Tumshukuru Rais Samia, tukimkumbuka Festo Sanga

Muktasari:

BAADA ya subira ya muda mrefu ya wadau wa michezo hasa soka, hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo ambayo yanaonekana kuponya nyoyo zao.

BAADA ya subira ya muda mrefu ya wadau wa michezo hasa soka, hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo ambayo yanaonekana kuponya nyoyo zao.

Akihutubia katika mkutano wake na vijana uliofanyika katika Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza Jumatatu wiki hii, Rais Samia alitoa maagizo mawili ambayo yameonekana kuwakosha wadau wa michezo nchini kwani yanagusa moja kwa moja nyanja hiyo.

Kwanza alikiagiza chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha inakarabati viwanja vyote inavyomiliki ili viwe na eneo zuri la kuchezea, huku akishauri viweke nyasi bandia na iwapo suala hilo ni gumu kwa gharama zake, basi ikodishe kwa wawekezaji wanaoweza kugharamia hilo.

Lakini pia alitoa ahadi kwa wananchi kuwa serikali itahakikisha inajenga vituo vya michezo kwa watoto wadogo na kuvisimamia angalau katika kila mkoa nchini ili iweze kusaka, kuvumbua na kuendeleza vipaji ambavyo vitaitangaza vyema na kuitoa kimasomaso nchi yetu siku za usoni.

Changamoto hizo mbili ambazo Rais ameagiza zishughulikiwe, kwa muda mrefu ndio zimekuwa kilio cha wadau na vyama vya michezo nchini kwa sababu kwa kiasi kikubwa ndio zimechangia kuifanya nchi yetu kuwa nyuma katika nyanja ya michezo licha ya kuonekana kuna vipaji vingi.

Suala la ubovu wa eneo la kuchezea la viwanja vingi nchini ambavyo idadi kubwa vinamilikiwa na CCM, limekuwa na athari kubwa kwa mchezo wa soka kwa kusababisha majeraha kwa wachezaji yanayosababisha timu kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwatibu ambacho kingeweza kutumika katika shughuli nyingine za uendeshaji.

Pia uwepo wa idadi kubwa ya viwanja visivyo na eneo zuri la kuchezea umekuwa ukisababisha vijana wengi kushindwa kuonyesha vipaji vya soka, hivyo idadi kubwa kujikuta wakishindwa kutimiza ndoto zao za kisoka.

Ni vigumu kwa makocha kuwaandaa wachezaji bora na wenye ushindani katika viwanja ambavyo havina eneo zuri la kuchezea kwa sababu walimu wanalazimika kutowapa mazoezi mazuri ya ufundi na mbinu ambayo ni nguzo muhimu katika kujenga mchezaji bora na mwenye ushindani wa kimataifa.

Pamoja na hayo, pia viwanja hivyo kwa namna moja au nyingine vinachangia kushusha hadhi ya soka na ligi yetu na hiyo inaweza kukimbiza wawekezaji ambao pengine wangeweza kushawishika kuingiza fedha katika udhamini kwenye soka letu kwa vile mechi hizo zinaonyeshwa katika luninga.

Kwa upande mwingine agizo la Rais Samia kwamba serikali ihakikishe inajenga vituo vya michezo angalau katika mkoa ni jambo linalotazamwa kama ukombozi mkubwa kwa sekta ya michezo.

Uwepo wa vituo hivi utatusaidia kupata wanamichezo bora na wenye ushindani ambao wameandaliwa vyema kiufundi, mbinu na kisaikolojia kuweza kuishi maisha ya kiweledi kama wanamichezo tofauti na hivi sasa ambapo wengi wanaibuka bila kupata misingi bora wakiwa katika umri mdogo.

Tukiwa na idadi kubwa ya wanamichezo waliopitia katika misingi sahihi, tutakuwa na uhakika wa kukuza uchumi na pato la nchi kupitia kodi watakayolipa kutokana na mapato watakayochuma lakini pia uwekezaji wataufanya jambo litakaloongeza wigo wa ajira kwa vijana wengine wa Kitanzania.

Wakati tukimpongeza Rais kwa kuonyesha kujali sekta ya michezo na kuanza kuipangia mikakati ya kuifanya ipige hatua ni vyema pia kuwakumbuka wadau ambao kwa namna moja au nyingine wametoa mchango mkubwa katika kuiamsha serikali na kuikumbushia wajibu wake katika hili.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Makete, Festo Sanga ambaye siku chache kabla ya maagizo ya Rais, alipaza sauti bungeni kuomba serikali itafute suluhisho la changamoto ya ubovu wa eneo la kuchezea la viwanja vya soka nchini lakini pia ujenzi wa vituo vya michezo kwa vijana wenye vipaji.

Maombi haya ya Mbunge Sanga ndio yalikuwa pointi mbili za msingi ambazo Rais alizigusia katika mkutano wake na vijana wakati akitoa muelekeo wa serikali yake kuhakikisha sekta ya michezo inapiga hatua.

Kufanikiwa kwa maombi ya Mbunge Sanga kunapaswa kuwaamshe wabunge wengine waliopewa kazi ya kuwasemea wanachi bungeni kuwa wanapokuwa katika chombo kama kile wanapaswa kujikita zaidi katika kusaka suluhu ya kero zinazowagusa wananchi kwenye majimbo yao na Tanzania kwa ujumla badala ya kwenda kupigania maslahi yao binafsi.