UCHAMBUZI: Haji Manara alizingua hapa msimbazi

NDUGU yangu Haji Manara wamekula kichwa. Kwa ile audio niliyoisikia pale klabuni siku ile, sikuona jinsi anavyobaki.

Tena haswa ukizingatia Mnyama kashinda Kigoma na Kombe kabeba. Kimaadili malumbano ndani ya uongozi ni jambo la kawaida kabisa. Lakini ya namna gani? Yakujenga. Ili muendelee au mfikie muafaka na jambo lolote liwe na tija lazima kuwe na hoja, mtu mmoja aseme na mwingine amsikilize na kama kuna ulazima amjibu kwa hoja kukubali, kupinga au kuboresha jambo husika.

Lakini kwenye vikao halali vya ndani. Si kubwatuka kwenye vijiwe au mitandao ya kijamii na kutoa siri za ndani ya sehemu husika. Manara alisikika akilumbana na uongozi wa juu wa Simba akimaanisha Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez. Manara kwenye sauti zake alizojirekodi zilivuja na kuwekwa kwenye mtandao alikuwa akimshutumu Barbara kwamba anaivuruga Simba na hampendi yeye.

Barbara hajataka kumjibu, lakini alichokifanya Manara hata kama angekuwa ana hoja hakuwa sahihi. Ni vurugu zile, ametumia njia isiyo sahihi kufikia ujumbe wake. Hali kama ile kwa klabu ya wanachama kama Simba inaweza kuzua taharuki na kuvuruga hali ya mambo.

Angeenda ndani ya uongozi na kupeleka mashtaka yake kimyakimya hata kama wangeshikana mashati wangeamua kwa staili nyingine, lakini kosa kubwa alilofanya kimaadili ni kumdhalilisha bosi wake hadharani tena kwa lugha ya kejeli.

Kwa menejimenti inayojielewa hakuna namna ambavyo Manara angeweza kuendelea kuchekewa au kuendelea kuwepo kazini hata kama alikuwa na hamasa ya namna gani kwa mashabiki wa Simba.

Lazima ifike sehemu taasisi isimame kisha watu wafuate. Hakuna mtu mkubwa kuliko taasisi. Ingawa mtu ni muhimu kwa maendeleo ya taasisi. Nidhamu ya uongozi ni kitu cha msingi sana kwa vile inaongeza umoja. Kwa namna yoyote kama Simba wangeendelea kumhofia Manara kwa kitendo kile walikuwa wanakwenda kupasuka kuanzia kwenye uongozi wenyewe, wanachama, mashabiki na hata wachezaji na hakuna mantiki yoyote ya kuwa na makundi kwa ajili ya mtu mmoja. Wakati mwingine kuna ulazima wa kufanya uamuzi mgumu kwa masilahi ya taasisi au kuweka usawa sehemu fulani. Narudia tena simaanishi kwamba Barbara yuko sahihi ila kwa kilichotokea wengi wanasimama nae si kwavile ni mwanamke bali njia ambayo Manara aliitumia kufikisha ujumbe wake haikuwa sahihi. Alikosema taimingi.

Lazima wakati mwingine viongozi waelewe hata kama ushawishi kiasi gani haohao Simba ndio waliokupa na unapaswa kuwaheshimu kwa namna mbalimbali usivimbe kichwa ukapitiliza. eshimu uongozi wa mpira kama uongozi mwingine wowote wenye nia thabiti ya kufikia malengo. Kilichomtokea Manara kiwe fundisho kwa viongozi wengine na wadau wa soka wajifunze kuheshimu utaratibu na wajue kwamba uongozi ni wito na ni sehemu muhimu sana katika maendeleo ya soka la Tanzania haswa katika ngazi ya klabu.

Pamoja na mambo mengine yoyote lazima viongozi kuheshimiana, kustahiana na kuwa na njia nzuri ya kujadiliana mambo yenu na kufikia muafaka kwa njia inayofaa.

Haya mambo yanayofanywa na viongozi kwa namna moja au nyingine yanaathiri mpaka saikolojia za wachezaji ndani na nje ya uwanja. Yanaibua mpaka sintofahamu baina ya wanachama. Tusitumie vibaya kivuli cha mashabiki au ukubwa wa klabu zetu kwa masilahi binafsi.

Lengo letu liwe kukimbizana na maendeleo chanya kuhakikisha tunafanya vitu vikubwa zaidi ambavyo vitabeba hadhi ya klabu zetu na kukuza soka la Tanzania. Kwavile naamini kwa namna yoyote ile kama klabu zikifanya vizuri na zikiwa na uongozi imara soka la nchi litakwenda kwenye uelekeo mzuri na wenye faida. Hata Wachezaji wetu watafaidi na watajifunza mengi kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Hii yote ni manufaa ya uongozi thabiti ambao wenye malengo ya mafanikio siyo kulumbana au kuonyeshana kwamba fulani ni zaidi ya fulani kutokana na hiki na hiki. Viongozi lazima wajifunze kuheshimu nafasi zao na wasitumie soka kama kichaka cha kuonyesha umaarufu.


IMEANDIKWA NA DOTTO JONGWE