Washkaji kinoma, ila kitaumana kwenye Dabi

Muktasari:

LINAPOKUJA suala la mechi ya Simba na Yanga kunakuwa na upinzani wa pande mbili, unaweza kudhani watu ni maadui. Lakini baada ya mechi mmojawapo anapoambulia kichapo au kutoshana nguvu vikosi vyao, basi stori zinaendelea kama kawaida.

LINAPOKUJA suala la mechi ya Simba na Yanga kunakuwa na upinzani wa pande mbili, unaweza kudhani watu ni maadui. Lakini baada ya mechi mmojawapo anapoambulia kichapo au kutoshana nguvu vikosi vyao, basi stori zinaendelea kama kawaida.

Dabi inakuwa na ushindani wa hali ya juu ambao hata wachezaji wakijuana kiasi gani, stori zitapigwa baada ya dakika 90 wakati tayari matokeo yameamuliwa nani amekuwa mbabe wa mwenzake.

Mwanaspoti linakuletea mastaa washikaji wa timu hizo, lakini wakati wa mechi ushikaji wao huuweka pembeni, ila haimaanishi kwamba urafiki unakuwa umetoweka.


MANULA vs METACHA

Kipa wa Simba, Aishi Manula ni rafiki na kipa wa Yanga, Metacha Mnata. Unataka kujua wanakutana wapi? Ipo hivi, wawili hao wote ni nguzo kwenye timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, hivyo wakikutana ni maswahiba na hupiga stori na wakiweka Usimba na Uyanga pembeni wakiutanguliza utaifa.

Lakini wanapokutana kwenye mechi ya dabi mambo huwa tofauti. Kila mtu hutetea furaha ya mashabiki wake na kulinda usalama wa timu kutofungwa.


SHIKhALO vs ONYANGO

Kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo na beki wa kati wa Simba, Joash Onyango wakiwa uwanjani kucheza dabi unaweza kudhani ni watu wasiofahamiana kabisa, lakini kumbe wanatoka nchi moja (Kenya) na ni washikaji wanaopiga stori baada ya dakika 90 za mchezo.

Hilo liliwahi kuelezwa na Shikhalo alipofanya mahojiano na gazeti hili, alipodai kuwa baada ya kuifunga Simba fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, huku Onyango akiwa amekosa penalti mojawapo zilizowanyima ubingwa alikoma kwa kutaniwa.

“Baada ya mechi nikamfuata Onyango nikamwambia kwamba unataka utukoseshe pesa kama ulivyofanya kwenye mechi tuliyotoka sare, nikacheka na kumwambia leo zamu yenu kulia. Nilidaka penalti yake, nilimsoma mwili wake ukiwa umesita kufanya uamuzi,” alisema Shikhalo.


MUGALU, TUISILA vs MUKOKO

Chris Mugalu yupo Simba. Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe wapo Yanga. Ukiwaona uwanjani wanavyopambania timu zao huwezi kuamini kama wanafahamiana au wanatoka nchi moja - DR Congo. Nje na kazi wanazungumza Kikongomani wakipiga stori na kicheko juu.


NIYONZIMA vs KAGERE

Hata isingekuwa kukutana kwenye dabi, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima wangekutana kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Rwanda. Niyonzima ndiye nahodha wa timu hiyo, hivyo Kagere angelazimika kuzungumza na kiongozi wake. Wawili hao ni washikaji.


AME vs MWAMNYETO

Mabeki Bakari Mwamnyeto wa Yanga na Ibrahim Ame wa Simba kabla ya kutua katika timu hizo walikuwa chini ya kocha wa Juma Mgunda anayeifundisha Coastal Union.

Wachezaji hao ushikaji wao umeanzia Tanga, hivyo wanapokutana baada ya dakika 90 ni washikaji wanaopiga stori.