SIO ZENGWE: Samatta amekuja, tunasema anaogopa kuumia!

Tuesday October 12 2021
zengwe pic
By Angetile Osiah

WIKI iliyopita lilitokea tukio la kufedhehesha kwa mshambuliaji wetu nyota, Mbwana Samatta na soka kwa ujumla.

Ilikuwa ni baada ya timu ya taifa, Taifa Stars kulala kwa bao 1-0 mbele ya Benin kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya makundi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia.

Stars ilifanya jitihada kubwa na kupata nafasi mbili za wazi ambazo zilipotezwa na Simon Msuva na John Bocco katika mazingira ya kimchezo ambayo humtokea yeyote yule, hata wale nyota duniani kama Ronaldo, Messi na Mbappe.

Kwa namna fulani, Wabenin walikuwa wametuzidi kimbinu na mfungaji wa bao alikuwa na utulivu mkubwa na uwezo wa kuamua matokeo, kiasi kwamba huwezi kuwalaumu sana mabeki wetu kwa kushindwa kufunga njia mapema, wala kipa Aishi Manula kwa kushindwa kuufikia mpira ule wa mbali ulioelekezwa upande wake wa kushoto.

Samatta, kama ilivyo kwa makocha wengi, alikuwa akitokea upande wa kushoto, hivyo kazi ambayo amezoea kuifanya katika ngazi ya klabu, akawa haifanyi; kazi ya kumalizia juhudi za wengine kwa kusukumia mpira wavuni.

Badala yake akawa akihaha kulia na kushoto, kati na nyuma kwa ajili ya kutafuta mipira—wakati mwingine kusaidia kuzuia na kuipeleka timu mbele na hivyo haikuwa rahisi kumuona akiruka juu mbele ya goli kujaribu kufikia mipira ya krosi wala kuchupa kujaribu kusukumia wavuni mipira ya chini ya krosi. Badala yake alionekana akijaribu kushuti kutoka mbali, jambo ambalo haliwezi kuwa la uhakika kwa asilimia kubwa.

Advertisement

Pengine kutokana na kutopewa majukumu yale ambayo huyabeba kwenye klabu, baadhi ya watu ambao usomaji wao wa mchezo hutokana na matokeo wakaanza kulaumu kwamba ‘eti’ Samatta huwa hajitoi kwa uwezo wake wote anapoitwa kuchezea timu ya taifa kwa madai kuwa anaogopa kuumia.

Binafsi nilistuka nilipoona yule bwana anamuuliza Samatta swali kama lile.

Muuliza swali alitakiwa awe amemuona vizuri Samatta kwenye mchezo ule kabla ya kumtupia swali na kusingizia ‘eti’ mashabiki ndio wana mtazamo huo.

Pengine ni kutokana na kucheza soka katika ngazi ya juu duniani, Samatta alikuwa na busara za kutosha kumjibu muuliza swali. Alimjibu kirahisi tu kwamba amezungumza na hao mashabiki lini na kwamba anaamini hawasemi hivyo.

Ni jambo rahisi tu. Kama Samatta angekuwa hataki kuja kucheza kwa kuhofia kuumia, angeweza hata kutangaza kustaafu kuchezea timu ya taifa. Hakuna ambaye angemlazimisha aje.

Na wapo ambao hutumia hata madaktari wa klabu kumtangaza kuwa majeruhi, hivyo kuhitaji mapumziko ya muda mfupi kwa lengo la kumkwepesha kuchezea nchi yake na kumuandaa kwa mchezo muhimu unaofuata wa klabu.

Samatta angeweza kutumia njia yoyote asije. Na hapo angeweza kuelekeza nguvu zake zote katika klabu yake kuliko kuja kuteseka kwenye timu ambayo anaweza hata asichukue posho na asione athari, achilia mbali kuumia na kushindwa kucheza huko kwenye ajira yake.

Swali lile lilimkosea heshima nyota na nahodha wetu, ambaye mafanikio yake yamekuwa hamasa kwa wachezaji wengi vijana ambao sasa wameanza kuondoka kwa wingi kwenda kucheza nje.

Tunahitaji kumpa Samatta heshima kubwa kwa jinsi ambavyo amekuwa akijitoa kwa taifa lake, kulinganisha na nyota wengine ambao hutafuta visingizio kibao kukwepa majukumu ya taifa.

Kile kisingizio cha kutafuta views nyingi kwa kuuliza maswali ambayo ‘eti’ mashabiki wanayataka, kisitufikishe mahali ambapo tunaweza hata kuichezea lulu yetu.

Tunahitaji uelewa wa hali ya juu wa mchezo kabla ya kutengeneza maswali yetu kwa wachezaji na kocha baada ya mchezo ili kuepuka kuibua matatizo ambayo hata hayakutakiwa yawepo.

Tuna wachezaji wachache waliofikia kiwango cha Samatta. Kwa wenzetu hao ni lulu na ni kipenzi cha mashabiki, hivyo ni vigumu kukuta wakiulizwa maswali ya kuwafedhehesha. Tulinde vito vyetu.

Advertisement