Agosto yaipa faida Namungo

Dar es Salaam. Takwimu zisizovutia za Primiero De Agosto pindi inapokuwa ugenini, zinawapa nguvu wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Namungo katika mchezo wa kwanza baina yao utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, leo jioni.

Licha ya mafanikio ya Agosto katika miaka ya hivi karibuni, timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi huko Angola imekuwa haifanyi vizuri mara kwa mara pindi inapokuwa ugenini kulinganisha na inapocheza katika ardhi ya nyumbani.

Katika mechi zao 10 walizocheza ugenini kwenye mashindano ya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni, wameibuka na ushindi mara mbili, kutoka sare nne na kupoteza mechi nne, wakipachika mabao 10 huku wakiruhusu nyavu zao zitikiswe mara 14 hivyo wana wastani wa kuruhusu bao moja katika kila mchezo na pia kufunga bao moja.

Lakini wakati Agosto wakiwa na takwimu dhaifu pindi wawapo ugenini kwenye mashindano ya kimataifa, Namungo wenyewe japo wamecheza mechi chache za kimataifa, wana historia ya kutumia vyema ardhi ya nyumbani ambapo wameibuka na ushindi katika mechi zote mbili za raundi zilizopita ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al Rabita ya Sudan Kusini na mchezo mwingine walicheza dhidi ya El Hilal El Obeid ya Sudan ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Timu itakayopata matokeo mazuri katika mchezo huo wa leo na ule wa marudiano ambao pia utachezwa katika Uwanja wa Azam Complex, keshokutwa Jumatano, itajihakikishia kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika.

Namungo na Agosto zitalazimika kucheza mechi zote mbili za hatua ya mchujo hapa Tanzania katika Uwanja wa Azam Complex, kutokana na uamuzi uliotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) baada ya mechi baina ya kwanza baina ya timu hizo iliyopangwa Angola kushindwa kufanyika.

Mechi hiyo ya ugenini ambayo Namungo hawakucheza licha ya kusafiri hadi Angola, haikuchezwa baada ya msafara wa Namungo kuwekwa arantini kutokana na wachezaji wake watatu, Lucas Kikoti, Hamis Fakhi na Fred Tangalu kudaiwa walibainika na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 sambamba na mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Omary Kaya.

Ni fursa muhimu kwa Namungo FC kujiweka katika nafasi nzuri ya kuandika historia kubwa katika medani ya soka nchini ya kuwa timu ya kwanza kufika hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza.

Licha ya Simba na Yanga kuwahi kuingia hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika kwa nyakati tofauti, hazikufanya hivyo zikiwa zinashiriki kwa mara ya kwanza na badala yake zilisubiri kwa muda mrefu ndipo zikafanya kitu kama hicho.

Namungo katika mchezo wa leo itawakosa Kikoti, Fakhi na Tangalu ambao wako Angola lakini pia hawatokuwa na majeruhi wa muda mrefu,

Blaise Bigirimana lakini nafasi zao huenda zikazibwa na Erick Kwizera, Khamis Khalifa, Reliants Lusajo na Nzigamasabo Styve.

Kocha wa Namungo FC, Hemed Morocco alisema timu yake iko tayari kuvaana na Primiero De Agosto na ana imani kubwa watawatupa nje Waangola hao.

“Sisi tuko vizuri na tunaendelea na maandalizi yetu kwa ajili ya kuwakabili Agosto. Tunatambua ni timu kubwa na nzuri lakini tunaamini kwa namna tulivyojiandaa tutapata matokeo mazuri dhidi yao na kuwatoa mashindanoni,” alisema Morocco.

Katibu wa Namungo, Ally Selemani alisema kuwa kwa upande wa uongozi, maandalizi yote yamekamilika.