SIO ZENGWE: Akina Tshabalala wamewapa ushindi wachezaji, lakini...

Mwanzoni mwa millennia hii kuliibuka mjadala mkubwa kuhusu malipo ya wanamichezo, hasa wanasoka na wachezaji wa mpira wa kikapu. Baadhi ya viongozi mabahili waliibua hoja kuwa wachezaji wanapata malipo makubwa kupita wanavyostahili.

Hoja kama hiyo ni rahisi kueleweka kwa haraka. Fikiria kwamba mchezaji nyota kama, Mesut Ozil anayechukua dola 350,000 za Kimarekani kwa wiki (sawa na zaidi ya Sh700 milioni za Kitanzania), atazitumiaje ili angalau matumizi yafikie robo ya kiwango hicho kwa wiki.

Kiwango hicho chaweza kuwa mshahara wa miaka hata mitatu kwa mfanyakazi wa kawaida wa nchi nyingi. Kwa hiyo mtu anapojenga hoja kwa kutumia tarakimu kama hizo anaeleweka haraka sana bila ya kuzingatia mambo mengi.

Lakini watetezi wa wanamichezo walikuwa na hoja nzito zaidi. Kwao, hata kiwango hicho kilikuwa bado hakikidhi mahitaji ya wanamichezo na wakataka kuwepo na malipo zaidi ili wachezaji waishi maisha ya uhakika wakati wote.

Walisema kipindi cha mwanamichezo kushiriki michezo kwa kiwango cha juu kinachoweza kumpatia fedha nzuri ni kifupi sana, kulinganisha na wafanyakazi wengine. Mwanamichezo anaweza kudumu katika unyota kwa kipindi kisichozidi miaka kumi, isipokuwa wale ambao si wa kawaida.

Akilipwa kiwango cha kawaida cha mshahara, akiwekeza hataweza kudunduliza kiwango ambacho kitamuwezesha kumudu maisha baada ya kustaafu soka. Hata wafanyakazi wa kawaida ambao wanawekeza katika mifuko ya hifadhi ya jamii, wanahitaji kuchangia kwa miaka 15 ili waweze kupata malipo mazuri ya kila mwezi baada ya kustaafu.

Iweje basi wanamichezo walipwe kwa viwango vya kawaida? Kwa malipo ya viwango vya kawaida, ndio tutakuwa na kundi la wachezaji kama hawa wa kwetu waliocheza kwa kiwango cha juu wakati wa soka la ridhaa, wakapata umaarufu, lakini maisha yao ya sasa hayalingani na sifa walizotengeneza sit u ndani ya nchi bali hata nje.

Tunahitaji kuwa na mfumo wa malipo kwa wachezaji ambao utawahakikishia maisha mazuri ya baadaye na si malipo ya kijungu jiko, yaani ya kumuwezesha kupeleka mkono kinywani. Kuna maisha baada ya kustaafu soka. Na hata mwanamichezo anapofikia ukomo wa kucheza kwa kiwango cha juu na hivyo kulazimika kuchezea timu ambazo uchumi wake si mzuri, anaweza kujikuta akihangaika iwapo hakulipwa vizuri wakati akicheza soka la kiwango cha juu.

Niliposikia kuna Tshabalala, John Bocco na Shomari Kapombe hawajakamilishana na uongozi wao kuhusu hali yao ya baadaye klabuni, nilihisi kuwa suala la maisha yao ya baadaye ndio limezingatiwa zaidi na huenda ndilo linachelewesha wachezaji hao kusaini.

Ingawa lilifuatiwa na sinema nyingi zilizoishia kwa kuwazomea watani wao wa jadi waliokuwa wakisubiri kwa hamu Simba ishindwe kuafikiana nao, suala muhimu lilikuwa maslahi ya wachezaji hao kuzingatiwa.

Natumaini kulikuwa na wakala ambaye alikuwa akifanya mazungumzo na uongozi hadi kufikia makubaliano yaliyofanya waanguke katika nyaraka za Simba. Kama mahitaji yao yalizingatiwa, basi ni ushindi kwa wachezaji, si akina Tshabalala pekee, bali wengine wote wanaotegemea mpira kuendesha maisha yao.

Na kama ilivyo duniani kote, kunapokuwa hakueleweki habari za kusiah kwa mkataba na kutosainiwa mpya huvujishwa na kusambaa kwa kasi ili kustua viongozi na kuwafanya waanze kukimbia kurekebisha mambo mapema, kitu ambacho humnufaisha mchezaji.

Labda ambalo linaweza kuangaliwa vizuri ni kipi kizingatiwe. Ada ya kusaini mkataba mpya au kupandisha mshahara. Maana nilisikia gumzo la “mpeni mzawa hizo Sh100 milioni”.

Kwa kawaida mchezaji anapoongeza mkataba, ada ya kusaini mkataba (sign on fee) haiwezi kupanda kwa kuwa mkataba wake lazima ueleze bonsai anazotakiwa kupata baada ya msimu kuisha, kitu ambacho kitathibitisha ufanisi wake.