Wataweza? mastaa hawa wapo mtegoni Ligi Kuu

WAKATI dirisha dogo la usajili la Ligi mbalimbali nchini likifungwa rasmi Januari 15 baada ya kila klabu kuboresha kikosi chake kutokana na mapungufu yaliyoonekana, yapo majina yenye wasifu mkubwa ndani na nje ya nchi ambayo hutazamwa kwa jicho la tatu.

Baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara zilishusha vifaa vyao vipya, huku wengine wakiongezewa mikataba ili kujiweka sawa kwa ajili ya mzunguko huu wa pili ulioshika kasi.

Mwanaspoti linakuletea majina ya nyota kadhaa waliosajiliwa dirisha hili kwenye Ligi Kuu Bara wanaotazamwa kuzibeba timu zao kutokana na wasifu wao.


JEAN BALEKE (SIMBA)

Amejiunga na Simba akitokea Nejmeh SC ya Lebannon alikokuwa anaitumikia kwa mkopo akitokea TP Mazembe. Baleke ametua Simba huku mashabiki wakiwa na matarajio naye makubwa hususan eneo la ushambuliaji wakati wa michuano mbalimbali ya ndani na ile ya kimataifa kutokana na uzoefu wake licha ya kuwa na umri wa miaka 21 tu.

Msimu wa 2020/21, Baleke aliibuka kinara wa ufungaji bora akiwa na TP Mazembe baada ya kufunga mabao 14 nyuma ya nyota, Fiston Mayele aliyefunga 13 wakati huo akiitumikia AS Vita ya Congo kisha kuwashawishi mabosi wa Yanga kunasa saini yake.


KENNEDY MUSONDA (YANGA)

Tayari ameonja utamu wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho kipya kwake dhidi ya Ihefu Januari 16 tangu alipojiunga dirisha dogo akitokea Power Dynamos ya nchini Zambia aliyokuwa anaichezea.

Musonda ni mshambuliaji anayetazamwa kuleta ushindani na mchezaji wenzake, Mayele ambaye kwa upande wake ameshaonyesha ni hatari kiasi gani kuzifumania nyavu kwani hadi sasa ndiye kinara akiwa na mabao 15 ya Ligi Kuu Bara.

Wakati anaondoka Power Dynamos, Musonda alifunga mabao 11 akiwa ndiye kinara kisha kutua Yanga badala ya TP Mazembe ambayo nayo ilikuwa kwenye rada za kuinasa saini yake kabla ya Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said kufanya umafia.


ABDULAI IDDRISU (AZAM FC)

Licha ya Azam FC kumsajili kipa Mcomoro, Ali Ahamada mwenye uzoefu na soka la Afrika ila bado ameonekana kushindwa kabisa kuendana na kasi ya ushindani kutokana na kile ambacho kinaonekana wazi kuruhusu mabao ya uzembe yanayowagharimu.

Baada ya hilo mabosi wa kikosi hicho walitua hadi nchini Ghana kwa ajili ya kupata saini ya kipa, Abdulai Iddrisu ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia matajiri wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kuachana na klabu yake ya Bechem United.

Msimu wa 2021/2022, Iddrisu alicheza michezo 31 na kutengeneza Clean Sheets 18 akiwa ni kipa wa kwanza kutoruhusu bao kwenye michezo saba mfululizo ya msimu na kupewa tuzo ya kipa bora akiwashinda, Ibrahim Danlad wa Asante Kotoko na Jojo Walcott wa Chalton Athletics.


ISMAEL SAWADOGO (SIMBA)

Sawadogo ambaye ni raia wa Burkina Faso amesajiliwa akitokea klabu ya Difaa El Jadida ya nchini Morocco huku mashaka makubwa kwa wadau wengi wa soka ni kutokana na nyota huyo kutocheza michezo ya ushindani tangu Februari mwaka jana.

Katika kulithibitisha hilo kwenye kikosi cha Difaa El Jadida alicheza michezo tisa tu akitumia dakika 581 ingawa haina maana anaweza akashindwa kufanya vizuri japo takwimu zake ndizo ambazo zinaleta wasiwasi kwa mashabiki wa Simba.


NELSON OKWA (IHEFU)

Okwa ni miongoni mwa viungo washambuliaji waliotarajiwa kufanya makubwa akiwa na Simba iliyomsajili msimu huu akitokea Rivers United ya nchini kwao Nigeria baada ya kuonyesha kiwango kizuri ingawa mambo yamekwenda kombo kwa staa huyo.

Okwa ambaye alikuwa anaaminika ni mbadala wa Clatous Chama ameshindwa kabisa kuingia kikosi cha kwanza tangu alipokuwa, kocha Zoran Maki, Juma Mgunda na sasa Robert Oliviera ‘Robertinho’ hivyo viongozi kumtoa kwa mkopo Ihefu FC ili kunusuru kipaji chake.

Hakuna asiyejua presha iliyopo kwa klabu hizi mbili kubwa nchini za Yanga, Simba hivyo licha ya kushindwa kuwika huko na kuonyesha makali yake kutokana na ushindani wa namba huenda Ihefu ikamfanya kurejesha matumaini mapya kwa mabosi wake.


YUSUPH ATHUMAN (COASTAL UNION)

Ushindani wa namba ndani ya Yanga umemfanya Yusuph kuomba kutolewa kwa mkopo kwenda Coastal Union ili kunusuru kipaji chake hasa ukiangalia bado ni kijana mdogo ambaye ana malengo ya kufika mbali zaidi.

Kujiunga kwake na ‘Wagosi wa Kaya’ ni mtego mwingine kwake wa kuthibitisha uwezo wake kutokana na ukweli hakuna ushindani mkali wa nafasi eneo la ushambuliaji kama ilivyokuwa Yanga ambayo imekuwa na mastaa wengi wakali.

Yusuph alijiunga na Yanga Agosti 2, 2021 baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Biashara United na kusaini mkataba wa miaka mitatu.


VICTOR AKPAN (IHEFU)

Ni moja ya kiungo aliyeziingiza vitani klabu kubwa hapa nchini ili kupata saini yake lakini ni Simba ambayo ilifanikiwa kumnasa akitokea Coastal Union msimu huu baada ya kuonyesha kiwango kizuri huku ikielezwa alijiunga kwa kiasi cha Sh100 milioni.

Raia huyu wa Nigeria alibeba matumaini makubwa kwa Wanasimba lakini kadri ambavyo siku zilizidi kwenda alishindwa kabisa kulishawishi benchi la ufundi kumtumia hivyo kuamua kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Ihefu akiungana na wenzake, Okwa.

Ni dhahiri Simba ilikuwa kina kirefu kwa staa huyu hivyo mashabiki watakuwa na kazi moja tu ya kufuatilia mwenendo wake kwani sehemu aliyopo naamini ni salama kutokana na kutokuwa na presha kubwa ya kiushindani tofauti na kule alikotoka.


FRANCY KAZADI (SINGIDA BIG STARS)

Kinachosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi ni kuona moto ukiendelea kwa Kazadi ambaye ameonyesha makali yake akiwa na kikosi hicho kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika hivi karibuni na kuibuka mfungaji bora baada ya kutupia mabao sita. Kazadi hakuwa na timu kuanzia Septemba mwaka jana tangu alipoachana na El Masry SC ya Misri ila tayari ameanza kuonyesha ni mwiba kwa makipa na sasa kinachosubiriwa ni kuona makali yake akiyahamishia kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara.


MAONI YA WADAU

Nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema; “Usajili siku zote huwa ni kamari unaweza ukamuona mchezaji anacheza vizuri huko ukamsajili ila akashindwa kufiti kwenye timu yako, yapo mambo mengi ila ninachoamini, wameshindwa kuingia katika mfumo wa benchi la ufundi.”

Kwa upande wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila anasema wachezaji wengi hushindwa kutamba kwenye klabu za Simba na Yanga kwani wanaposajiliwa wanajisahau wanaenda kukutana na waliokuwa bora yao hivyo mwisho hujikuta wanafeli.