UCHAMBUZI: Simba, Yanga zinakuwaje kubwa bila kukamiwa?

BAADHI ya timu katika Ligi Kuu Bara zimekuwa hazitazamwi wala kuzungumzwa vizuri na mashabiki wengi wa Yanga na Simba na hata baadhi ya wadau wa mpira wa miguu nchini.

Mfano wa timu hizo ni Namungo FC, Mtibwa Sugar, Biashara United, Ruvu Shooting, KMC, Kagera Sugar na Prisons.

Zimekuwa zikitafsiriwa na kuonekana kama timu ambazo hucheza kwa kukamia zaidi pindi zinapokutana na Yanga, Simba au hata Azam tofauti na jinsi zinavyocheza dhidi ya timu nyingine tofauti na hizo.

Kitendo cha timu hizo kuzipa usumbufu mkubwa Yanga, Simba au Azam katika mechi wanazokutana kinaonekana kutowafurahisha mashabiki wengi wa timu hizo kubwa nchini ambao wamekuwa wakishangazwa na kukasirishwa na jinsi wachezaji wa timu hizo wanacheza kwa kujitolea pindi wakutanapo na vigogo hivyo vya soka nchini lakini wanapokutana na nyinginezo hawaonyeshi ushindani mkubwa.

Mara kadhaa tumeshuhudia mashabiki wa timu hizo kubwa nchini wakiwalalamikia na kukasirishwa na wachezaji wa timu tofauti pindi wanapoonyesha kiwango bora au kupata matokeo mazuri pale wanapokutana na Simba, Azam au Yanga wakidai wanaonyesha kujituma zaidi pindi wanapokutana na timu zao tofauti na nyinginezo zinazoshiriki katika ligi.

Tulilishuhudia hili wakati Simba ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Prisons na baada ya kuilazimisha sare kama hiyo Yanga, wachezaji wa KMC wamejikutan wakizua mijadala katika maeneo tofauti nao wakionekana kama wakamiaji.

Hata hivyo ni jambo la kushangaza kuona watu wakiwalaumu wachezaji wa timu nyingine kukamia pindi wanapokutana na Simba, Yanga na Azam na wakati mwingine kufanikiwa kuvuna pointi lakini baadaye wanaenda kupoteza pointi dhidi ya timu zinazoonekana kuwa nazo daraja moja au zile ambazo zimezizidi.

Suala la Yanga, Simba na Azam kukamiwa pindi zinapokutana na timu mbalimbali tofauti na nyingine kwanza linasababishwa na aina ya maandalizi ambayo timu hizo zinayafanya kabla ya mechi husika inayozikutanisha.

Timu za wastani au ndogo, mara nyingi zinapokaribia kukabiliana na zile kubwa mara nyingi kiwango chao cha maandalizi huongezeka maradufu kwa sababu zinajua kwamba zinakutana na washindani ambao wana ubora wa kimbinu na kiufundi kuliko wao hivyo kama wasipojiandaa vizuri wanaweza kujikuta wakipoteza mchezo kwa idadi kubwa ya mabao.

Watatumia muda mwingi kuzisoma timu hizo na wachezaji wao na kutafuta namna bora ya kuhakikisha hawawaletei madhara katika mechi itakayowakutanisha hivyo hadi wanapoingia wanakuwa tayari wameshaandaa mikakati ya kuwadhibiti wasilete madhara.

Mbaya zaidi kiwango cha maandalizi kwa timu kubwa huwa ni cha wastani au cha chini jambo linalotoa faida kubwa kwa timu ndogo kwani zinakuwa zimeingia uwanjani zikiwa zimejiandaa vyema na hivyo kutoa ushindani wa hali ya juu.

Sababu nyingine ni wachezaji wa hizo timu kubwa kutocheza kwa tahadhari kubwa jambo linalopelekea baadhi ya nyakati kujisahau na kufanya makosa ambayo mwishoni huishia kuzigharimu timu zao na kuzifanya zipate wakati mgumu mbele ya akina Prisons, Kagera Sugar, Namungo na wengineo.

Sio dhambi kwa timu kukamiwa na nyingine na hili tumelishuhudia katika maeneo mengi duniani tangu enzi na enzi.

Suluhisho la hilo lipo mikononi husika mwa timu na wachezaji wao na sio kutumia nguvu kubwa kunyooshea kidole wengine kwamba wanakamia pindi wakutanapo na timu zao.

Kwanza ni kwa wachezaji wa timu zao kuhakikisha wanafanya mazoezi ya kutosha yatakayowafanya wawe fiti zaidi ya wale wa timu nyingine lakini pili ni kuhakikisha zinakuwa na mpango bora wa kukabiliana na timu zinazocheza soka la kukamia kama wanavyosema.

Timu zao hizo kubwa zimekuwa zikishiriki mashindano ya kimataifa mara kwa mara ambako zinakutana na wapinzani wanaocheza soka la ushindani mkubwa na walio fiti pengine mara tatu au hata nne ya timu zetu hapa nchini.

Bila kukutana na timu zinazowapa ushindani wa kweli na kuzikamia, Simba, Yanga na Azam zitakuwa zinabweteka na kulemaa na kujiona kwamba ziko tayari kwa ushindani na hivyo kupelekea kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa.

Maana ya timu kubwa ni uwezo wa kupambana kupata matokeo mazuri katika mazingira yoyote yale iwe pindi inapocheza dhidi ya timu zinazocheza soka la kuvutia au zile zinazocheza soka la shoka.

Kama leo hii mashabiki wa Simba, Yanga na Azam hawataki wawe wanakamiwa na timu nyingine basi hawapaswi kuwa wanatamba kuwa timu zao ni kubwa hapa nchini.