SIO ZENGWE: Kwa heri msimu mbovu 2020/21, tumejifunza mengi

Muktasari:

WAKATI janga la ugonjwa wa virusi vya corona, covid-19, lilipochachamaa kote duniani huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likiwa limeutangaza kuwa ni ‘dharura ya dunia’, nchi nyingi zilisimamisha shughuli za mikusanyiko, michezo ikiwamo.

WAKATI janga la ugonjwa wa virusi vya corona, covid-19, lilipochachamaa kote duniani huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likiwa limeutangaza kuwa ni ‘dharura ya dunia’, nchi nyingi zilisimamisha shughuli za mikusanyiko, michezo ikiwamo.

Na hali ilipoanza kuwa nafuu huku michezo ikiruhusiwa kuendelea bila ya mashabiki, baadhi ya nchi ziliendelea kuchukulia janga hilo kuwa ni dharura ya dunia.

Zile zilizoweza na ambazo kanuni zake zilizingatia kuibuka kwa majanga yaliyo juu ya uwezo wa binadamu yanayoweza kuvuruga shughuli za kawaida, zilikatisha mashindano yao kwa kutangaza bingwa na wawakilishi wengine wanaotokana na ligi zao.

Hii ilifanywa kwa kuzingatia kuwa kuna kesho. Yaani msimu wa mapumziko uwepo wa kutosha na maandalizi kwa ajili ya msimu mpya yawe na muda mzuri, ili msimu unaofuata usiathiriwe sana na kuchelewa kumalizika kwa ligi, wachezaji kutopata muda wa kutosha wa kupumzika, walimu kutopata muda wa kutosha wa kuandaa timu zao na mambo mengine mengi kama biashara yanayoambatana na michezo.

Matokeo yake, Ulaya yote imeshamaliza msimu wao wa 2020/21, lakini bado Afrika inahaha kwa kuchelewa kumaliza msimu wa 2019/20 na kuchelewa kuanza kwa msimu wa 2020/21 na hakuna shaka kwamba hali hii itaendelea msimu ujao. Na sababu ipo kubwa tu; janga la covid-19 na kifo cha Rais John Magufuli.

Ni kweli corona ilituyumbisha na kwa mara ya kwanza tulipata msiba wa Rais ambaye yuko madarakani, lakini ni kwa kiasi gani tulichukulia masuala hayo kuwa ni dharura na hivyo kuhakikisha tunafanya mambo yetu kidharura?

Katika dharura kama hizo mbili, usingetegemea timu iachiwe mwezi mzima bila ya kucheza mechi hata moja eti kwa sababu ina majukumu ya kimataifa. Usingetegemea klabu za Yanga na Simba zisiingie uwanjani wiki nzima eti kwa sababu zina derby yao.

Usingetegemea mechi zichezwe kama kawaida kana kwamba hakuna kitu kinachoweza kusababisha msimu kuchelewa kuisha. Hata Chama cha Soka Ulaya (Uefa) kilihamishia mechi za hatua za mwisho za Ligi ya Mabingwa nchini Ureno na mechi hizo zikawa za mkondo mmoja ili kuhakikisha michuano hiyo inamalizika mapema hasa kutokana na ukweli kwamba kwa kuhamishia mechi kituo kimoja, hakuna timu ambayo inakuwa mwenyeji na hivyo mechi moja ingetosha.

Tulishindwaje kutenga mikoa maalum kwa ajili ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ili kurahisisha usafiri na kupunguza muda wa timu kusafiri kutoka kwake hadi kituoni. Hali kadhalika, hakukuwa na wazo mbadala la kuendesha Ligi Kuu katika mazingira ya dharura ili iishe kwa wakati?

Hatukuwa na wazo mbadala la kuendesha Kombe la FA ili fainali ichezwe mapema kabla ya kuhitimishwa kwa msimu na badala yake mechi ya fainali ndio inachezwa siku ya kumaliza msimu? Wenzetu hujua tarehe ya fainali na uwanja siku msimu unapoanza. Hivi kweli tunaweza kusema bado hatujafikia kiwango hicho kwa kuwa sisi ni Watanzania?

Leo hii, timu za FDL zimefuzu kucheza hatua ya mtoano (play off) ili kujua kama zinapanda daraja msimu ujao, zinasubiri kwa takriban wiki tatu au zaidi ili zipangiwe tarehe za kukutana na wapinzani wao kutoka Ligi Kuu, ambayo imemalizika jana. Ni kwa kiasi gani wamiliki wa klabu hizo watamudu kuwaweka pamoja wachezaji hadi kipindi cha mechi hizo? Ni kwa kiasi gani mechi hizo zitakuwa na ushindani?

Ligi Kuu, Perfect Chikwende amerudi kwao Zimbabwe, Carlinho amerudi kwao Angola, Fiston amerudi kwao Burundi na orodha inaendelea hivyo hivyo… wako waliorudi Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwingineko. Hawa wote wameondoka kabla ya msimu kuisha na baadhi mikataba yao iliisha Juni na hata kama hawakuwa wanapewa nafasi vikosini, utamaduni ni wachezaji wote kuagwa mara baada ya msimu kuisha.

Unawezaje kuwa na ushindani unaotakiwa kama uendeshaji ligi hauzingatii matukio makubwa ya dharura ya kitaifa na yale ya duniani? Katika mazingira haya ni lazima ligi iwe inaudhi, inakera, iliyojaa lawama na manung’uniko na yule anayefurahia kuonekana anabebwa.

Kuna haja kubwa wa kuacha kujificha kwenye kichaka cha kusema, ‘wenzetu wako mbali’ ndio maana mambo yao yanaendeshwa kwa utaratibu mzuri. Huko ni kulea unyonge, uzembe na kutowajibika ipasavyo. Hata kile kichaka cha ‘mbona wao hawakufanya hivyo’, ni ujinga mwingine unaochelewesha maendeleo.