SIO ZENGWE: Tuhuma za hujuma alizotoa Kaze zilinistua

Monday February 22 2021
zengwe pic

WIKI iliyopita ilikuwa ngumu kwa klabu ya Yanga baada ya kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Kagera Sugar katika mechi ya kwanza kwa klabu hiyo kuruhusu zaidi ya mabao mawili katika mechi moja msimu huu.

Ni matokeo ambayo kwa timu yenye kiu ya ubingwa, kongozi anaweza kujikuta anasema lolote hasa baada yay ale matukio ambayo klabu hiyo inaamini kuwa yangeweza kuipa penati ambazo zingeipa ushindi na kuweka hai matumaini yake ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya kuukosa kwa miaka miwili.

Na kwa matukio haya adhabu zinazotolewa na Shirikisho la Soka (TFF) dhidi ya viongozi na wafanyakazi wa klabu hiyo huku madai yao na rufaa zikiwa hazisikilizwi, ungetegemea kiongozi wa Yanga kushindwa kujizuia na kuropoko lolote lile dhidi ya shirikisho hilo na waendeshaji wa Ligi Kuu ambao ni Bodi ya Ligi.

Lakini viongozi walidhibiti pumzi zao na kutoa tamko linalohoji masuala kadhaa huku wakitoa mfano wa maamuzi ambayo wanaona yanaweka maswali mengi kwa waendeshaji mpira na kuzua tafsiri ambazo zinaweza kusababisha madhara. Na uongozi uliishia kwa maswali kwamba wenye dhamana wana timu ambazo wanaona zinafaa kutwaa ubingwa, au wanataka Yanga ijitoe na mengine kadhaa.

Nawasifu viongozi wa Yanga kwa kudhibiti pumzi zao badala ya kuibuka na majumisho kwamba kuna njama dhidi yao na kupandisha hasira mashabiki wao ambao wanaweza kufanya lolote wakati wowote. Zile picha za jezi na panga zilinitisha hadi nikajiuliza kama wenye dhamana wanaona kinachoendelea na wanajua athari zake.

Hata zile hekaheka kabla ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar zilituma salamu kwamba mambo si shwari.

Advertisement

Lakini kwa kuwa viongozi hawakufikia hatua ya kuwaachia mashabiki na wanachama waamue wanavyotaka kwa kuwa hapo ingekuwa mshikemshike.

Kilichonistua ni kauli ya kocha wa Yanga, Cedric Kaze kufikia majumuisho kwamba timu yake inahujumiwa. Sikutarajia kusikia kauli kama hiyo kutoka kwa kocha kwa kuwa ni kauli ya kisiasa na si kiufundi.

Kwa kawaida makocha wanapoulizwa na waandishi kuhusu uamuzi, hujipa muda kuangalia vizuri matukio yenye utata ili aweze kuzungumzia na kama yalikuwa bayana, basi huzungumzia matukio hayo na kuonyesha udhaifu wa uamuzi bila ya kuhusisha na njama nyingine zozote au hujuma kwa kuwa alichokiona ni matukio tu.

Kwenda mbali na kuhusishs uamuzi mbovu au makossa ya uamuzi na njama za kuhujumiwa ni kosa ambalo linaweza kusababisha aadhibiwe kwa kuwa ni vigumu kuthibitisha kuwa uamuzi fulani mbovu au makossa fulani yana uhusiano na njama za kuihujumu timu au kuibeba timu fulani.

Ni kweli uamuzi mbovu unaweza kutokana na njama za watu fulanifulani, lakini pia hutokana na ubovu wa waamuzi wenyewe. Ni bahati mbaya sana mechi za Simba na Yanga huangaliwa sana na kufuatiliwa kila tukio, lakini wakati mwingine unapoangalia timu nyingine unaona kabisa kuna ombwe kubwa la uzoefu katika waamuzi wetu.

Wengi huingia uwanjani kama viranja, kama polisi, na kama mahakimu ambao ni vigumu kuzungumza nao kwa kawaida. Kamera zinatuonyesha wakitoleana macho ya hasira na wachezaji na wapo wanaothubutu hadi kuwasukuma wachezaji, jambo linalotengeneza mazingira ya vurugu iwapo wachezaji nao watahamaki.

Wenzetu wameweka utaratibu wa wataalamu wa uamuzi kukutana kila baada ya raundi kujadili matukio yote na kuyatolea mwongozo, jambo ambalo huwafanya waamuzi wawe makini wakijua kila wafanyacho kitapitishwa katika chujio na watalaamu na si kamati ya masaa 72.


Imeandikwa na Angetile Osiah

Advertisement