UCHAMBUZI: Simba, Yanga waitendee haki ‘Kariakoo Derby’

Muktasari:

MECHI ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu huu baina ya Simba na Yanga imewadia na itachezwa leo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

MECHI ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu huu baina ya Simba na Yanga imewadia na itachezwa leo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kutoka Arusha ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo itakayoanza saa 11 jioni huku Simba wakiwa wenyeji baada ya mchezo wa kwanz abaina yao uliochezwa Novemba 7, 2020 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Hapana shaka mechi ya kesho ina nafasi kubwa ya kutoa muelekeo wa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu huu kulingana na utofauti wa pointi uliopo baina ya timu hizo mbili katika msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa.

Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 61 huku Yanga wakiwa katika nafasi ya pili na pointi zao 57 ingawa mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi Kuu wana mechi mbili za viporo mkononi wakiwa wamecheza jumla ya mechi 25 huku Yanga wakicheza idadi ya michezo 27.

Kwa Simba ikiwa itaibuka na ushindi kesho, maana yake itaongoza msimamo wa Ligi kwa utofauti wa pointi saba na kama wakipata ushindi katika mechi zao mbili za viporo maana yake watawatangulia watani zao kwa utofauti wa pointi 13 na hivyo baada ya hapo watahitajika kupata ushindi katika mechi nne tu ili watwae rasmi ubingwa.

Yanga yenyewe, ushindi utaiwezesha kupunguza pengo la pointi baina yake na Simba na kisha kuombea watani zao wafanye vibaya katika mechi zao za viporo ili kuweka hai matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Hakuna ubishi kwamba Simba na Yanga zinapokutana huwa ndio mechi kubwa kuliko zote kwa ngazi ya klabu hapa nchini kutakana na ukongwe, mafanikio, idadi ya mashabiki pamoja na uwekezaji ambao umefanywa kwa timu hizo zote mbili.

Ni mchezo ambao unakutanisha kundi kubwa la wachezaji wa daraja la juu wanaocheza soka hapa Tanzania lakini pia hata makocha na wataalamu wwazuri wa kusaidia utimizaji wa majukumu ya benchi la ufundi.

Uzito na mvuto huo ndio umefanya mechi baina ya Simba na Yanga kutikisa na kuwa habari kubwa sio tu ndani ya Tanzania bali pia nchi jirani, Afrika na baadhi ya maeneo duniani na kupelekea ifuatiliwe kwa karibu kuanzia kwenye luninga, magazeti ama kurasa za mitandao ya kijamii.

Kwa maana nyingine, mechi hii ni miongoni mwa alama za soka la Tanzania na ndio maana hadi kila kukicha imekuwa haipotezi mvuto wake tofauti na baadhi ya mataifa ambayo leo hii mechi zao za watani wa jadi, hazina tena ule msisimko ambao uliwahi kuwepo miaka ya nyuma.

Leo zikitajwa mechi tano bora za watani wa jadi na zenye msisimko mkubwa barani Afrika, kwa namna yoyote huwezi kuiacha ya Simba na Yanga na ni lazima uiweke pembezoni mwa nyingine kana ya Wydad Casablanca na Raja Casablanca ya Morocco,Al Ahly na Zamalek (Misri), Esperance na Etoile Du Sahel(Tunisia) na Kaizer Chiefs.

Kutokana na hilo, Simba na Yanga zinapaswa kuupa thamani kubwa mchezo wa kesho na zihakikisha zinathibitisha kwa vitendo kwamba mechi baina yao inapaswa kupata heshima kubwa nje na ndani ya mipaka ya Tanzania.

Ndani ya dakika 90 zituonyeshe mashabiki soka safi na la kiwango cha juu lililosheheni mbinu na ufundi ili watazamaji wale watakaokuwepo uwanjani na kwenye luninga waone thamani ya gharama walizotumia kuhakikisha wanashuhudia mchezo huo.

Mbali na hilo, litakuwa ni jambo jema kwa kila upande kuhakikisha unachunga nidhamu katika dakika zote za mchezo, kuanzia kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi, viongozi pamoja na mashabiki ili mechi hiyo iweze kumalizika salama na kila mmoja baada ya hapo aendelee na maisha yake mengine pasipo bughudha.

Nidhamu kwa kiasi kikubwa inatakiwa kuwepo kwa mashabiki kwani wao mara kwa mara ndio wamekuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani katika mechi mbalimbali zinazokutanisha timu hzo.

Kinyume na hapo watakuwa hawajalitendea haki soka la Tanzania na wadau wa mpira wa miguu kiujumla na wanaweza kushusha hadhi yake kwani mechi hii itatazamwa na kundi kubwa la watu nje na ndani ya Tanzania ambao wanaweza kujenga au kubomoa taswira ya soka letu na utamaduni wetu kiujumla.