Simba mpango ni ule ule

Tuesday September 28 2021
simba pic
By Thobias Sebastian

JANA Jumatatu, msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ulianza rasmi huku kila timu ikiwa imejipanga kwa ajili ya kusaka pointi tatu kila mechi watakayocheza na timu pinzani.

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo itaanza mechi yao ya kwanza ugenini Uwanja wa Karume mjini Musoma, wakikaribishwa na wenyeji wao Biashara United. Wote hao wanashiriki michuano ya kimataifa, Simba inashiriki Ligi ya Mabaingwa Afrika na wapinzani wao wametinga hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho aAfrika.

Msimu huu, ligi inaonekana kuwa na mvuto wa aina yake kwa maana ya kupata ushindani kutoka timu 16, pamoja na pesa za udhamini ambazo watazipata kutoka kwa wadhamini mbalimbali.

Kutokana na ushindani huo kila timu ilifanya maandalizi ya kutosha kulingana na mahitaji yao ikiwemo kusajili wachezaji ambao watawapa matokeo matokeo mazuri.

Simba iliweka kambi yao sehemu tofauti, ilianza na Morocco ambako ilicheza mechi mbalimbali za kirafiki na baadaye jijini Arusha nako ilicheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.

Makala haya inagusa maeneo mbalimbali ambayo mabingwa hao watetezi watayapitia msimu huu.

Advertisement


BAJETI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’aliweka wazi kuwa kikosi hicho kwa msimu mmoja kinatumia si chini Sh6 Bilioni kujiendasha kwenye mambo yote ya msingi.

Mo Dewji alieleza pesa wanayotumia kufanya usajili, usafiri wa ndani na nje ya nchi, hoteli, kambi pamoja na gharama nyingine inatumikia si chini ya kiasi hicho.

“Wanalipa mishahara wachezaji, makocha na waajiri wote ni sehemu ambayo gharama hiyo inafikia kwa msimu mmoja jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa Simba kuwa na mafanikio ndani na nje ya nchi.”

Uchambuzi uliofanyiwa na gazeti hili maeneo mbalimbali usafiri wa basi wanatumia mwisho Morogoro ila zaidi ya hapo wanatumia ndege kama ambavyo ilivyo kipindi inasafiri nje ya nchi.


BENCHI LA UFUNDI

Katika kuhakikisha inafanya vizuri msimu huu imeboresha benchi la ufundi kwa kuwaongeza wataalumu wengine wawili ambao msimu uliopita hawakuwepo.

Benchi la ufundi kwasasa linaongozwa na Dider Gomes, ameongezwa kocha msaidizi Hitimana Thiery na Selemani Matola ambaye muda mwingine alikosekana kutokana na kwenda kusoma.

Pia wamemwajili mtaalamu wa tiba ya misuli, Msauzi Fareed Cassim aliyechukuwa nafasi ya Paul Gomes, wana faida ya makocha sita ambao watafanya majukumu tofauti.

Cassim aliyewahi kufanya kazi na Yanga anasema; “Nimefurahi kujiunga Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja jukumu langu ni kuhakikisha kikosi chetu kinakuwa hakina wachezaji majeruhi kwa kuwapa ratiba nzuri ya kufanya mazoezi na namna ya kutunza miili yao,” anasema Cassim na kuongeza;

“Kama ikitokea kuna mchezaji amepata majeraha basi tutaanglia namna gani ya kumpatia matibabu kamilifu na yale ya kuyafuata ili kupona haraka na kurejea uwanjani mapema kwa ajili ya kuipigania timu.

“Nimefurahi kufanya kazi pamoja na wataalamu wenzangu katika eneo hilo Daktari Yassin Gembe na kocha viungo, Adel Zrane ambao tangu nimefika nchini tumekuwa tukishirikiana.”


WALIOSAJILIWA

Wamesajili wachezaji 11 ambao wengine wanaziba mapengo ya nyota wao wawili, Clatous Chama na Luis Miquissone waliouzwa, wapya hao ni Jeremiah Kisubi, Israel Mwenda, Hennock Inonga Baka, Pape Sakho, Sadio Kanoute, Denis Kibu, Dancun Nyoni, Abdulsamad Kassim, Jimson Mwanuke, Yusuph Mhilu na Pater Banda. Sakho anasema kuwa; “Nimekuja hapa kwa ajili ya mafanikio na sitamani kuona hilo linashindikana mpira ni mchezo wa wazi nitapmbana na kucheza katika ubora wangu wote kuona jambo hili linafanikiwa,” anasema Sakho.


WALIOACHWA

Miraji Athumani ndiye pekee aliyeachwa anasema kuwa;” Maamuzi ambayo niliyafanya ni haya kujiunga na KMC ambayo naimani ni timu nitapata nafasi ya kucheza na kutimiza malengo yangu ya kuwa mchezaji mwenye mafanikio,”


MKOPO

Wamewatoa wachezaji wanne kwa mkopo ambao ni Said Ndemla na Ibrahim Ame wameenda Mtibwa Sugar, David Kameta ‘Duchu’ (Biashara United) na Parfect Chikwende aliyetimkia Afrika Kusini. Duchu anasema; “Baada ya hapo ndio niliamua kutafuta nafasi ya kwenda kucheza kwa mkopo na hapa Biashara ni timu sahihi kwani napata nafasi ya kucheza ikiwemo michuano ya kimataifa,”


KUANZIA UGENINI

Msimu uliopita mechi ya kwanza walianzia ugenini Uwanja wa Sokoine Mbeya walicheza dhidi ya Ihefu na kupata ushindi wa mabao 2-1, yaliyofungwa na Mzamiru Yassin na John Bocco.

Msimu huu wanaanzia tena ugenini mechi zao mbili wataanza dhidi ya Biashara United na Dodoma Jiji.


UWANJA

Kama ilivyo kawaida na misimu mingine, Simba watatumia viwanja viwili Uhuru na Benjamin Mkapa kama vya nyumbani labda itokee shida ambayo itakuwa nje ya uwezo wao katika viwanja hivyo.

Wakati huo huo kanuni za ligi zinaruhusu timu zote za Ligi Kuu kuchagua mechi mbili ambazo zitachezwa nje ya uwanja wake wa nyumbani kama itapendezewa kufanya hivyo. Kutokana na aina ya uchezaji wa soka la kupiga pasi nyingi viwanja vya Uhuru na Mkapa ni rafiki kutokana na falsafa za mabingwa hao na huwa wanapata wakati mgumu wanapocheza viwanja ambavyo havina eneo zuri la kuchezea.


MECHI YA DABI

Msimu uliopita Simba hawakupata ushindi walipocheza mechi mbili za Dabi dhidi ya watani zao Yanga ambao mchezo wa kwanza ulimalizika kwa suluhu na wao ndio walisawazisha.

Mechi ya kwanza Yanga walianza kupata bao kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti lililofungwa na Michael Sarpong ambaye kwa sasa hayupo kikosini, Simba lilisawazishwa na Joash Onyango kwa kichwa dakika chache kabla ya mchezo kuisha.

Mechi ya mzunguko wa pili Simba walikubali kufungwa bao 1-0, lilifungwa na kiungo, Zawadi Mauya baada ya kupiga shuti kali lililomgonga Shomary Kapombe na kuzama nyavuni.


MALENGO

Gomes anasema msimu uliopita walichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao ya Jamii na sasa wamepanga kutetea baadhi ya makombe.

“Tuna mashindano mengine Ligi ya mabingwa Afrika msimu uliopita tuliishia robo fainali ila msimu huu tunamalengo ya kufika hatua moja mbele kwani hayo ndio yatakuwa mafanikio kwetu,” anasema Gomes.
Advertisement