Ajibu gari limewaka, atulizwa

KIWANGO cha mshambuliaji mpya wa Azam, Ibrahim Ajibu kimewaibua mastaa wa soka na kusema mchezaji huyo ana kiwango kizuri lakini yeye mwenyewe ndio anajichelewesha kwenye kufanya kazi yake vizuri.

Ajibu amejiunga na Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuvunja mkataba na Simba.

Mshambuliaji huyu alianza kucheza kombe la Mapinduzi na uwezo wake ambao ameuonyesha kwenye mashindano hayo imewafanya wapenzi wa soka wamshike sikio na kutaka ajitambue ili aendelee kuwa kwenye ubora mkubwa zaidi ya sasa.

Katika mchezo wa juzi kwenye fainali ya kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba, Ajibu alikuwa kiungo mwenye ubora wa kusambaza mipira kwenda langoni kwa wapinzani wake.

Ajibu alionyesha utulivu wa kukaa na mpira na pasi zake fupi na ndefu kuhakikisha mipira inasonga mbele lakini pia staili yake ya kupiga mipira mirefu.


WADAU WAFUNGUKA

Mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema Ajibu ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini kuna muda anakuwa kama hajitambui kwenye kuendeleza kipaji chake.

Mogella alisema matatizo ya Ajibu hayajaanza leo, lakini yeye mwenyewe hajataka kubadilika na kama atakubali kubadilika basi atakuwa kwenye ubora zaidi ya sasa.

“Ajibu ana ubora wa zaidi anachokifanya sasa, shida anacheza na kuona kama tayari ameshamaliza, mfano Morisson yeye ni mchezaji mzuri lakini bado hatosheki na akiwa uwanjani anafosi kwenye kupeleka mashambulizi mbele na sio kupiga pasi tu,” alisema Mogella.

Upande wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Herry Morris alisema: “Sikutegemea kiwango kizuri kutoka kwa Ajibu ambacho amekionyesha, anatakiwa ajitambue na awe siriazi na kazi yake basi atazidi kuwa bora.”