Sonso: Niliumia sana kuondoka Yanga

WAKATI dirisha la usajali Bongo likifungwa, Klabu ya Ruvu Shooting ilitangaza kupata saini ya beki Ally Mtoni ‘Sonso’ kwa uhamisho huru akitokea Kagera Sugar.

Sonso ni miongoni mwa mabeki waliofanya vizuri nchini kutokana na kiwango ambacho alikionyesha akiwa na timu ya Lipuli FC ya mkoani Iringa, jambo lililowavutia mabosi wa Yanga kumsajili.

Idadi kubwa ya mashabiki walianza kumfahamu Sonso akiwa Lipuli, lakini ukweli ni kwamba beki huyo alianzia mchangani katika timu ya Kauzu FC.

Kauzu ni timu iliyopo Temeke, Dar es Salaam na imepata umaarufu kutokana na ushiriki wake wa mashindano ya Kombe la Ndondo.

Baada ya kupanda na kushuka kwa beki huyo, Mwanaspoti lilimtafuta na kupiga naye stori ambapo alieleza safari yake ya soka na mambo mbalimbali aliyokutana nayo.


MAISHA YA YANGA

Mtoni alijiunga na Yanga Desemba 2018 akitokea Lipuli ya Iringa, na beki huyo anasema maisha yake katika klabu hiyo yalikuwa mazuri, licha ya kutofikia malengo ambayo alijiwekea ya kuendelea kufanya vizuri kama mashabiki walivyokuwa wanamjua.

“Unapocheza klabu kubwa kama Yanga unakutana na mambo mengi kuanzia ndani na nje ya uwanja. Kila shabiki anataka ucheze kwa kiwango kikubwa bila kushuka kwenye kila mechi. Hali hiyo inasababisha kujikuta unakuwa na presha muda wote na kushindwa kufanya vizuri,” anasema.


KUONDOKA YANGA

Sonso anasema kuondoka kwake Yanga ilikuwa ni jambo la kuumiza katika maisha yake kwani aliamini kuwa bado ana nafasi ya kufanya vizuri na kuwaaminisha mashabiki kuwa uongozi wa Yanga haukukosea kumsajili.

“Nakumbuka siku moja niliitwa na kiongozi mmoja (jina tunalo) akaniambia anasitisha mkataba wangu, hivyo nitafute klabu nyingine ya kuchezea. Kwa kweli iliniuma sana, lakini nilichukulia kawaida tu kama changamoto za kimaisha,” anasema.


ZAHERA FRESHI TU

Beki huyo anasema katika maisha yake ya soka hatakaa amsahau aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera baada ya kugundua kipaji chake na kuamua kumpeleka katika timu hiyo.

“Wakati nipo Lipuli tulicheza na Yanga na baada ya ile mechi Mwinyi Zahera akaniambia kijana una uwezo mkubwa sana, hivyo tutawasiliana,” anasema Sonso.

“Nikachukulia masihara, lakini kumbe alikuwa ana nia ya dhati ya kunisajili. Dili likakamilika na nikatimiza ndoto zangu za kucheza klabu kubwa hapa nchini, jambo ambalo sitakaa nilisahau moyoni mwangu daima.”


KULIKONI KAGERA?

Sonso anasema hakuwa na maisha mazuri baada ya kujiunga na Kagera Sugar, lakini yote aliyopitia amesahau na anachotaka ni kurejea katika kiwango alichozoweleka.

“Mchezaji yeyote anapitia changamoto kama ilivyonitokea, lakini siwezi kusema kuwa nimefeli, bali nimechukulia hasi ili kuhakikisha narejea katika kiwango changu bora,” anasema.


SOKA LIMEMLIPA

Mchezaji huyo anasema kupitia mpira wa miguu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa tangu alipoanza kucheza, ingawa hawezi kuweka wazi vitu ambavyo amevifanya katika maisha yake.

“Soka limenilipa, namshukuru Mungu, nimefungua biashara mbalimbali ambazo zinaniongezea kipato ukiachilia mbali kazi yangu mama ya kucheza mpira,” anasema.


MAISHA NJE YA SOKA

Sonso anasema anapenda kuangalia movie mbalimbali za ndani na nje ya nchi, kwani hujikuta akijifunza mambo mengi kwenye maisha kupitia tamthilia hizo.


UHUSIANO NA MKWASA

Beki huyo anasema amekuwa na mawasiliano mazuri na kocha Boniface Mkwasa tangu wakiwa Yanga, jambo lililomvutia kujiunga naye tena Ruvu Shooting baada ya mkataba wake na Kagera Sugar kumalizika.

“Mkataba wangu ulipomalizika Mkwasa alinipigia simu na kuniambia ananihitaji. Binafsi nilifurahi sana kufanya naye kazi kwa sababu natambua uwezo wake, unaweza kunifanya kuwa bora na kurejesha makali yangu kama ya mwanzo,” anasema.


MSHAMBULIAJI TISHIO

Mchezaji huyo anasema Ligi Kuu Bara ina washambuliaji hodari ambao wamempa akili na maarifa ya kutafuta namna ya kupambana nao uwanjani.

“Washambuliaji wengi ni wazuri. Siwezi kuwataja kwa majina, ndio maana wanaweza kufunga mabao. Kwa maana hiyo kama mlinzi unatakiwa kuwa makini na yule ambaye unadhani ni tishio,” anasema Sonso.


CHANGAMOTO, MALENGO

Sonso anasema amepitia milima na mabonde hadi kufikia alipo, licha ya wengi kumuona kama alipata zali tu la kucheza Yanga na Taifa Stars.

“Nilianza kucheza soka timu za madaraja ya chini huko mtaani katika mitaa ya Magomeni, Mwananyamala na Kinondoni lakini nilicheza Ndondo Cup nikiwa na timu ya Kauzu FC mwaka 2016,” anasema.

“Baada ya hapo nilichukuliwa na Lipuli msimu wa 2016-2017, tukafanikiwa kuipandisha Ligi Kuu na kupata namba katika kikosi cha kwanza huku nikiwa nahodha.”

Kwa sasa Sonso anasema anataka kufanya vizuri akiwa na Ruvu Shooting tofauti na alikokuwa mwanzo ambako alikuwa kwenye kipindi kigumu. “Nataka watu wamuone Sonso yule wa Lipuli ambaye kila mmoja aliona kiwango changu. Hivyo namuomba Mungu anisaidie na kuniongoza kutimiza kile ninachokitamani.”