UCHAMBUZI: Hili la Ajibu Yanga inaweza kurudia yaleyale ya Sarpong

Friday June 11 2021
ajibuu pic

KILA unalotaka kufanya ili upate mafanikio unahitaji kuanza na tathmini ya kufahamu ni kipi unahitaji na ujue utakipata vipi ili uweze kuwa na usahihi wa yale ambayo unayakusudia.

Unapofanya makosa ya kushindwa kupata tathmini ya kina unaweza kujikuta unaanguka katika lile unalotaka kufanya na badala yake kama ulikuwa na watu wenye matarajio makubwa nyuma yako unaweza kujikuta umewaangusha kwa lile ambalo umefanya.

Wiki moja iliyopita uliibuka mjadala mkubwa uliowafanya wengi kutofautiana juu ya usajili wa kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu kurejea Yanga na kwamba klabu hiyo inataka kumsajili tena akitokea klabu ileile ambayo alitokea awali.

Hatua nzuri ni kwamba Ajibu alikuwa ni yule yule wa nyakati zile kutokana na nyakati zile alikuwa anakosa nafasi na sasa pia akiwa anatokea katika nyakati hizohizo za kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika klabu ya Simba.

Hakuna asiyekubali kuhusu uwezo wa Ajibu unapozungumzia wachezaji waliozaliwa na kipaji kikubwa. Ajibu anaweza kuwa ndani ya tano bora. Akiwa na mpira na akaamua kufanya kazi yake ni vigumu kumuona anaendelea kucheza Tanzania.

Mungu anatakiwa kushukuriwa kwa kumbariki kipaji kilichokamilika ambacho wengine wamenyimwa ila naye kuna jambo moja kubwa amenyimwa ambalo ndio linalomuhukumu ambalo ni kukosa nidhamu ya mchezo anaoucheza kwa kutakiwa kujituma.

Advertisement

Kosa hili ndio linalomuhukumu pale Simba na kufikia kusotea benchi muda mrefu na hatua mbaya zaidi hata katika safari za hapa ndani za hivi karibuni amekuwa akikosekana akiwa na anguko baya zaidi.

Wako wengi ambao wamezidiwa kipaji na Ajibu pale Simba lakini huwezi kuwaweka nje kisha ukampa Ajibu nafasi kutokana na wanachomzidi Ajibu ni kujituma kwao ndio silaha ambayo wanamuulia Ajibu.

Wakati fulani Ajibu akiwa Yang atena kwenye ubora wake mkubwa niliwahi kuongea na kocha wa zamani wa klabu ya Township Rollers ya Botswana, Nikola Kavazovic, nilimuliza aliona kipaji gani wakati anakutana na Yanga, alitaja wachezaji watatu ambao aliwapenda ila Ajibu akamuweka wa mwisho kabisa.

Nilimuona kama ni mtu aliyechanganyikiwa kwa uamuzi wake wa kumweka Ajibu wa mwisho wakati huo akili yangu ikimuona kama ni staa ambaye alitakiwa kutajwa wa kwanza kisha jamaa akanijibu yule ana kipaji lakini shida yake ni mchezaji anayecheza kwa majukwaa lakini pia hawasaidii wenzake.

Safari hii nikashangaa tena Yanga kuhusishwa na mchezaji wa namna hiyo kisha nikajiuliza wako watu kweli wanaofanya tathmini ya kina ya timu yao au bado kuna kundi la watu au watu wachache wanaoendelea kuishi maisha yaleyale?

Kosa kubwa ambalo linaiangusha Yanga ni kukosa tathmini ya kina katika wachezaji ambao wanataka kuwasajili. Hali ilivyo au picha inayojionyesha wako wachache na inawezekana wakawa hawana taaluma sahihi. Wanafanya uamuzi unaozidi kuiumiza klabu hiyo.

Mfano mzuri ni usajili wa mshambuliaji kama Michael Sarpong ambaye au hata Fiston Abdulrazack ambao wote hawa wawili nina shaka na kina cha tathmini iliyofanyika mpaka wakajiridhisha na kuamua kuwasajili.

Sarpong amevuma katika msimu mmoja tu pale Rwanda akiwa mfungaji bora lakini sio sifa sana ya kumfanya asajiliwe na klabu kama Yanga ambayo inahitaji mtu sahihi zaidi ya Sarpong ambaye sasa ni wazi ameshindwa kufanya kile ambacho alitarajiwa na umma wa watu wa soka nchini.

Endapo Yanga wangekuwa na watu sahihi katika kujua kuangalia ubora wa mchezaji sidhani kama wangepoteza fedha kirahisi kama ambavyo walifanya na badala yake wakavuna walichopanda.

Hali hiyo ikajirudia tena kwa Fiston ambaye naye akaanguka na kuiangusha klabu hiyo kwa kushindwa kufanya kile ambacho kilitakiwa kufanyika ndani ya kikosi hicho.

Siwezi kuwalaumu sana ambao wanasajili kwa kuwa pia wako wachezaji ambao waliwasajili na kufanya vyema lakini maeneo hayo mawili kazi ya kujiridhisha uamuzi hayakufanyika sawasawa na baadaye kuiangusha timu hiyo.

Naamini changamoto hizi zinaweza kuwasaidia Yanga katika kufanya uamuzi sahihi lakini bado naona kama wanaweza kubaki palepale endapo wataendelea kufikiri ndani ya boksi badala ya kufikiria nje ya boksi ili uweze kuwa na upana wa kujua ubora halisi wa wachezaji wanaowahitaji ili kuimarisha timu hiyo ambayo imepoteza ubingwa kwa misimu mitatu na wa nne huu unaingia.

Advertisement