SIO ZENGWE: Zawadi za Afcon 2023 ziende kwa wachezaji

Mara nyingi tunashangazwa na migogoro ya wachezaji wa mataifa makubwa ya Afrika Magharibi kudai posho na wakati mwingine kufanya mgomo wakati wa fainali za Kombe la Dunia.

Huwa tunashangaa kwa sababu nchi hizo kama Nigeria, Cameroon, Ivory Coast na Senegal zina wachezaji ambao wanalipwa vizuri kwenye klabu wanazochezea barani Ulaya, kiasi kwamba suala kama posho za Sh300,000 (kama Dola 150) kwa siku haziwezi kuwasumbua.

Isitoshe, baadhi kama Sadio Mane au George Weah wakati alipokuja Tanzania na timu yake ya Liberia, huweza hata kugharimia safari na malazi ya timu, hivyo iweje kuwepo na mgogoro wa posho?

Wakati Cameroon ilipokuja Tanzania ndio nilihisi moja ya matatizo yanayosababisha migogoro ya posho. Cameroon walidai ada kubwa ya kushiriki mchezo huo, lakini tuliwashusha hadi walipofikia uwezo wetu wa kumudu kulipa.

Baada ya mchezo tulienda hotelini kwa ajili ya kuwalipa hiyo ada ya ushiriki. Baada ya viongozi kupokea fedha hizo kidogo na kusaini nyaraka, walianza kugawana hapohapo mbele ya macho yetu. Walijua hakuna mchezaji atakayeulizia ada ya mchezo kwa sababu ya kariba ya wachezaji waliokuwa nao na mambo mengine.

Kumbe wachezaji wa mataifa makubwa kama hayo huwa hawafanyi migomo ya posho kwa sababu ya njaa, bali kutaka kuwawajibisha viongozi wao kwa soka la nchi.

Kama wanadiriki kudhulumu wachezaji nyota duniani wa hadhi yao vipi huko ndani ya nchi? Fedha zinakwenda kweli kule zinakotarajiwa? Zinakoelekezwa?

Wakati fainali za Mataifa ya Afrika zilipopamba moto kwa matokeo ya kutotarajiwa, Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Patrice Motsepe alisema kiwango hicho kilichoonyeshwa kwenye fainali za mwaka huu kimetokana na kuongezwa kwa fedha zawadi kwa washindi.

Alisema mapato ya wachezaji walio timu za taifa za nchi za Afrika yanatofautiana sana, kwa maana wapo wanaolipwa vizuri na wale wanaolipwa kiwango kidogo.

“Wachezaji wengi (kwenye fainali za Afcon) hawalipwi fedha kwa kiwango sawa na nimejifunza kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kama ukiongeza fedha ambazo zinakwenda mifukoni mwao na ukawaambia tumeongeza fedha za zawadi, itawahamasisha kwa kiasi kikubwa,” Motsepe aliiambia BBC Sport Africa.

Maana yake fedha za zawadi haziwezi kupangiwa shughuli nyingine labda kwa ridhaa ya wachezaji wenyewe.  Na lazima kuwepo na makubaliano kabla ya kuanza kwa mashindano kwa kuwaambia wachezaji watapata nini kwa kila hatua watakayoishia.

Hata mgogoro wa nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar, Haroub Canavaro na chama cha soka cha visiwani humo, ulitokana na suala hilo.

Kwa kawaida, Rais Paul Kagame huelekeza fedha za zawadi kwa washindi wa michuano ya Kombe la Kagame, ziende kwa wachezaji, na fedha hizo hugawiwa taslimu pale uwanjani.

Kwa kulijua hilo, Canavaro hakufanya ajizi baada ya kukabidhiwa fedha uwanjani. Aliita wachezaji wenzake na wengine waliostahili mgawo na wakagawana hapo hapo uwanjani, kitendo kilichozua hasira kwa viongozi wa ZFA hadi wakatangaza kumfungia.

Cha msingi hapa ni fedha hizo ziwafikie wachezaji. Fainali za Afcon 2023 zimemalizika Jumapili, huku Tanzania ikiondolewa hatua ya makundi ambako kwa mara nyingine imeshika mkia.

Lakini hilo halijaifanya iondoke mikono mitupu. Kwa mujibu wa CAF, timu sita ambazo katika makundi yao zilimaliza mkiani, zitaondoka na Dola 500,000 za Kimarekani kila moja.

Yaani Tanzania inatakiwa ilipwe takriban Sh1.3 bilioni kwa kushika mkia kwenye kundi la Afcon 2023.

Kwa mujibu wa Motsepe, fedha hizi zinatakiwa ziende kuwatia nguvu na kuwahamasisha wachezaji wetu.

Sijui kama kuna makubaliano hayo ama hali itakuwa kama kwa wale vijana wadogo ambao waliambia fedha zao za zawadi zitaenda kuimarisha miundombinu katika kituo cha soka cha Tanga.

Ni muhimu hili likajulikana mapema ili lisivuruge wachezaji ambao hadi sasa wamekuwa wakijitoa kwa moyo wao wote kutetea taifa.

Ni vizuri hili likatolewa taarifa mapema wakati huu tukijiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) ambazo zitafanyika mwaka huu nchini Tanzania, Kenya na Uganda ikiwa ni majaribio ya Afcon 2027 ambazo nchi hizi tatu zitaandaa mwaka 2027.

Kwa mujibu wa CAF, bingwa ataondoka na dola milioni 7, mshindi wa pili dola milioni 4, wakati timu zilizofungwa mechi za nusu fainali zitapoozwa kwa dola milioni 2.5 kila moja.

Timu nane zilizoondolewa katika raundi ya 16 bora, kila moja itapata dola 800 milioni, wakati timu mbili zilizoshika nafasi ya tatu lakini hazikusonga mbele kwenda hatua ya mtoano zitapata dola 700 milioni.

Ni muhimu basi kwa mamlaka, ambayo ilisema ilishafanya majadiliano na wachezaji kuhusu kila kitu, ikafanyia kazi suala hilo mapema.

Na wachezaji wakijua kuwa fedha kama hizo zinakwenda mifukoni mwao, vita ya kupigania nafasi kwenye timu ya taifa itakuwa kubwa na matokeo yake ni kuwa na timu bora kabisa.