Zimeupiga mwingi nyumbani

Muktasari:

IKIWA Ligi Kuu Bara msimu huu inaelekea ukingoni, tunakuleta uchambuzi kuhusu timu zilivyotumia vyema viwanja vyake vya nyumbani hadi sasa.

IKIWA Ligi Kuu Bara msimu huu inaelekea ukingoni, tunakuleta uchambuzi kuhusu timu zilivyotumia vyema viwanja vyake vya nyumbani hadi sasa.

Msimamo wa timu zote 18 zinazoshiriki ligi hiyo pamoja na matokeo yake ya mechi za nyumbani pekee uko hivi.


AZAM FC

Azam ndiyo kinara wa mechi za nyumbani ikiwa na pointi 34 imecheza mechi 15 nyumbani na kushinda 10, sare nne, 0-0 dhidi ya Prison, 2-2 dhidi ya Ruvu, 2-2 dhidi ya Namungo, na 1-1 dhidi ya JKT Tanzania na kupoteza moja pekee dhidi ya Yanga kwa kufungwa bao 0-1.

Ugenini Azam imeshinda mechi saba, ikitoa sare tano na kupoteza mechi tatu, 1-0 dhidi ya Mtibwa, 1-0 dhidi ya KMC na 2-1 dhidi ya Coastal Union.


SIMBA

Simba inashika nafasi ya pili kwa mechi za nyumbani pekee ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 13 za nyumbani. Wameshinda 10, sare mbili dhidi ya Azam (2-2) na Polisi Tanzania (1-1) na kupoteza moja kwa kulala 0-1 dhidi ya ‘Wazee wa Kupapasa’ Ruvu Shooting.

Simba inaongoza kushinda mechi za ugenini ikiwa imeshinda mechi 11, sare mbili dhidi ya Mtibwa na Yanga na kupoteza moja dhidi ya Prisons.


YANGA

Wanashika nafasi ya tatu na pointi 32, kwenye mechi za nyumbani wakiwa wameshinda mechi tisa, sare tano, 1-1 dhidi ya Prisons, 1-1 mbele ya Simba, 1-1 dhidi ya Namungo, 3-3 na Kagera, sare ya 1-1 dhidi ya KMC huku ikipoteza moja kwa kulala 0-1 kwa Azam kwa bao lile la kideoni la Prince Dube.

Pia ugenini Yanga imeshinda mechi tisa, ikitoa sare tano na kupoteza moja kwa kufungwa bao 2-1 na Coastal Union.


IHEFU

Ihefu ipo nafasi ya nne na alama 32 ikiwa imecheza mechi 17 nyumbani na kushinda 10, sare mbili na kupoteza tano kwa kufungwa 0-1 na Biashara, 0-2 dhidi ya Gwambina, 0-3 dhidi ya Yanga, 0-2 dhidi ya Azam na 0-2 mikononi mwa Mtibwa.


KMC

KMC nayo ni miongoni mwa timu tano zilizotumia vyema uwanja wa nyumbani ikikusanya pointi 29 ikiwa imecheza mechi 13 nyumbani ikishinda tisa, sare mbili na kupoteza mbili 1-2 dhidi ya Yanga na 0-1 dhidi ya Polisi Tanzania.


BIASHARA UNITED

Biashara ni ya sita ikiwa ni timu ngumu kufungika nyumbani kwake, imevuna alama 28 nyumbani ikishinda mechi nane 8 nyumbani, sare nne na kupoteza tatu, 0-1 dhidi ya Yanga, 0-1 dhidi ya Simba na 0-1 dhidi ya Coastal.


KAGERA SUGAR

Kagera inashika nafasi ya saba ikiwa Uwanja wake wa Kaitaba imevuna pointi 27, kwenye mechi 16 za nyumbani ikishinda nane, sare tatu na kupoteza tano kwa kufungwa 0-2 na Simba, 0-1 na Namungo, 1-2 na Mbeya City, 0-1 na Yanga na 0-1 na JKT Tanzania.


MTIBWA SUGAR

Mtibwa inakuwa ya tisa kwani hadi sasa imecheza mechi 17 nyumbani na kuvuna alama 26 kwa kushinda saba, sare tano na kupoteza tano ikifungwa bao 0-1 na Yanga, 0-1 na Coastal Union, 0-1 na Dodoma Jiji, 0-2 na Gwambina na 1-2 na Polisi Tanzania.


RUVU SHOOTING

Wazee wa kupapasa wapo nafasi ya 10 na alama 24 wakiwa wamecheza mechi 13 nyumbani na kushinda saba, sare tatu na kupoteza tatu, 0-3 dhidi ya Simba, 0-2 dhidi ya Dodoma Jiji na 0-3 dhidi ya Ihefu.


TANZANIA PRISONS

Makamanda wa Pira Gwaride wanakuwa wa 11 na pointi 24. Katika uwanja wao wa Nelson Mandela Sumbawanga wamecheza mechi 14 na kushinda saba, sare tatu na kupoteza nne dhidi ya Azam 0-1, Polisi 0-1, Kagera 0-1 na Dodoma Jiji 0-1.


NAMUNGO

Namungo wanashika nafasi ya 12 na alama 24 kwani hadi sasa wamecheza mechi 15 kwenye uwanja wao na kushinda mechi sita, sare sita na kupoteza tatu, 0-1 dhidi ya Polisi, 0-1 dhidi ya Mbeya City na 1-3 dhidi ya Simba.


COASTAL UNION,

Wagosi wa Kaya wanasimama nafasi ya 12 na alama 24, wamecheza mechi 15 nyumbani wakishinda sita, sare sita na kupoteza tatu kwa kufungwa 0-1 dhidi ya Polisi Tanzania, 0-2 dhidi ya Mtibwa Sugar na 0-7 dhidi ya Simba.


DODOMA JIJI

Hawa wanashika nafasi ya 13 kwani katika mechi 14 walizocheza nyumbani msimu huu wameshinda sita, sare tano na kupoteza tatu, 0-1 dhidi ya Polisi, 1-2 dhidi ya Simba 2-1 na Namungo 1-0.


JKT TANZANIA

JKT wanakaa nafasi ya 14 wakiwa na alama 20, wamecheza mechi 15 nyumbani hadi sasa wameshinda mechi sita, sare mbili dhidi ya Tanzania Prisons 1-1, na Polisi Tanzania 1-1 huku wakipoteza mechi saba.


POLISI TANZANIA

Uwanja wa nyumbani kwa Polisi umekuwa si kitu kwani hadi sasa wamecheza mechi 14 na kushinda nne pekee dhidi ya Dodoma Jiji 3-0, Mtibwa 1-0, KMC 1-0 na Namungo 2-0 huku ikipoteza mechi nne na kutoa sare sita nyumbani, wanashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa mechi za nyumbani.


MBEYA CITY

Wanashika nafasi ya 16 na alama 16, wameshinda mechi tatu tu hadi sasa kati ya 13 walizocheza nyumbani msimu huu, 0-1 dhidi ya Mwadui, 0-6 dhidi ya JKT Tanzania na 0-2 dhidi ya Ruvu Shooting na kutoa sare saba huku wakipoteza tatu.


GWAMBINA

Ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiriki Ligi Kuu, wanashika nafasi ya 17 na alama 14 wakiwa wamecheza mechi 15 na kushinda tatu tu, 2-0 dhidi ya Ihefu, 2-0 dhidi na Mtibwa na 4-0 dhidi ya Coastal, sare saba na kupoteza tano.


MWADUI

Tayari wameshuka daraja lakini kabla hawajamaliza ligi mechi za nyumbani pia ndiyo inashikililia mkia kwa kuwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 16 nyumbani ikishinda tatu dhidi ya Dodoma Jiji 1-0, Mbeya City 2-0 na Ihefu 2-0 sare nne na kupoteza nane.