UCHAMBUZI: Anayetamani kuondoka Simba SC anakwenda wapi?

Saturday May 01 2021
ROBO FULL SIMBA
By Mwanahiba Richard

KLABU nyingi nchini hivi sasa wachezaji wao wamemaliza mikataba ikiwa na maana kwamba asilimia kubwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara utakapomalizika nao watakuwa huru.

Ligi inamalizika mwezi Julai, lakini mikataba mingi inamalizika Mei ingawa sasa haiwezi kumalizika hadi ligi itakapomalizika kwani awali ilikuwa inamalizika Mei.

Wengi wanaangalia klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam FC kwamba ndizo zenye uhitaji mkubwa wa kuwa na wachezaji wazuri na hivyo wanapaswa kufanya usajili mzuri ama kuwaongezea mikataba mipya nyota wao.

Timu hizo zenye uwezo kifedha ndizo zinazungumziwa zaidi kwenye usajili ingawa haujafunguliwa rasmi bali tayari timu zimeanza mazungumzo ya usajili mpya ama kuongeza mikataba.

Nyota wa Simba na Yanga ndiyo gumzo na hivi sasa anayezungumziwa zaidi ni beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amedumu Simba kwa zaidi ya miaka miatano anatajwa kuhamia kwa watani wao, Yanga.

Simba wanajiamini kwelikweli, hawajamuongeza mkataba Tshabalala ambaye inadaiwa amebakiza mkataba wa miezi miwili na meneja wake, Herry Mzozo amesisitiza kutaka Sh100 milioni kuwa ndiyo thamani ya mteja wake.

Advertisement

Mbali na kiwango hicho cha pesa, Mzozo anasisitiza mchezaji wake kama Simba watahitaji kumuongezea mkataba mpya, basi anayepaswa kumpa mkataba huo ni tajiri na mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammad Dewji ambaye mara kadhaa huwa anaonekana akiwasainisha mikataba baadhi ya wachezaji mahiri wa kikosi hicho.

Mzozo anaona hivi sasa ni wakati wa mteja wake kusajiliwa moja kwa moja na tajiri huyo na sio kupitia kiongozi mwingine wa klabu na hiyo nadhani anaona thamani ya mteja wake kwasasa ni kusaini mbele ya tajiri wa klabu hiyo.

Kelele zimekuwa nyingi sasa juu ya Tshabalala lakini viongozi wa Simba wametulia wala hawana hofu, hiyo inatokana na namna timu yao ilivyojipambanua kwa sasa barani Afrika.

Inafanya vizuri michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hata ligi ya ndani inataka kutetea ubingwa.

Ikifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu Bara basi itakuwa ni mara ya nne mfululizo kwao, na ni mambo yanayopewa kipaumbele kwao kipindi hiki, mechi za robo fainàli ya CAF, Ligi Kuu na kutetea kombe la Shirikisho la Azam na usajili ni kipaumbele chao cha nne.

Wanachotamba viongozi wa Simba ni mafanikio wanayoyapata ndani na nje ya nchi ndio maana wanaona wachezaji wao hawawezi kuhama timu hata kama muda wa usajilì ukibaki mdogo, wanaamini kwamba hakuna timu inayoweza kutoa fungu nono na kumnasa mchezaji wao.

Kuna zaidi ya nyota watano ndani ya Simba ambao mikataba yao imekwisha na wapo kikosi cha kwanza, wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine lakini haiwashitui viongozi wao wanajua hakuna sehemu ya kwenda zaidi ya kubaki Msimbazi kwenye mishahara minono na posho za maana kila wanapocheza mechi.

Ni kweli ndani ya Simba kuna neema ya kipesa, hawana shida yoyote na wala hawali njaa. Wapo vizuri kuanzia ndani hadi nje ya uwanja ndio maana hata wale wanaotupwa jukwaani wanajisikia raha tu kuwepo - hawatamani kuondoka, bali wanachotaka ni kuona akaunti zao zinasoma namba nyingi kila mwezi.

Wanahisi kwamba hata wakienda timu zingine hawatapata huruma nzuri ya kipesa kama hapo Simba na wanasahau kabisa suala la viwango vyao kushuka hilo hawajali na hakuna aliyestuka si mchezaji wala mameneja wao.

Cha kujiuliza hao wachezaji wa Simba wakitaka kuondoka wanakwenda wapi hasa wale ambao wanasugua benchi ama kuwa ndugu watazamaji wa jukwaani ambao hawana mawazo ya kulinda viwango vyao.

Ni klabu gani itawàchukuwa wakalia benchi wa Simba ama washangiliaji jukwaani, inafika wakati wanapaswa tu kuachwa jinsi walivyo ili akili zao ziamue zinataka nini kati ya mambo mawili Pesa na Kucheza.

Advertisement