UCHAMBUZI: Tusipoacha soka la ujanja tutaendelea kutaabika tu!

Monday April 05 2021
uchambuzi pc

Hakuna anayejua ni mdudu gani anayelitafuta soka la Afrika Mashariki na Kati? Ukanda mkongwe kuliko wote barani Afrika. Inatia uchungu pale unapoviangalia vipaji vikubwa vya soka vilivyotapakaa katika ukanda huo na hali halisi inayozikuta timu za nchi wanachama na klabu zao.

Sio Tanzania tu, vipaji vipo vingi hata Uganda, Rwanda, Kenya na Burundi. Hapo sijazitaja Sudan, Ethiopia na Eritrea zinazopiga soka la kampa...kampa tena..!

Michuano ya kufuzu Fainali za Kombe la Afrika (Afcon) 2021 imekamilika mapema wiki hii kwa timu za nchi 23 kati ya 24 zimeshafuzu fainali hizo za 33 zitakazofanyika Cameroon.

Mshiriki wa mwisho anapatikana kati ya Benin na Sierra Leone zilizopo Kundi L zilizoshindwa kuvaana Machi 30 kutokana na zengwe linalozidi kutibua uungwana wa soka Afrika, yaani janga la corona.

Janga hili limekuwa likitumiwa vibaya na baadhi ya nchi na hata klabu hasa zikiwa nyumbani ili kuhujumu wageni wao, tofauti ilivyo kwa mataifa mengine nje ya Afrika.

Timu zimekuwa zikitegemea janga la corona kunufaika nje ya uwanja. Ebu tuachane nayo, sio mada yangu kwa leo!

Advertisement

Ukiachana na timu hizo, nyingine 23 zimeshatangulia fainali hizo ili kuwania ubingwa unaoshikiliwa kwa sasa na Algeria walioubeba mwaka 2019 pale Misri kwa kuicharaza Senegal.

Tofauti na fainali zilizopita, Ukanda wa Cecafa uliwakilishwa na timu nne za Kenya, Uganda, Tanzania na Burundi, safari hii ukanda huo umetoa timu mbili tu kati ya nane zilizoshiriki hatua ya makundi ya mchujo.

Halafu sasa, zote zinatoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Sudan na Ethiopia ndio zilizopata nafasi tena dakika za lala salama, huku timu nyingine sita ikiwamo Rwanda na Sudan Kusini zilimaliza nafasi ya tatu ya makundi yao.

Ile dhana ukanda huu umeanza kuimarika, ni ndoto za alinacha tu, kwani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini nazo ziliishia makundi ya kuwania kufuzu fainali hizo, huku Djibouti ikitolewa raundi za mchujo na Eritrea na Somalia zikishindwa kushiriki kabisa. Hapo ndipo penye tatizo!

Mataifa hayo tisa yaliyojitosa kushiriki yameshindwa kupenya kwenye mchuano wa timu 52 zilizokuwa zikiwania nafasi hizo 24 na kuambulia mbili tu, huku nafasi 22 zikienda kwa kanda nyingine zenye watetezi Algeria, wenyeji Cameroon, Nigeria, Ghana, Mali, Burkina Faso, Guinea, Gabon, Senegal na Gambia.

Nyingine ni Zimbabwe, Misri, Comoro, Tunisia, Guinea ya Ikweta, Guinea Bissau, Mauritania, Cape Verde, Morocco na Ivory Coast. Huku nafasi ya mwisho ikiwa ni Benin au Sierra Leone.

Ukiangalia orodha hiyo, Comoro imefuzu kwa mara ya kwanza kama ilivyo Gambia, inayonolewa na kocha aliyefurushwa Yanga, Tom Saintfiet. Tena imefuzu mbele ya Kenya. Inashangaza kidogo, yaani Comoro ina soka kubwa kuliko Kenya? Dunia kweli inaenda kwa kasi.

Mauritania inaenda kwa mara ya pili mfululizo, huku Malawi, Cape Verde, Guinea ya Ikweta na Guinea Bissau zikienda kwa mara tatu.

Ila tatizo linaanzia hapa. Katika fainali za mwaka 2017 Cecafa ilipelekea timu moja ya Uganda, ikiwa ni baada ya muda mrefu kupita bila Cecafa kupenyeza timu kwenye fainali hizo za Afrika.

Wadau wa soka wa ukanda huu walipata imani wakiamini moshi mweupe kwa mataifa yao umejitokeza na sasa heshima inarudi.

Kweli buana, fainali zilizofuata haikushangaza kuona ukanda huo ikipeleka timu nne kwa mpigo. Ikiwa ni rekodi kwao na kutoa tumaini safari ya Cameroon, idadi ingeongezea maradufu!

Wengi waliamini safari ndio imeanza ya kuleta mapinduzi Afrika kwa ukanda huo, hata hivyo, badala ya idadi kuongezeka, mwaka huu imepungua na hakuna anayejua fainali zijazo hali itakuwaje?!

Nadhani ni muda mwafaka kwa mabosi wanaosimamia soka. Wasiendelee kulala tena kwa kujifunika shuka gubigubi, badala yake waamke na kujitathmini. Hizi si dalili njema. Ni kuonyesha wamefeli katika kusimamia soka la ukanda huu. Imepita miaka mingi tangu ukanda huu kushuhudia timu zao zikibeba ubingwa. Ilikuwa mwaka 1970, Sudan iliipofanya kweli, ikiwa ni miaka nane tangu Ethiopia ilipotwaa wakati idadi ya timu shiriki ikiwa chache mno.

Kwa Afrika Mashariki, hali ni mbaya zaidi kwani, tangu 1978 Uganda ilipofika mchezo wa fainali, nchi za ukanda huo zimekuwa wasindikizaji tu na hakuna anayeshtuka! Hapo sitaki kugusia ndoto za kwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia. Hizo haziowti kabisa, kwani ni kama wasimamizi wake wamekubali unyonge wa kudumu.

Ni wakati wa viongozi wa Cecafa na wadau wote wa ukanda huo kujitathmini kujua wapi wanapokwamia, ilihali baadhi ya nchi zao zina ligi bora na kushirikisha timju zenye wachezaji wenye vipaji vikubwa wengine wakicheza nje ya Afrika.

Hakuna siri ukiondoa Sudan na Ethiopia kwa ukanda huo wa Cecafa, Uganda ndio inayoibeba Afrika Mashariki. Imeshiriki fainali hizo mara saba, ikifuatiwa na Kenya kisha Tanzania iliyoenda mara mbili, lakini kwa ukanda mzima Ethiopia ndio baba lao ikishiriki mara 10 ikifuatiwa na Sudan iliyoshiriki mara nane. Hii haitoshi!

Inawezekana kuna mahali wanmakosea, ikiwamo pia kuendesha soka kwa ujanja ujanja lionachangia tuwakwamisha kila wakutanapo na wenzao ambao wanafanya mambo yao kwa mipango na mikakati ya muda mrefu kuwafanya waendelee kuwa bora.

Kama hujui Cecafa inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wanachama wengi baada ya Afrika Magharibi (WAFU) wenye nchi 16 na Kanda ya Kusini (COSAFA) nchi 14, huku kanda yenye idadi ndogo kabisa ikiwa ni Afrika Kaskazini (UNAF) yenye nchi tano, mbele ya Kanda ya Afrika ya Kati (UNIFFAC) yenye nchi nane.

Kitu cha ajabu ukanda wa Kaskazini yenye idadi ndogo ya nchi ndio vinara wa mafanikio zaidi, ikitwaa ubingwa wa Afcon mara 11, ikifuatiwa na Afrika Magharibi yenye mataji 9 kisha Afrika ya Kati yenye 8.

Cecafa na ukongwe wake wakiwa ni miongoni mwa waasisi wa michuano hiyo ya Afrika iliyonza 1957 ina mataji mawili tu kama ilivyo kwa Cosafa iliyoundwa hivi karibuni.

Tatizo la ukanda huu wa Cecafa sio kwenye timu za taifa tu, bali hata kwenye ngazi za klabu timu zake zimekuwa zikiburuzwa mbele ya timu za kanda nyingine kuonyesha bado ina kazi kubwa ya kuhakikisha wanaondoka kwenye minyororo hiyo ya unyonge.

Viongozi wa Cecafa chini ya Rais wao, Wallace Karia na wenzake pamoja na wadau wasipokaa chini na kufanya tathimini kujua kinachowaangusha, basi tusitarajie miujiza yoyote, kwani ni wazi hatujakubali kuendesha soka letu kwa njia zinazokubalika katika kujipatia mafanikio.

Soka ni mchezo unaochezwa hadharani, ukifanya hila au ujanja wowote ni lazima litakuumbua kama tunavyoendelea kuumbuka mbele ya mataifa ya nchi nyingine zilizoamua kwenda na kasi ya mabadiliko ya soka la kisasa kwa kuwekeza na kukuza soka lao.

Advertisement