UCHAMBUZI: Simba walijifunza, wametekeleza msimu huu

Hakuna kitu muhimu kwa binadamu kama kujifunza na kujua, kwani siku zote kujifunza sio lazima kujua ndio maana kuna wengine wanajifunza lakini hawafanikiwi kujua, hivyo si kila anayejifunza hujua kile alichojifunza.

Nasema hivyo kwa sababu katika mchezo wa soka pia somo hilo na ni miongoni mwa masomo muhimu katika mafunzo yote kuanzia ya wachezaji, makocha hadi waamuzi ambapo hufundishwa kuwa katika tasnia hii kila siku ya mechi au mazoezi huwa ni siku ya kujifunza kitu kipya hivyo tunatakiwa kujifunza na kukijua ili kikitokea siku nyingine tuweze kukabiliana nacho.

Ni kutokana na tofauti hiyo iliyopo kati ya kujifunza kitu na kujua ndio maana huwa linakuja suala la uzoefu kwa wachezaji ambalo hutofautisha thamani ya mchezaji kati ya mzoefu na yule asiyekuwa na uzoefu ambapo mwenye uzoefu huwa na manufaa kwa timu kupitia ujuzi alioupata katika muda aliokuwa akicheza na kukutana na changamoto mbalimbali ambazo ndizo zilizomuongezea ujuzi baada ya kujifunza.

Nazungumza hivyo baada ya kuona wiki iliyopita timu ya Simba ikipata ushindi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly kutoka nchini Misri, huku washabiki na wafuatiliaji wote wa mechi wakiridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na Simba katika mchezo huo.

Moja kati ya sababu kubwa iliyowafanya Simba kuweza kupata matokeo hayo ni uzoefu walioupata kupitia mashindano hayohayo msimu uliopita na kuweza kujua kile kinachotakiwa kufanyika ili kufika mbali katika mashindano.

Ni kweli na hapana shaka kuwa miongoni mwa mechi kubwa na zilizoweka historia kwa Simba ni mechi dhidi ya Al Ahly ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na wadau wengi wa soka kutoka kila kona ya dunia.

Hii ni kutokana na ukubwa wa mechi na umaarufu wa timu hiyo duniani hasa ukizingatia kuwa wametoka kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa) hivi karibuni na kukutana na moja kati ya timu kubwa duniani ya Bayern Munich kutoka Ujerumani.

Kabla ya mechi kuchezwa, kwa ukubwa wa timu ya Al Ahly na ubora wa wachezaji mmojammoja wa kikosi ilikuwa ni vigumu kwa wafuatiliaji wengi wa mchezo wa soka nchini kufikiria, sio tu suala la Simba kushinda mechi hiyo, bali kushinda na kuonyesha uwezo mkubwa wa soka kuanzia kwenye eneo la timu hadi mchezaji mmojammoja.

Upande uliokuwa ukiangaliwa ulikuwa ni mmoja tu - yaani upande wa ubora wa Al hly na sio ubora wa Simba.

Lakini baada ya mchezo kuanza Simba ilifanikiwa kuthibitisha kwa vitendo kuwa makosa waliyoyafanya katika misimu iliyopita katika mechi za kimataifa lilikuwa ni somo na walijifunza na kujua nini kinachotakiwa kufanyika ili kuweza kukidhi mahitaji ya mechi kubwa kama hizo.

Hivyo mechi dhidi ya Alhy inaweza kutumika kama uthibitisho baada ya kuanza mechi hizi za hatua ya makundi kwa kuchukua alama tatu katika mechi nje ya nchi dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).

Ni pale timu inapopata mafanikio kupitia njia kama hii ndio umuhimu wa kujifunza huwa unaonekana, kwani bila ya Simba kujifunza kupitia misimu iliyopita isingekuwa kazi rahisi kuweza kushinda katika mechi hii ya Dar es Salaam na kuwathibitishia wafuatiliaji wa mchezo kuwa wameshinda katika mechi waliyostahili kushinda kutokana na uwezo walioonyesha wachezaji uwanjani.

Na mwalimu yeyote anayefundisha huridhika pale anapoona mwanafunzi aliyemfundisha akifanikiwa kutekeleza kile alichomfundisha, hivyo kuthibitisha kuwa alitumia muda sahihi wa kujiunza na kujua.

Ni kutokana na hali hiyo ndio maana ameweza kutekeleza kutokana na kile alichojifunza, hivyo Simba isingekuwa imefanya maandalizi stahiki kulingana na mahitaji pengine kundi hili linalohusisha timu za Al Ahly, AS Vita, El Mereikh lingeendelea kutafsiriwa kama ni kundi la kifo kwa Simba, huku washabiki wa timu za Al Ahli na As Vita wakiendelea kutafsiri kama ni kundi jepesi kwao.

Kwa maana nyingine ni kwamba matokeo haya yana thamani kubwa kwa soka letu, kwani yataanza kubadilisha mtazamo wa kiakili wa wadau wa soka nchini ambao tumezowea kuzitafsiri timu zetu kama dhaifu zinapokutana na timu kama hizi kutoka mataifa ya Afrika Kaskazini.

Ikumbukwe kuwa taifa la Misri ambapo timu ya Al Ahly ndiko inapotoka ndilo lenye mafanikio makubwa zaidi kwa timu zake kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa barani Afrika mara nyingi ukianzia na Al Ahly wenyewe ambao ndio wanaongoza kwa kulitwaa taji hilo mara tisa, huku klabu za nchi hiyo zimelitwaa mara 15, hivyo kuwa ndio vinara kama nchi.

Imeandikwa na Mchambuzi; ALLY MAYAY