Wanapanda ndege sana hawa Simba

UKISIKIA uzoefu basi Simba kwa sasa ina uzoefu. Msimu huu imeonekana kuwa moto Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni msimu wa tatu baada ya 2018/19 kufika robo fainali kabla ya 2019/20 kutolewa hatua za awali.

Huenda moto ilionao mwaka huu unachagizwa na moto waliopitia misimu miwili mfululizo hapo nyuma kwani wajuzi hunena ‘ili Dhahabu iwe, lazima ipite kwenye Moto’ na Wekundu hao wa Msimbazi misimu miwili hiyo waliyopita basi moto waliupata ndio maana nao sasa wako moto.

Achana na habari za msimu wa 2018/19 kufungwa jumla ya bao 12 ugenini kwenye michuano hiyo hatua ya makundi wakipigwa 5-0 na Al Ahly, 5-0 tena na AS Vita pale DR Congo, pia wakapokea 2-0 kutoka JS Saoura pale Algeria lakini walikaza na kutusua kundi hilo kwani waligeuza uwanja wa Taifa kwa sasa Mkapa kuwa machinjio yao na kuwachinja wote hao na kutinga robo fainali.

Msimu uliofuata (2019/20) walitepeta. Ni Luis Miquissone huyu huyu aliyewasulubu Al Ahly juzi kati kwa Mkapa, ndiye aliwafungashia virago msimu huo akiwa na UD Songo hatua ya awali kabisa kwenye mtoano wakitoa suluhu (0-0) nchini Msumbiji na kutoa sare ya bao 1-1 kwa Mkapa.

Bao la UD Songo lilifungwa na Miquissone dakika ya 12, huku Simba wakisawazisha kwa penati dakika za lala salama (87) kupitia kwa Erasto Nyoni matokeo yaliowaondosha Simba na UD Songo kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.

Hayo yote yalikuwa mapito magumu Simba waliyopitia wakati wakijijenga kuwa Simba wa sasa aliyemfunga AS Vita bao 1-0 ugenini kwenye dimba lile lile alilopigwa tano misimu miwili iliyopita na anayemfunga Ahly 1-0 kwa Mkapa na kucheza soka safi la kuvutia bila kupaki basi.

Hiyo ilikuwa ni historia fupi ya Simba kwenye michuano hiyo. Hata hivyo, mada kuu ni kikosi cha wanaume 11 ambao wakati Simba inapita katika moto huo walikuwepo wakiungua ili kukomaa na mpaka sasa wapo ndani ya Simba inayonolewa na kocha Gomes Da Rosa.


Aishi Manula

Ni kipa anayeonekana kuwa bora zaidi kwa sasa akifanya ‘saves’ za maana kwenye mechi ngumu za Simba. Ndiye yule yule aliyepigwa tano pale Cairo, akapokea tano Kinshasa, pia kukubali mbili pale Méridja, Algeria.

Kupitia vichapo hivyo, alijifunza, akapata uzoefu na ndiyo maana kwa sasa anaonekana bora vile, sio kwa bahati mbaya bali alijifunza.


Mohamed Hussein ‘Tshabalala’

Kama unakumbuka mechi kati ya Ahly na Simba pale Misri, Simba akifungwa 5-1, mabao yote yakifungwa kipindi cha kwanza, upande wa ‘Tshabalala’ kwa maana ya beki ya kulia Waarabu walionekana sana kuutumia kutengeneza mabao yao.

Vile vile, msimu uliopita watu walimbeza kwenye michuano hiyo mikubwa, Tshablala wa sasa si yule wa miaka miwili iliyopita ubora umeongezeka, kiufupi anacheza kibingwa.

Shomary Kapombe

Siku zote changamoto humkomaza mtu, Kapombe naye ni mmoja wa wachezaji waliokuwepo Simba misimu mitatu mfululizo ikishiriki Ligi ya Mabingwa lakini majeraha yaliyokuwa yakimwandama yalimkosesha kushiriki mechi za msimu wa 2018/19.

Msimu uliofuata alikuwa fiti na kazi yake ilionekana kila alipokuwa akipangwa kucheza jambo ambalo limemfanya kupata uzoefu zaidi na kuzidi kuwa bora kila kukicha.

Erasto Nyoni

Ukisikia mchezaji kiraka ndio huyu, kwa mara nyingi amekuwa akipangwa kucheza namba tofauti tofauti na kuzitendea kazi inavyostahili, Nyoni ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa na Simba misimu mitatu hii waliyoshiriki mfululizo Ligi ya Mabingwa na amekuwa akifanya vyema kila akipewa nafasi.


Paschal Wawa

Liwake Jua ama inyeshe Mvua, kwa jumla tangu aanze kucheza soka huu ni mwaka wa tano sasa kushiriki michuano hiyo hivyo ni mzoefu mzuri na mkomavu.

Wawa amekuwa nguzo ya msingi eneo la ulinzi la Simba. ameshiriki na Simba kwenye misimu yote mitatu ya hivi karibuni ambayo kikosi hicho kimecheza na ameonekana kuwa imara zaidi hususan mwaka huu.

Jonas Mkude

Akiwa mchezaji aliyekaa Simba kwa miaka mingi zaidi kuliko wenzake (10) Mkude amekuwa akisimamia vyema eneo la kiungo bila kutikiswa na mtu yeyote.

Licha ya kwamba kwa mwaka huu hajacheza mechi hata moja ya michuano hiyo lakini misimu miwili iliyopita alikuwa moja ya wachezaji walioisaidia Simba kufika hapa ilipo.


Mzamiru Yassin

Haimbwi sana lakini kazi yake akiwa ndani ya jezi ya Msimbazi si mchezo. Mzamiru ni moja kati ya wachezaji 11 waliopo Simba msimu huu ambao walishiriki mapambano ya Ligi ya Mabingwa katika misimu miwili mfululizo iliyopita na mpaka sasa yupo na anakiwasha.


Clatous Chama

Kwa sasa huwezi zungumzia kikosi cha Simba ukasahau kumtaja Mzambia huyu, Chama kwa misimu mitatu hii aliyokaa Simba amejitofautisha na wachezaji wengi wa kigeni waliopita pale Msimbazi, misimu miwili iliyopita kwenye michuano hiyo Chama alikuwepo na aliisaidia sana Simba.


Said Ndemla

Hapo kati watu walimbeza huku wengine wakitaka aondoke Simba kwa kigezo cha kutopata nafasi ya kucheza muda mwingi, uvumilivu umekuwa silaha ya ukuaji wake. Leo hii Ndemla akiwa dimbani Wanasimba hawana mashaka naye na ameshiriki misimu yote mitatu Simba iliyocheza Ligi ya Mabingwa Afrika.


Meddie Kagere

Moja ya majina ambayo makipa wengi wanayaogopa ni hili la Kagere. Kagere anajua kufunga na ndio silaha tegemeo pale Msimbazi kwa misimu miwili iliyopita ya Ligi ya Mabingwa kwa Simba. Kagere anashiriki ligi hiyo kwa mara ya tatu sasa akiwa na Simba.

Hassan Dilunga

Kwa mara nyingi Simba wamekuwa wakimtumia kama Winga licha ya kwamba ana uwezo pia wa kucheza eneo la kiungo mshambuliaji kwa ufasaha. Dilunga ni miongoni mwa mastaa wa Simba ambao wapo kikosini hapo katika misimu mitatu hii ambayo wekundu wa msimbazi wameshiriki Ligi ya Mabingwa hivyo uzoefu anao wa kutosha.