UCHAMBUZI: Haya mawili yafanyiwe kazi msimu ujao

MSIMU wa 2020/2021 umemalizika kwa Simba kutwaa mataji mawili makubwa ya soka hapa nchini ambayo ni Kombe la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam.

Timu za Simba, Yanga, Azam na Biashara United ndizo zimepata fursa ya kuwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya klabu Afrika msimu ujao baada ya kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.

Bahati mbaya imekuwa kwa timu za Mwadui, Ihefu, JKT Tanzania na Gwambina ambazo zimeshuka daraja kutoka Ligi Kuu kwenda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zikipishana na timu za Geita Gold na Mbeya Kwanza ambazo zimepanda daraja.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, tumeshuhudia jumla ya timu 10 zikiteremka hadi Ligi Daraja la Pili ambazo ni Majimaji, Njombe Mji, Mawenzi Market, Boma, Singida United, Alliance, Mbao, Rhino Rangers, AFC na Lipuli.

Hapana shaka kwamba kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu 2020/2021 ni mwanzo wa maandalizi ya msimu mpya wa 2021/2022.

Na kutokana na kuchelewa kumalizika kwa msimu wa 2020/2021, ni jambo lililo wazi kwamba muda wa maandalizi kwa ajili ya msimu ujao ni finyu kwani kuna muingiliano wa ratiba na matukio ya kisoka ambayo yanalazimisha timu kuwapa muda mfupi wa mapumziko wachezaji na maofisa wao wa benchi la ufundi.

Mfano kuna mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 23 yanayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), na baada ya kumalizika kwake leo Ijumaa, keshokutwa Jumapili kunaanza mashindano mengine ambayo ni yale ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati yakijulikana kama Kombe la Kagame.

Mashindano hayo yatamalizika Agosti 15 na baada ya hapo kutrakuwa na wiki ya mechi za timu za taifa, mashindano ya klabu Afrika ambayo yataanza mwanzoni mwa Septemba lakini pia Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza mwezi huohuo.

Kwa kutambua ufinyu huo wa muda, hivi sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) wametoa fursa kwa wadau mbalimbali wa mpira wa miguu kutoa maoni na ushauri juu ya kanuni na taratibu zinazoendesha mashindano mbalimbali yaliyo chini ya mamlaka hizo.

Kutokana na fursa hiyo ningependa kushauri marekebisho katika kanuni na taratibu kadhaa katika msimu ujao ili tuweze kuwa na mashindano bora zaidi ya hapo nyuma.

Miongoni mwa marekebisho hayo yawepo katika kanuni ya kupanda na kushuka daraja kwa timu kuanzia zile za Ligi Kuu haid katika Ligi Daraja la Pili.

Kanuni ya msimu uliomalizika, inafafanua kuwa timu mbili vinara wa Ligi Daraja la Kwanza, zitapanda moja kwa moja daraja na kutinga katika Ligi Kuu.

Na timu mbili ambazo zitafuata katika FDL, zitacheza mechi za mchujo na timu zilizoshika nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu ili kusaka fursa ya kuwemo katika ligi hiyo.

Kanuni hii ina malengo mazuri ya kuzifanya timu za Ligi Daraja la Kwanza kuwa imara zaidi kabla hazijaingia Ligi Kuu lakini kwa upande mwingine haizitendei haki kutokana na mazingira yanayozunguka na kuzibeba timu za Ligi Kuu.

Timu za Ligi Daraja la Kwanza nyingi hazina uwezo kiuchumi na ikumbukwe ligi yao inawahi kumalizika hivyo zinalazimika kuzisubiria timu za Ligi Kuu kwa muda mrefu kabla ya kucheza nazo mchujo jambo ambalo linazifanya zipoteze ubora na ufiti wa mechi na kujikuta zikishindwa kutoa upinzani.

Suluhisho la hili ni kubadili utaratibu wa kucheza mechi za mchujo. Ama watumie utaratibu wa kuchezesha droo kwa timu zote nne au timu mbili za Ligi Kuu zikutane zenyewe kwa zenyewe na timu mbili za FDL zicheze zenyewe na mbili zitakazoshinda zicheze Ligi Kuu.

Lakini pia kuna huu utaratibu wa kupeleka mechi za hatua ya nusu fainali na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam katika viwanja vya mikoa isiyo na timu kwenye Ligi Kuu kwa lengo la kuamsha ari na hamasa ya soka katika mikoa husika.

Ni utaratibu mzuri lakini unapaswa kufanyiwa marekebisho ambapo badala ya kuteua viwanja hivyo wakati mashindano yamefikia hatua ya robo fainali, ni vyema TFF ifanye uteuzi huo kabla ya msimu kuanza.

Kuwekwe vigezo, masharti na muda maalum kwa mikoa inayotaka kuwa mwenyeji wa mechi hizo katika kuandaa viwanja na vikishindwa kufanya kwa wakati vipokonywe hakii hiyo na ipelekwe katika mikoa ambayo inakidhi.

Kuchelewa kuteua viwanja kunasababisha maandalizi yake yawe ya kulipua na mwisho wa siku kunapelekea viwanja kutumika bila kuwa na ubora stahiki.

Hayo ni mfano tu wa mambo ambayo ningependekeza yarekebishwe katika msimu ujao ingawa yako mengi na hayawezi kutosha humu.