Waamuzi, ratiba vilitibua uhondo wa Ligi Kuu 2020-21

KUNA mambo ambayo yatabaki kumbukumbu mbaya za msimu huu wa 2020/2021 ulioishia leo.

Kati ya hayo ni kutibuliwa kwa ratiba huku pia waamuzi wakichangia kupunguza uhondo wa ligi.

Nyota mbalimbali wa zamani wamevunja ukimya na kuonyesha wasiwasi wao katika nafasi hizo mbili na kushauri ziboreshwe msimu ujao.


Mosses Mkandawile

Kipa huyu nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars anasema ratiba ya msimu huu ilikuwa na utata.

“Timu moja kuwa na viporo vingi ilikuwa kikwazo msimu huu,” anasema Mkandawile.

Anasema ili kuondoa mkanganyiko wa ratiba na kusingizia mechi za kimataifa, waratibu wapange ratiba ya Ligi kwa kuangalia kalenda ya kimataifa.

“Ratibaya Ligi ilipunguza uhondo msimu uliokwisha, Ligi inapaswa kuwa na uwiano sawa wa mechi kati ya timu na timu, lakini timu nyingine inapokuwa na viporo vingi ina ‘take advantage’,” anasema.

Anasema marefa wengi walichangia kupunguza utamu wa Ligi na kushauri msimu ujao wapewe mafunzo kabla ya ligi kuanza.

“Waamuzi pia ilikuwa ni changamoto msimu huu, wengi hawakumudu kutafsiri sheria za soka, msimu ujao wapewe semina, sheria ya 17 na zisizungumzwe kwa mdomo tu, zifanywe kwa vitendo uwanjani.

“Kuna waamuzi walionekana hata sheria mpya za FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), hawajazielewa, hivyo msimu ujao waanze kwanza kupewa semina kabla ya Ligi Kuu kuanza,” anasema Mkandawile.


Fikiri Magosso

Nyota huyu wa zamani wa Simba anasema ligi imefanyika kwa kiwango bora, japo kulikuwa na changamoto hasa kwenye ratiba.

“Lakini pia mzunguko wa pili ushindani ulipungua tofauti na ligi ilivyoanza kwenye mechi za mzunguko wa kwanza.

“Hii imefanya ushindani kuhamia kwenye vita ya kuepuka kushuka daraja, timu zaidi ya nane kusikilizia matokeo ya mechi za mwisho,” anasema.

Anasema kwenye timu zilizomaliza zikiwa nafasi za juu zilistahili hasa Simba iliyotwaa ubingwa.

“Simba ilistahili ubingwa ambao umechangizwa na ushiriki wao wa kimataifa ambako kuliwaongezea hamasa, Yanga sijui nini kiliwapata mzunguko wa pili, lakini ilianza vizuri na matokeo yao ya mzunguko wa kwanza yaliongeza presha kwa Simba na kunogesha upinzani,” anasema.


Malota Soma

Mchezaji huyu wa zamani wa Simba na Taifa Stars anasema ratiba ya msimu wa 2020/2021 haikutendewa haki.

“Ligi ilianza vizuri, kulikuwa na ushindani mzunguko wa kwanza, lakini ratiba haikutendewa haki,” anasema.

Anasema duniani kote hakuna Ligi Kuu ambayo timu inakuwa na viporo vitano na zaidi.

“Mechi za viporo sana zikizidi ni viwili, lakini viporo vitano ni utaratibu mbovu ambao msimu huu kiukweli ulipunguza amsha amsha ya Ligi Kuu.

Anasema msimu ujao katika upangaji ratiba, mechi za kimataifa zizingatiwe na timu moja isiwe na viporo vingi kwa kigezo kuwa inacheza kimataifa.

“Kama timu inacheza kimataifa baada ya wiki mbili, katikati ya muda huo icheze mechi mbili ili kupunguza gepu, lakini timu kuwa na viporo vitano, hii sijawahi kuisikia nchi zingine ni hapa kwetu tu, msimu ujao hilo liangaliwe.”.


Ally Mayay

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay anasema msimu uliokwisha timu zilizoingia kweye kinyang’anyiro cha ubingwa zilianza kuoekana mapema kuanzia mzunguko wa 25.

“Hili linapaswa kuwa funzo kwa msimu ujao, makocha na viongozi na hata wachezaji wajifunze kutokana na makosa ya msimu huu na bahati nzuri msimu ujao, klabu zitakuwa na uwezo kujiendesha hata kama sio kihivyo, lakini pesa itakuwepo.

“Kingine mabenchi ya ufundi yalikuwa ni changamoto mzunguko uliopita, japo hii ni changamoto ya muda mrefu katika soka letu, lakini msimu ujao tunapaswa kubadilika.

“Kwani ukifuatilia ni benchi lipi lilipewa nafasi ya kusajili kwa asilimia angalau 70, hayawezi kuzidi matatu, msimu ujao makocha wahusike kwa kusajili angalau kwa asilimia 70 ili hata ikitokea kiwango kibovu tumlaumu,” anasema Mayay.

Anasema msimu wa 2020/2021 makocha wengi walitupiwa lawama kwa makosa ambayo si yao, wengi walisajiliwa timu na viongozi lakini kwenye ubora wa wachezaji na ubora wa timu wao ndiyo walitupiwa lawama.


Sanifu Lazaro ‘Tingisha’

Nyota huyu wa Yanga na Taifa Stars anasema, msimu wa 2020/2021 ulianza kwa kuonyesha utakuwa na ushindani, lakini kibao kiligeuka katika mechi za mzunguko wa pili.

“Mzunguko wa kwanza ulikuwa na ushindani, lakini mzunguko wa pili timu nyingi ziliaonekana kuanza kupotea.

“Hata wachezaji walioanza kufunga mzunguko wa kwanza, mzunguko wa pili hawakuonekana kucheza kwa ‘perfomance’ ile ile, hivyo mzunguko ujao, makocha waliangalie hilo,” anasema.