Tariq: Sio Simba tu yeyote namfunga

UKITAJA mafanikio ya Mbeya City hadi sasa lazima utataja majina ya mastaa wanaong’ara kikosini akiwemo mshambuliaji Tariq Seif ambaye amekuwa gumzo msimu huu.

Mbeya City imekuwa na matokeo mazuri tangu msimu uliopita ikiwa chini ya kocha Mathias Lule aliyetimkia Singida Big Stars na sasa inaongozwa na Mubiru Abdalah. Makocha hao wote ni Waganda.

Pamoja na kwamba timu hiyo ndio kinara wa sare Ligi Kuu Bara ikiwa nazo saba, lakini imekuwa na mvuto inapokuwa uwanjani ikipambana kutafuta matokeo mazuri.

Tariq alijiunga na vijana hao wa jijini Mbeya msimu huu akitokea Polisi Tanzania, ambapo tayari amefunga mabao manne na asisti nne akizidiwa na mwenzake Sixtus Sabilo aliyefunga mabao saba na kuhusika mengine sita.

Straika huyo katika mazungumzo na Mwanaspoti amefunguka mengi ikiwamo changamoto na mafanikio, uchu wa kucheza timu kubwa na matarajio yake msimu huu.


BAO LAKE SIMBA

Nyota huyo anafichua kuwa siyo mara ya kwanza kuwafunga Wekundu wa Msimbazi kwani aliwahi kufanya hivyo akiwa na Stand United msimu wa 2017/18.

Anasema wakati timu hiyo ikicheza katika Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa) Dar es Salaam aliwafunga bao la kichwa akiunganisha krosi ya Sabilo japokuwa walilala kwa mabao 2-1.

Anasema kuwa bao aliloifunga Simba majuzi aliwazidi mikimbio mabeki wa Msimbazi lakini ikiwa ni maelekezo ya kocha wake baada ya kuwasoma wapinzani jambo ambalo alilitekeleza kwa ufasaha.

Anasema siyo kwamba anafurahia au kuchukia kuifunga timu hiyo kubwa, isipokuwa timu yoyote anayokutana nayo na akapata nafasi ya kufanya hivyo haachi kuifunga.

“Mimi timu yoyote naifunga na siyo mara moja kuwafunga Simba na wala sichukii au kufurahia, haya ni majukumu yangu na yeyote mwingine namfunga,” anasema straika huyo.


HAJARIDHIKA

Mshambuliaji huyo mwenye nguvu na kasi uwanjani anasema kama straika bado hajaona makali yake kwani jukumu kubwa kwake ni kufunga mabao, hivyo kwa sasa hajaridhika.

Anasema idadi ya mabao aliyonayo na mechi alizocheza ni mambo mawili tofauti akisema kuwa kwa sasa anapambana ili kuongeza kasi zaidi katika ufungaji mabao.

Tariq anakiri kuwa bado hajapata upinzani mkali wa mabeki kwenye mechi alizocheza na timu walizokutana isipokuwa ni utulivu na bahati vinakosekana katika

utupiajia mabao mengi akiahidi kwenye mechi zinazofuata atafanya kweli.

“Kwanza jukumu langu ni kufunga. Sasa ukiangalia mechi nilizocheza na idadi ya mabao niliyonayo utaona ni vitu viwili tofauti. Siyo kwamba mabeki wananipania ila ni bahati na umakini vinapungua, nahitaji kuvuka hapa,” anasema Tariq.


SHANGILIA YAKE

Mwamba huyo amekuwa na staili tofauti ya ushangiliaji, lakini ile ya majuzi alipoisawazishia Mbeya City dhidi ya Simba iliwashangaza mashabiki wengi wa soka nchini.

Mchezaji huyo aliyewahi kukipiga Yanga anasema ushangiliaji huo aliuchota kwa nyota wa zamani wa Liverpool, Man City, Inter Millan na AC Millan, Mario Ballotelli.

“Ninashangilia kwa staili mbalimbali, lakini ile ya juzi nilikumbuka ‘role modal’ wangu Mario Balotelli kwa kuwa namkubali sana, ndio nikashangilia hivyo,” anasemanyota huyo.


SIMBA NA YANGA

Mchezaji huyo anaweka wazi kwamba kazi yake ni soka hivyo hachagui wala kubagua timu ya kuchezea na kwamba mchezaji yeyote mwenye ndoto ya mafanikio lazima aziwazie Simba na Yanga.

Nyota huyo anasema anazifikiria zaidi timu hizo kwani uwezo anao uwanjani na lolote anaweza kufanya akiaminiwa na kocha akibainisha kuwa msimu huu amepania kufanya mambo makubwa.

“Kazi yangu ni mpira popote naweza kucheza. Hata hivyo mchezaji yeyote mwenye ndoto ya mafanikio lazima aziwaze timu kubwa ikiwamo Simba na Yanga. Nikipata nafasi naweza kufanya makubwa,” anasema.

Anaongeza kuwa mara ya mwisho kufunga idadi kubwa ya mabao ni pale alikuwa Biashara United, alipofunga 11, hivyo msimu huu anatataka kuvunja.


AJIVUNIA REKODI

Tariq anasema moja ya mafanikio anayojivunia kwenye kazi yake tangu aanze soka la ushindani msimu wa 2016/17 ni kupandisha timu daraja na hajawahi kushusha.

Anasema mara ya kwanza kucheza soka la ushindani akiitumikia Transit Camp inayoshiriki Championship kwa sasa aliipandisha daraja la kwanza (kwa sasa Championship) kabla ya kutimkia Stand United aliyoinusuru kushuka Ligi Kuu.

Anasema baada ya kudumu Stand United kwa miezi sita, aliiacha pazuri kisha kutimkia Biashara United ambako aliikuta pabaya na kuipambania kubaki Ligi Kuu.

“Najivunia kupandisha na kuzinusuru timu. Transit Camp niliyochezea kwa mara ya kwanza niliipandisha Championship, Stand na Biashara United nikazinusuru,” anasema.


KINACHOIBEBA CITY

Mshambuliaji huyo anasema mafanikio iliyo nayo Mbeya City ni kutokana na maelewano mazuri ya wachezaji na maelekezo ya benchi la ufundi ambayo yanawapa kujiamini mastaa hao wawapo uwanjani.

Anasema safu ya ushambuliaji imekuwa imara kutokana na muunganiko bora wa wachezaji watatu Tariq, Sabilo na Awadh Juma na wengine ambayo imewapa matokeo mazuri.

Mchezaji huyo anasema kwamba malengo ya timu ni kumaliza katika nafasi nne za juu, hivyo kila mmoja anapambana katika nafasi yake ili kuhakikisha kwamba anaisaidia Mbeya City kufikia malengo na kwamba kila mechi kwao ni vita ya pointi.

“Tumekuwa na maelewano mazuri eneo la mbele, lakini mafanikio yote ni ya timu kwa ujumla. Kila mmoja anapambana kwa nafasi yake kufikia malengo,” anasema mchezaji huyo.

Anaeleza kuwa muunganiko alionao sasa unamkumbusha alipokuwa Stand United na Sabilo, Bigiramana Blaise na George Makang’a, huku Biashara United akikiwasha vyema na Innocent Edwine na George Makang’a.