Simba inashinda lakini haifurahi

SIMBA juzi Jumatano imeondoka Uwanja wa Benjamin Mkapa na ushindi mwingine wa bao 1-0, dhidi ya Namungo lakini haikuwa na furaha kabla, wakati na baada ya mchezo huo wa Ligi Kuu duru ya 11.
Furaha ya mashabiki wa Simba ilipotea tangu Oktoba 23 mwaka huu ilivyopata sare ya 1-1 na mtani wao wa jadi, Yanga na baada ya hapo ilipoteza mechi iliyofuata kwa 1-0 na Azam FC lakini mchezo uliofuata walifutwa machozi kwa kushinda 5-0 mbele ya Mtibwa. Licha ya ushindi huo mkubwa kwa msimu huu Simba ilioupata dhidi ya Mtibwa, mashabiki wa kikosi hicho cha Juma Mgunda walifurahi kwa muda tu kwani mechi iliyofuata waliambulia sare ya bao 1-1, dhidi ya Singida Big Stars, kisha kushinda 1-0 dhidi ya Ihefu na juzi kuichapa Namungo 1-0 matokeo ambayo ni mazuri kwa timu lakini yanawaumiza mashabiki.
Kinachowafanya mashabiki wa Simba kuumia zaidi ni namna timu yao inavyocheza. Simba haiko kwenye ubora wake hali isiyowapa matumaini mashabiki na wadau wake ya kufanya vizuri kwenye kuwania ubingwa wa ligi na kufika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika jambo lililojidhirisha kwenye mechi ya juzi kutokana na mashabiki kuzomea na kukebehi zaidi ubora wa timu yao zaidi ya kufurahia kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.


MCHEZO ULIVYOKUWA
Simba ilianza kwa kutafuta bao la mapema huku ikicheza kwa kasi kupitia kati na pembeni walipokuwa wakicheza mawinga Pape Sakho na Augustine Okrah lakini mpango huo ulifia kwenye miguu ya wachezaji wa Namungo.
Namungo ilichagua kuanza kwa kukaa nyuma ya mpira na kuwasubiri Simba ili iwakabe na kufanikiwa kwa dakika 30 za kwanza kabla ya makosa yaliyofanywa na kuwapa Simba nafasi moja ambayo waliitumia kuandika bao.
Baada ya Simba kuona ngome ya Namungo imekuwa ngumu kufunguka, ilianza kupiga mipira mirefu kutoka nyuma kwenda mbele pembeni na moja ya mpira huo ulifanikiwa baada ya beki wake Henoc Inonga kupiga pasi ya namna hiyo iliyomfikia beki wa kulia Mohammed Hussein aliyepanda kushambulia na kuingia nao ndani ya boksi kisha kumpa pasi Moses Phiri aliyekuwa karibu zaidi na goli na kuweka mpira nyavuni kiulaini.
Baada ya Simba kupata bao hilo, Namungo ilifunguka na kutaka kusawazisha lakini haikufanikiwa licha ya kufanya mabadiliko manne yaliyolenga kushambulia zaidi, nda. Katika dakika zote 90 walizocheza Namungo, ni nafasi mbili pekee zilikuwa za hatari kwa kipa wa Simba, Aishi Manula na zote zikitengenezwa na Lusajo lakini alishindwa kuzitumia vyema na mechi kumalizika kwa Wekundu wa Msimbazi kushinda 1-0.

SHIDA NI HAPA
Huenda mashabiki wa Simba wakawa sahihi kutofurahia ubora wa timu yao, lakini nyuma yake ni kikosi cha wachezaji waliopo ndani yake na kile wanachokifanya kwenye mechi.
Ubora wa mastaa wengi wa Simba hususan eneo la ushambuliaji ni wa kawaida na hawajawa na ari ya upambanaji wala kuonyesha njaa ya mabao mengi kama ilivyo kwa kinara wa kufunga kikosini hapo, Moses Phiri mwenye mabao sita hadi sasa.
Kukosekana kwa kiungo wake, Clatous Chama aliyefungiwa mechi tatu ni moja ya sababu za Simba kutocheza kama ilivyozoeleka kwa kutoa burudani na kutengeneza mabao kwani wachezaji wanaopata nafasi hawajafikia kile anachokifanya Chama.
Kocha Mgunda mara nyingi ameonekana kukwama kwenye kufanya mabadiliko ya wachezaji na hilo alilithibitisha juzi kwani licha ya Kibu Denis kushindwa kuonesha kiwango bora, hakumtoa na badala yake alitoka winga Okrah na kuingia kiungo Victor Akpan ambaye asili yake ni kiungo wa ulinzi.


PHIRI,  JANZA WALITISHA
Mshambuliaji  wa Simba Phiri ambaye ni mfungaji wa bao pekee kwenye mchezo, licha ya soka la timu yake kutoridhisha alionekana muda mwingi kufanya vizuri na kuisimbua sana ngome ya ulinzi ya Namungo.
Wengine wa Simba waliokuwa bora ni Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute.
Kocha mkuu wa Namungo, Honor Janza aliweza kucheza mechi na Simba namna alivyotaka na mpango wake ulitimia kwa kiasi kikubwa kwani mabadiliko aliyoyafanya yalimlipa licha ya kupoteza mechi.


WASIKIE WENYEWE
Kocha Mgunda wa Simba baada ya mechi alieleza kufurahishwa na ushindi na kusema anakwenda kuboresha na kurekebisha zaidi kikosi chake kwaajili ya mechi zijazo.
“Nafurahi tumepata ushindi, ndiyo matokeo tuliyoyahitaji. Tumeona mapungufu yetu na tunaenda kuyafanyia kazi lakini pia kuboresha yale mazuri,” alisema Mgunda.
Kocha msaidizi wa Namungo, Shadrack Nsajigwa pia alifurahishwa na kiwango cha timu yake na kuweka wazi sababu ya kupoteza.
“Tuliingia na mbinu ya kuwaacha Simba wacheze mpira sisi tukabe na kufanya mashambulizi ya kushitukiza naamini kwamba tulifanikiwa katika eneo moja na kufeli katika eneo lingine.
“Tulifanikiwa lakini kwa bahati mbaya tulifanya kosa moja ambalo walilitumia kutuadhibu na sisi tukashindwa kutumia vyema makosa yao,” alisema Nsajigwa.