Ukweli ni upi matumizi ya Kahata ndani ya Simba

FRANCIS Kahata, ni nyota raia wa Kenya anayekipiga kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara ambao ni wawakilishi wa nchi kwenye michuano mikubwa Afrika ya Ligi ya Mabingwa, Simba.

Alisajiliwa Simba akiwa kwenye kiwango bora kabisa ambapo alipata nafasi ya kucheza na kuonyesha kile alichokuwa nacho ingawa kadri siku zinavyozidi kwenda nafasi yake ilianza kupotea, hakuwa Kahata yule aliyetua akitokea Gor Mahia.

Msimu uliopita ndiyo hasa alianza kuondoka kwenye ramani na hata msimu ulipomalizika alitabiriwa kuwa huenda wangeachana naye ama kumtoa kwa mkopo wakati wa dirisha dogo, lakini bado anadunda tu ndani ya Simba.

Nilikuwepo kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyomalizika Visiwani Unguja, Zanzibar ambapo Yanga ilitwaa ubingwa huo huku Simba ikishika nafasi ya pili.

Simba na Yanga walikutana kwenye fainali hizo ambapo bingwa alipatikana kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 90 kutoshana nguvu kwa kutofungana.

Katika mashindano hayo, Kahata aliibuka Mchezaji Bora kwenye mechi yao walipocheza na Mtibwa Sugar ambapo alizawadiwa Sh200,000 huku akitwaa tuzo nyingine ya Mchezaji Bora wa mashindano akizawadiwa Sh4 milioni.

Kahata ni mchezaji mzuri na muhimu ndani ya Simba, labda hapati nafasi kutokana na aina ya mfumo wa makocha na kumuweka benchi, lakini sio kwamba ni mchezaji mbovu hadi kuingia kwenye tetesi za kutaka kutolewa kwa mkopo.

Hata hivyo, kinachowapa hofu wadau wa soka ni juu ya usajili unaoendelea ndani ya Simba hasa kwa wachezaji wa kigeni ingawa uongozi unadai kwamba hawajakata mtu.

Simba wanaendelea na usajili huo kwa ajili ya michuano ya kimataifa ambao utafungwa Januari 31, mwaka huu, lakini mashaka yapo kwa nyota mpya Perfect Chikwende kutoka FC Platinum ambaye kanuni hazimruhusu kucheza hatua ya makundi kwani tayari ameshiriki michuano hiyo na timu yake ya zamani.

Maswali ndipo yanapoibuka kwamba Chikwende amekuja Simba kuchukua nafasi ya mtu ili acheze mechi za Ligi Kuu Bara au atakuwepo tu mpaka msimu mpya utakapoanza kama hajasajiliwa kwa ajili ya ligi ya ndani.

Na kama amesajiliwa kwa ajili ya ndani, basi Simba itakuwa imefikisha idadi ya nyota 11 wa kigeni kwani walipomsajili Taddeo Lwanga kujaza nafasi ya Mbrazil Gerson Fraga walikuwa 10 - idadi ambayo inaruhusiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hapo ndipo hofu ya uwepo wa Kahata ndani ya Simba inapoanzia ila ni kwamba hawajamkata na ndiye ambaye jina lake lipo Caf kwa ajili ya michuano hiyo, hivyo atalazimika kuwepo kushiriki michuano hata kama hatapata nafasi ya kucheza, lakini Je Chikwende atacheza ligi ipi?

Simba wanapaswa kutueleza ukweli kama Kahata ameondolewa kwenye usajili wa wachezaji wa kucheza ligi ya ndani ili Chikwende acheze ama hili likoje au labda Chikwende atacheza mashindano gani na kwa kanuni zipi, huenda hapa wakitusaidia kutufafanulia itawasaidia wengi kwamba Simba hawana baya.

Simba hawajamaliza, yaani bado sana kukamilisha ile idadi ya wachezaji 10 kwa ajili ya mashindano haya hasa wanapigania kuvuka hatua ya makundi hivyo wanataka kuwa na kikosi imara na kipana zaidi, hivyo tutarajie kuwaona nyota wengine watakaosajili, ila wanapaswa kusaka wale ambao hawajashiriki michuano hiyo sasa ili pengine isiwe kama Chikwendwe wa kucheza ligi ya ndani.

Mashabiki na wadau wa soka nchini nadhani tunahitaji utulivu na kuona ni namna gani Simba watapanga kikosi chao hasa kwa kuzingatia huu usajili wao mpya kwa wachezaji wa kigeni, pia kufahamu zaidi matumizi ya Kahata na Chikwende kwenye mashindano hayo yote.