SIO ZENGWE: Yanga ilimsajili Baleke kisiasa zaidi

Muktasari:
- Ni mshambuliaji ambaye hupewa jina la “mbwa mwitu ndani ya boksi (au fox in the box’ kwa kuwa ndilo eneo ambalo analijua vizuri na analitumia vizuri.
JEAN Baleke ni mmoja wa washambuliaji hatari anapokuwa ndani ya eneo la penalti kutokana na uwezo wake wa kutokea mipira inayokatiza mbele ya goli na kuisukumia wavuni, au kujitengenezea nafasi nzuri ya kupewa mpira ili amalizie.
Ni mshambuliaji ambaye hupewa jina la “mbwa mwitu ndani ya boksi (au fox in the box’ kwa kuwa ndilo eneo ambalo analijua vizuri na analitumia vizuri.
Hivyo kwa klabu ambayo inataka huduma yake ni lazima iwe imemsoma makali yake na inaona inao wachezaji wa kumzunguka ili aweze kutumia vizuri kipaji chake cha kutikisa nyavu.
Ukimsajili Baleke halafu ukategemea afanye kazi ya kusaidia kushinikiza timu pinzani ipoteze mpira au yeye mwenyewe atafute mpira na ikiwezekana kupokonya wapinzani, utakuwa hujui vizuri huduma anayoitoa kwa ufasaha kwa timu yake.
La! Basi umsajili kwa makubaliano kwamba uwezo wake ndio utamuwezesha kupata namba katika kikosi kinachoanza na si kumsajili kwa kuwa unajua makali yake na udhaifu wake wa kutoweza kusaidia kupokonya mipira au kufunga magoli ya mipira ya mbali.

Nilipoona Baleke amesajiliwa Yanga huku kiungo kama Clatous Chama akiongezwa kwenye kikosi cha mabingwa hao, nikajua labda viongozi waliona jinsi mshambuliaji huyo anavyohitaji msaada wa kiungo mtulivu kwenye eneo la mwisho kama Chama.
Kwamba waliona ubora wa Baleke golini lakini wakaona udhaifu wake wa kutengeneza mabao kutoka mbali na hivyo alihitaji pia huduma ya kiungo wa juu mwenye jicho la pasi ya mwisho na utulivu wa hali ya juu golini na ndio maana ‘kifurushi’ cha Baleke kikamjumuisha Chama.
Kilichonishangaza ni wingi wa washambuliaji wa kati ambao walishathibitisha ubora wao msimu iliyopita. Hakukuwa na maswali kuhusu ubora wa Clement Mzize kwa jinsi ambavyo kila uchao anaonyuesha makali zaidi tangu aanze kupewa nafasi wakati wa Nasreddine Nabi.

Hakukuwa na maswali kuhusu Kennedy Musonda kwa jinsi alivyoshirikiana na Fiston Mayele kusaidia kuipeleka Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho na jinsi alivyojitahidi kuziba nafasi ya Mcongo huyo aliyetimkia Pyramids ya Misri.
Na hakukuwa na maswali kuhusu Prince Dube kutokana na uwezo mkubwa wa kutikisa nyavu na kutoa pasi za mabao kwa kipindi chote ambacho alipata nafasi ya kucheza akiwa Azam, japo majeraha yalikuwa yanamuweka nje mara kwa mara.
Kwa majina hayo matatu usingefikiria kuwa Yanga ilikuwa na haja ya kumsajili Beleke, mshambuliaji ambaye alishajijenga kama mchezaji wa kikosi cha kwanza cha timu yoyote akiwa kwenye umri wa miaka 23.
Ungetemea mshambuliaji wa nne kusajili angekuwa chipukizi anayeinukia ambaye angetumia muda wa kukaa benchi na wa mazoezi kujifunza kutoka kwa nyota kama hao watatu kama Mzize alivyochukuliwa Yanga na kujifunza kwa nyota wenye uzoefu aliowakuta.

Kumchukua Baleke ilikuwa ni uamuzi wa kumuweka kocha yeyote katika matatizo makubwa ya kufanya uamuzi, hasa kwa nchi kama hii ambayo mashindano ni machache hivyo kila mechi ni muhimu inayohitaji kocha apange kikosi cha ushindi wakati wote.
Hii ni kwa sababu hata mashindano kama Kombe la TFF ni nadra sana kwa klabu kubwa kama Simba na Yanga kukutana na klabu za madaraja ya chini zinaweza kumpa kocha fursa ya kutumia wachezaji tofauti, hasa vijana wadogo na wale ambao anataka kuwa na uhakika nao kwa kuwatumia katika hatua za awali za mashindano kama hayo ya Kombe la Shirikisho.
Kwa kawaida timu za Ligi Kuu huanzia hatua ya 32 bora ambako ni nadra sana kukutana na timu za Ligi Daraja la Kwanza. Mara nyingi hukutana na timu za Championship na baada ya hapo ugumu hurejea kama ule wa Ligi Kuu.
Katika hatua hizo, kocha ambaye kipimo chake ni matokeo mazuri kwa kila mechi, atataka kutumia kila silaha aliyo nayo na anayoiamini na iliyothibitisha ubora wake ili apate matokeo mazuri.

Kadiri siku zilivyoenda nilijua sababu za Miguel Gamondi na mrithi wake wa sasa, Sead Romovic kutomtumia mshambuliaji huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Na kadiri habari zinavyozidi kusambaa na kuthibitishwa na ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe, najiona nilikuwa sahihi kufikiria kuwa Baleke alikuwa ziada kwenye usajili wa Yanga.
Kwa jinsi uongozi wa Yanga ulivyoweza kukusanya wachezaji nyota katika kipindi cha miaka minne hadi vigogo hao wakafanikiwa kutengeneza tena jina barani Afrika, sifikirii kwamba hawakuweza kung’amua kuwa walikuwa wanamsajili mchezaji ambaye kwa vyovyote vile angekuwa ziada.
Sasa kwanini walimsajili wakati jicho lao la kuangalia uwezo wa wachezaji limekuwa ni bora?
Ni kweli walitaka kwa dhati huduma ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba? Je, hawakujiuliza sababu za watani wao kuachana naye? Waliwasiliana na benchi la ufundi wakashauriwa wamsajili?
JIbu linaloweza kuwa rahisi na la ukweli ni kwamba Yanga walimsajili Baleke kisiasa. Kuonyesha kuwa viongozi wanaweza kuwapora wapinzani wao mchezaji yeyote, hata kama hana manufaa kwao. Kucheza juu ya siasa za mashabiki wa Simba na Yanga. Haitakiwi ifike huko katika kuharibu mipango ya mchezaji na kuamua kumtelekeza katikati ya msimu mchezaji ambaye kwa kawaida hutakiwa kuwa kwenye kikosi kinachoanza.
Kwa kifupi, Yanga ilimsajili Baleke kisiasa na isipomalizana naye vizuri ataongezeka katika orodha ya wachezaji walioishtaki timu kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na uamuzi ukawa wa kuwalipa maelfu ya dola.