SIO ZENGWE: Ni muda sasa Azam bado haijazi mashabiki
KUNA kikundi kimoja nyuma ya lango kilishangilia muda wote wa mchezo baina ya Azam na TP Mazembe na vingine viwili viko pembeni vikifanya kazi kama hiyo.
Si wakati bao limefungwa wala wakati mchezo ukiendelea bila mashambulizi, vikundi hivi vinashangilia na shangwe zao zikiambatana na ngoma na wakati mwingine kutembea hatua chache.
Hata upande wa jukwaa kuu kuna watu wachache. Sehemu kubwa ya uwanja huu unaoweza kuchukua takriban watu 7,000 iko tupu, ingawa kelele ni hizo za ngoma na watu wakicheza wakati wote wa mchezo.
Haya ndiyo mandhari ya karibu mechi zote zinazochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, moja ya viwanja vizuri vya klabu binafsi. Azam Complex iko pembeni kidogo ya wilaya ya Temeke, na hivyo kwa mashabiki wa soka ambao hutumia mchezo huo kama burudani ya kupitia na si kuifuata, kwao huwa vigumu kufika hata kufuata mechi kati ya Azam na Prisons, ambazo zinafanya vizuri katika Ligi Kuu.
Hata zile mechi za Taifa Stars hushuhudiwa na watu wachache, ingawa ziko baadhi ambazo watu walifurika. Jaribio la Azam kuzipeleka Yanga na Simba lilikwamishwa na hoja za watu wanaopenda kupitia uwanjani kuona soka na si wale wanaotenga muda wao kuifuata burudani hii kubwa.
Hapa ninachoona ni kuwa hao wanaotarajiwa kuujaza uwanja ni mashabiki wa Simba na Yanga, ambao timu zao zinatumia ama Uwanja wa Benjamin Mkapa au wa Uhuru, hivyo kuifuata Azam kwenye uwanja wake, hata inapocheza na TP Mazembe, kwao ni kupoteza muda.
Azam, kama zilivyo klabu nyingine nyingi, imeshindwa kupika mashabiki wake zaidi ya vile vikundi vya ushangiliaji ambavyo pengine hulipwa kwa ajili ya kazi hiyo, lakini mioyoni mwa wanavikundi hivyo ni Simba na Yanga.
Ni kazi ngumu kuanza kupika mashabiki wako katika nchi kama hii ambayo mtu huanza kuzipenda Simba na Yanga akiwa bado mdogo na pengine kuanza kufundishwa na mzazi na hata kuvishwa rangi za klabu hizo akiwa hata hajui maana yake.
Na katika ulimwengu huu wa teknolojia, tunashuhudia uthibitisho huo. Yaani kila anayeipenda Yanga, basi mwanae lazima awe anaipenda Yanga. Hali kadhalika na Simba. Tunashuhudia picha za watoto wadogo wakiwa wamevishwa jezi za timu hizo mbili, na pengine hata kutoa maneno ya kashfa dhidi ya timu nyingine.
Jambo langu leo ni Azam na klabu nyingine kushindwa kutengeneza mashabiki wao pamoja na mafanikio yote ya uwanjani ambayo Azam imeyapata tangu ilipoanzishwa.
Wakati kampuni ya SSB inakubali kuwa na klabu ya soka, sidhani kama ilichokiangalia kikubwa ilikuwa ni timu kupata ushindi wa uwanjani. Nadhani hoja kubwa ilikuwa ni ya kibiashara kuwa ianzishwe klabu ambayo itatumika kusaidia kuendeleza biashara zilizo chini ya kampuni hiyo.
Ni dhahiri kuwa moja ya kazi ambazo zinaweza kufanikisha kuendeleza biashara hizo ni mafanikio uwanjani kwa kuwa yanatangazwa hadi kufika mbali. Lakini mafanikio hayo kama hayaambatani na timu kuungwa mkono na idadi kubwa ya watu, hayawezi kuwa imara.
Kwa hiyo, viongozi wa Azam walikuwa na kazi kubwa ya kujenga wigo mpana wa mashabiki ambao wanaweza kujaza uwanja japo wakati timu hiyo inapocheza mechi ngumu nyumbani dhidi ya timu kali, ukiachilia mbali Simba na Yanga.
Hiyo inamaanisha kuwa uongozi unapaswa kuwa na programu mbalimbali za kuanza kujenga kundi jipya la mashabiki hata kwa kutumia Azam TV.