Wakali wa Kariakoo derby

Muktasari:

Hii ni mara ya 106 kwa Simba na Yanga kukutana katika ligi tangu michuano hiyo ilipoanzishwa 1965.

UKONGWE una raha yake, unapokuwa na timu yenye vijana wengi halafu mpinzani wako ana wakongwe wengi unaweza ukafungwa kwa sababu ya uzoefu.

Kuelekea mtanange wa Kariakoo Derby, utakaopigwa leo Jumamosi pale Kwa Mkapa kila timu inajivunia lundo la wachezaji waliocheza mechi nyingi za dabi kwenye vikosi vyao.

Wachezaji hawa wanatazamwa kama sehemu muhimu ya mchezo huu kwa sababu uzoefu wao unaweza kuwa chachu ya timu zao kufanya vizuri.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya wachezaji waliocheza mechi nyingi za dabi kutoka timu zote mbili na hadi sasa wanaendelea kucheza.


MKUDE - SIMBA

Mkude alipandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2012 akitokea timu ya vijana ‘Simba B’. Ni mchezaji pekee ambaye amedumu hadi sasa akicheza kwa miaka tisa.

Kutokana na muda mrefu aliotumia kwenye viunga vya Msimbazi, nyota huyo anaonekana kucheza mechi nyingi zaidi za ligi za watani kuliko mchezaji mwingine kwenye kikosi chao.

NDEMLA - SIMBA

Kiungo Said Ndemla ni miongoni mwa vijana waliolelewa kwenye timu ya vijana Simba B kabla ya kupandishwa mwaka 2013 kama ilivyokuwa kwa Mkude.

Mechi nyingi alicheza akitokea benchi, lakini kukaa kwake muda mrefu kunamfanya kuwa mchezaji aliyecheza nyingi zaidi kulinganisha na wengine.

NIYONZIMA - YANGA

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mnyarwanda Haruna Niyonzima huu ni msimu wake wa tisa kucheza Ligi Kuu Bara na amecheza dabi kibao.

Niyonzima amecheza timu zote, Simba na Yanga, alipotoka Simba alirudi kwao na baadaye kurejea Yanga. Kwa sasa hapati sana nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza lakini bado anabaki kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi za derby na timu zote mbili.

Alitua Yanga mwaka 2011 akitokea APR na kudumu kwa miaka saba kisha kwenda Simba alikocheza msimu mmoja, alifanikiwa kuwa sehemu ya mechi iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.


TSHABALALA - SIMBA

Beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ huu ni msimu wa saba kwenye Ligi Kuu akiwa na Simba tangu ajiunge nayo mwaka 2014, akitokea Kagera Sugar.

Tshabalala amekuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha kwanza kwa zaidi ya misimu mitatu akiwa amecheza zaidi ya dabi tano. Ana asilimia nyingi za kucheza kwa sababu ndiye beki tegemeo kwa sasa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

KASEKE - YANGA

Mwaka 2015, Kiungo Deus Kaseke alijiunga Yanga akitokea Mbeya City, alicheza miaka miwili kisha kutimkia Singida United ilipopanda daraja msimu wa 2017/18.

Akiwa Yanga alicheza mechi ya dabi na baada ya kushindwa maisha ya Singida United ambayo imeshuka daraja alirudi Yanga anakotumika hadi sasa. Misimu minne aliyokaa Yanga, hii itakuwa derby ya 11 kukutana nayo iwe kucheza ama kutoicheza.


Bocco, Nyoni, Manula na Kapombe - Simba

Nyota wanne wa Simba waliotoka Azam FC kwa wakati mmoja, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni na John Bocco wameitumikia timu hiyo misimu mitatu ingawa Kapombe msimu wake wa kwanza hakuanza vizuri kutokana na majeraha.

Tangu wamejiunga Simba zimechezwa jumla ya dabi saba za Ligi Kuu hii inatazamiwa kuwa dabi yao ya saba, ikiwa watapata nafasi ya kucheza.