UCHAMBUZI: Wa kimataifa muwe watulivu, mjipange vyema

Muktasari:

LIGI Kuu Bara imemalizika, bingwa wakiwa ni Simba ambao wametetea kwa mara ya nne mfululizo na dirisha la usajili nalo limefunguliwa rasmi.

LIGI Kuu Bara imemalizika, bingwa wakiwa ni Simba ambao wametetea kwa mara ya nne mfululizo na dirisha la usajili nalo limefunguliwa rasmi.

Usajili huo unazihusu timu zote za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (FDL) na Ligi ya Wanawake (WPL).

Lakini katika usajili huo wengi wanaangalia zaidi timu za Ligi Kuu ambako kuna ushindani mkubwa ingawa hata ligi zingine zinao.

Baada ya ligi hizo kumalizika, waliopanda daraja wamejulikana kuwa ni Mbeya Kwanza na Geita Gold ambazo zilipanda moja kwa moja huku Pamba na Transit Camp zikisubiri mechi za mchujo ambazo zilianza jana Jumatano.

Pamba waliikaribisha Coastal Union wakati Transit Camp wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ambayo inashiriki kwa mara ya pili mfululizo kutokana na kikosi hicho kusuasua misimu ya hivi karibuni.

Hatua hiyo itamalizika keshokutwa Jumamosi, ambapo timu mbili zitashiriki Ligi Kuu msimu ujao huku mbili zikishiriki FDL kutokana na matokeo watakayoyapata katika mechi za mwisho.

Hapo pana kazi kubwa kwa timu za Ligi Luu - Coastal Union na Mtibwa Sugar kwani za FDL nazo zina hamu ya kupanda na zinaisaka nafasi hiyo muda mrefu.

Kwa upande wa timu nne ambazo zitashiriki michuano ya kimataifa baada ya Tanzania kupata nafasi nne za ushiriki wa Caf kutokana na Simba kufanya vizuri msimu uliopita, ni Simba na Yanga Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam na Biashara United watashiriki Kombe la Shirikisho barani humo.

Sasa basi, ninachotaka kugusia hapa ni juu ya usajili kwa timu zote, lakini kubwa zaidi hawa wawakilishi kwenye michuano ya kimataifa ili wasiende na vikosi vya majaribio na kuturudisha nyuma.

Misimu miwili iliyopita, Simba iliipatia Tanzania nafasi kama hii lakini ilipotokea timu zilizoshiriki zilikuwa kama wasindikizaji tu kwani zilitolewa mapema na kurudi nyuma kuwa na timu mbili pekee kwenye michuano hiyo.

Yanga na Azam FC wanaoonekana hivi kuwa na kasi ya kufanya usajili kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao, wanahaha kweli kweli ikionyesha kwamba wamepania kimataifa.

Simba hawana presha, kwanza hivi sasa ni wazoefu wanajua wpai pa kuwashika wapinzani wao pia kikosi chao bado kipo imara hata kama wanasajili basi usajili wao si wa presha kama ilivyo timu zingine.

Simba wanafanya ama watafanya usajili, lakini usajili wao sio wa kujenga timu, bali ni wa kuboresha kikosi. Hivyo hawatatumia nguvu kubwa kwenye hilo kama ilivyo kwa hizi timu zingine.

Biashara United hii ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo tangu ipande daraja misimu minne iliyopita, inadaiwa wamewahi kucheza mechi moja pekee ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Tusker FC ya hapo Kenya.

Hawa wanahitaji wanahitaji maandalizi ya maana, maandalizi ambayo si ya kujaribu, kuanzia usajili hadi kuwajenga kisaikolojia wachezaji wao ili waweze kumudu kupambana na timu ambazo watakutana nazo na huenda zitakuwa na uzoefu wa mashindano hayo.

Biashara wafanye usajili wa wachezaji bora, waingie kwenye michuano hiyo miguu yote miwili, wapigane na wapambane wasiangalie Namungo alikosea wapi, wasiangalie Namungo alifikaje makundi Kombe la Shirikisho.