Simba ni pesa tu

Muktasari:

SIMBA hawabahatishi, wamejipanga kila idara kwani lengo lao ni kufika levo za juu kabisa kwenye michuano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

SIMBA hawabahatishi, wamejipanga kila idara kwani lengo lao ni kufika levo za juu kabisa kwenye michuano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Hivi sasa kimataifa wamefika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo watakutana na Kaizer Chief ya Afrika Kusini mechi itakayopigwa nchini humo keshokutwa Jumamosi na baadaye watarudiana kwenye Uwanja wa Mkapa.

Mafanikio ya Simba yamekuja baada ya kuamua kuondoka kwenye mfumo wa kizamani wa wanachama na sasa wapo kwenye ukamilishaji wa mchakato wa kampuni.

Tayari Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ alishinda zabuni ya uwekezaji wa Sh 20 Bilioni ambapo sasa wanasubiri hatua ya mwisho ya FCC ili aweke mzigo huo.

Lakini hiyo haijazuia kwa mfanyabiashara huyo maarufu nchini kuweka mkono wake kuipambania Simba ili iwe timu bora na tishio Afrika ndiyo maana wanasajili vizuri, wanalipa mishahara minono kwa wachezaji.

Kupitia Mo Dewji, ni fungu la maana limetumika kutinga hatua hiyo Afrika, fungu hilo ni kuhakikisha wachezaji hawakosi huduma yoyote ikiwemo bonasi wanaposhinda mechi zao iwe ugenini ama nyumbani.

Katika uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti, imebanika kwamba Simba hadi hatua ya makundi imetumia zaidi ya Sh 2.6 bilioni.

Awali, wakati Simba inakata tiketi ya kwanza katika michuano hiyo, ilikuwa na malengo ya kutinga nusu fainali na sasa baada ya kumaliza msimamo Kundi A ikiwa kileleni na pointi 13 itapata nafasi ya kucheza dhidi ya mshindi wa pili wa kundi jingine huku Al Ahly aliyemaliza nafasi ya pili kwa pointi 11 atacheza na mshindi wa kwanza wa kundi jingine.

Mjumbe mmoja wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba alisema walianza mashindano hayo katika hatua ya awali na mpaka wanafika robo fainali walikuwa wamecheza mechi tano ugenini akimaanisha tatu hatua ya makundi na mbili hatua ya mtoano.

Anasema kila mechi moja ya ugenini walikuwa wanatumia si chini ya Dola 70,000 (zaidi ya Sh140 milioni pesa ya Kitanzania). Wakati huo huo, walicheza mechi tano nyumbani na kila moja walikuwa wanatumia si chini ya Dola 70,000 ambazo ni zaidi ya Sh140 milioni.

“Mgawanyiko wa pesa hizo katika mechi zetu za nyumbani tunawalipia marefa na maofisa wengine wa mchezo ambao wanakuwa si chini ya watano na kila mmoja analipwa si chini ya Dola 1000,” alisema mjumbe huyo na kuongezea kuwa;

“Dola 1000 inakuwa katika matumizi yao ya kula, kulala pamoja na mambo mengine ya msingi na pia tunawalipia pia tiketi za ndege ambazo zinakuwa si chini ya Dola 7000, ambazo kwa pesa za hapa nyumbani ni zaidi ya Sh14 milioni.”

Mjumbe huyo anasema gharama nyingine katika mechi zao za ndani wanakuwa na jopo la watu wasiopungua 70, ambao wote wanawalipia kipimo cha Covid-19, ni Dola 100 (zaidi ya Sh230,000) kila mmoja.

Anasema jopo hilo ni pamoja na wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, marefa, watoto wa kuokota mpira pamoja na maofisa wengine wote wa mechi.

“Tukiwa katika mechi za ugenini tunakuwa na msafara wa watu wasiopungua 50 ambao kila mmoja anapima Covid-19.

“Tunakuwa na gharama nyingine kama gari ya zimamoto, ya wagonjwa na matumizi mengine ambayo inakuwa si chini ya Sh10 milioni kwa mechi zetu za nyumbani.

“Kwahiyo hizi gharama nyingine kama gari la kubebea wagonjwa na zimamoto kwa mechi nane za nyumbani tumetumia Sh80 milioni.”

Mjumbe huyo alifafanua gharama kubwa wanayotumia kwa wachezaji wao kama bonasi katika kila mechi wanayocheza kwenye michuano hiyo Afrika.


MECHI ZOTE

Hapa ni bonasi kwa wachezaji ambapo wakishinda dau linakuwa kubwa, wakitoka sare dau linashuka na wakipoteza mechi hawapati chochote.

Mechi wanazoshinda ugenini ama nyumbani huwa wanalipwa kati ya Sh200 milioni na Sh230 milioni wakati sare inakuwa kati ya Sh100 milioni na Sh150 milioni.

Anasema mechi ya ugenini dhidi ya Plateau United walishinda bao 1-0, wachezaji walivuta Sh230 milioni wakati mechi ya marudiano nyumbani iliyoisha kwa sare walitoa Sh150 milioni.

“Katika mechi ya kwanza dhidi ya Platinum ya Zimbabwe wachezaji hawakuvuta kitu kwa sababu walifungwa bao 1-0, lakini mechi ya marudiano Benjamin Mkapa walishinda mabao 4-1, wachezaji walivuta Sh200 milioni.

“Hatua ya makundi tulianza kwa ushindi wa bao 1-0, ugenini dhidi ya AS Vita wachezaji walipata Sh200 milioni, mechi ya pili tulishinda bao 1-0, dhidi ya Al Ahly nyumbani walichukua Sh230 milioni,” alisema na kuongezea;

“Mechi ya tatu tulitoka sare ugenini na Al Merrikh ya Sudan ambapo walipewa Sh200 milioni, marudiano tulishinda bao 3-0, wakachukua tena Sh230 milioni.”

Mjumbe huyo anasema baada ya hapo walicheza mechi ya tano hatua ya makundi na AS Vita na kushinda bao 4-1 bonasi yake ilikuwa ni Sh230 milioni.

Alisema walipokwenda kukamilisha ratiba hatua ya makundi ugenini dhidi ya Al Ahly walifungwa bao 1-0, hapo hawakupata bonasi yoyote.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ anasema mpango wa kutoa bonasi wameuweka kwa ajili ya kuongeza morali kwa wachezaji kushindana kila mechi.

“Hizi bonasi si kama zinatoka klabuni hapana zinatoka mfukoni mwa mtu binafsi na huyo ni Mo peke yake na lengo lake ni kuongeza morali ya wachezaji,” anasema Try Again, huku mjumbe mwingine wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulam Ng’ambi anasema, wanalitaka taji la Afrika.