames Valley District School Board na kucheza katika timu ya London Basketball Academy ya nchini humo amewaomba Watanzania kumuombea ili avuke hatua hiyo na hatimaye kucheza Ligi maarufu ya NBA.

"NCAA ni kugumu, huko ndiko wachezaji wa NBA wanaandaliwa, inabidi kupambana zaidi, Watanzania waniombee na mimi sitowaangusha," amesema Atiki ambaye anatarajia kuanza maisha mapya nchini Marekani mwezi Juni.
Kocha wa Atiki, Bahati Mgunda amesema ukiachana na kusoma bure, Atiki ametanguliza mguu mmoja kucheza ligi maarufu ya NBA.

"Chuo alichoingia nacho mkataba kina timu inacheza NCAA Division I, hii ni Ligi kule Marekani ndiyo inatoa nyota wanaocheza kwenye NBA, Atiki kama atapambana muda wowote anaweza kuchaguliwa kucheza NBA," anasema Mgunda.

Amesema hiyo ni hatua kubwa kwa Mtanzania huyo, ingawa 'focus' ya Atiki sasa ni shule na kisha kupambana ili aweze kupata nafasi ya kucheza NBA.

"Kucheza NCAA sio jambo jepesi kabisa, ni hatua kubwa sana kwa Atiki, apambane ili kuonekana zaidi na kupata nafasi ya kucheza NBA ili atimize ndoto zake na kuitangaza nchi yetu," anasema.

Kama atafanikiwa, Atiki atakuwa Mtanzania wa pili kucheza kwenye Ligi hiyo, awali Hasheem Thabeet aliwahi kupata nafasi hiyo.