Simba imekosea hapa tu ishu ya Pablo

Wednesday June 15 2022
Pablo PIC
By Mohammed Kuyunga

NIMEMSIKIA Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alipomzungumzia aliyekuwa kocha wa Simba, Pablo Franco baada ya mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Mei 28 pale CCM Kirumba, Mwanza.

Bila unafiki wa Simba na Yanga, Nabi alisema Simba ilipaswa kumvumilia kocha huyo raia wa Hispania. Kwanini? Kwanza ikiwa ni mara yake ya kwanza kufundisha soka Afrika, lakini ameweza kuifikisha timu yake kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.


USHINDANI MKALI

Kama haitoshi, Nabi alisema Pablo ametoa ushindani mkali kati ya timu hizo katika mechi walizocheza.

Nabi alisema baada ya mchezo wa nusu fainali ya ASFC dhidi ya Simba, alizungumza na Pablo na kumwambia amekabiliana na majeraha ya wachezaji muhimu katika mchezo huo.

Advertisement

Tukiachana na Nabi, ukiangalia kwa undani Simba ilikuwa na ubora mbele ya Yanga katika michezo miwili ya Ligi Kuu msimu ulioisha pamoja na michezo hiyo yote kuisha kwa sare tasa. Ilichokosa Simba ni wachezaji wa kumaliza mechi.

Lakini leo hii Pablo amefukuzwa kwa sababu ya kupoteza mchezo wa ASFC, ila sababu zinazotolewa hazina mashiko na sio za kitaalamu. Simba inadai imeachana na kocha huyo kwa sababu ya kupoteza Kombe la Ligi Kuu Bara na ASFC.

Pia, inadaiwa kuwa Pablo ameshindwa kuifikisha Simba katika hatua nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kitaalamu hizi haziwezi kuwa sababu za kumwondoa kocha huyo katika kibarua chake.

Ikumbukwe kocha huyo mwenye uraia wa Hispania hii ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kufundisha timu Afrika.


WACHEZAJI WAMWANGUSHA

Pamoja na kwamba hii sio sababu ya kumtetea kubaki Msimbazi lakini tangu mchezo wake wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting, hadi ule wa mwisho dhidi ya Yanga yote ya uwanjani CCM Kirumba, kocha huyo alionekana kuwa na kitu. Pablo ni kocha mwenye uwezo wa kuifanya timu iwe na kasi katika kushambulia.

Katika mchezo dhidi ya Yanga baada ya kufungwa bao la dakika 25 na Feissal Salum ‘Fei Toto’, kipindi cha pili Simba ilirudi na nguvu baada ya kuishambulia Yanga mfululizo.

Laiti kama Simba ingekuwa na washambuliaji wanaoijua kazi yao, bao lile lingeweza kurudi.

Ilimbidi Nabi kubadili mchezo na kuzuia zaidi huku akitegemea kufunga kwa mipira ya kushtukiza kwa Fiston Mayele na Elite Makombo.


HAKUSAJILI HATA MMOJA

Simba inamfukuza Pablo akiwa hajasajili hata mchezaji mmoja. Amekuta wachezaji waliosajiliwa na uongozi wa Simba.

Klabu hiyo imeacha kuangalia tatizo la msingi na kumtupia lawama Pablo. Simba imekuwa na washambuliaji watatu ambao ni Meddy Kagere, John Bocco na Chris Mugalu.

Hakuna asiyejua kuwa Bocco na Mugalu walikuwa nje kwa muda mrefu wakiwa na majeraha.

Hawa ndio walikuwa wafungaji bora wa timu wa msimu uliopita, Bocco akiwa na mabao 16 na Mugalu 15. Wanapokaa nje kwa muda mrefu unategemea watakupa nini katika ligi inayofuata?

Kagere naye amekuwa Simba katika kipindi chote cha miaka minne ya mafanikio ya Simba. Lakini mchezaji huyo na wengine waliokuwa na kikosi hicho kwa miaka minne ya ubingwa wamekumbwa na uchovu wa kuitumikia timu muda mrefu.

Pia, Kagere pia amekuwa sio chaguo la Pablo katika kikosi cha kwanza kutokana na staili ya uchezaji wake.


CHAMA NA MIQUISSONE

Raia huyu wa Rwanda sio mchezaji wa kuhangaika na kutafuta mipira kama ilivyo kwa Mugalu. Kwanza hana uwezo mkubwa wa kumiliki mipira. Unapomtaka Kagere ahangaike kufuata mipira pembeni na kuwasubiri wengine wapande, utamtesa bure. Huyu ni mchezaji wa kusisimama, kutafuta nasafi na kusubiri kutengenezewa mipira na viungo.

Lakini msimu wa 2020/21 ulipoanza, Kagere hakuwa na mchezaji wa kumtengenezea nafasi hizo, hasa baada ya Clatous Chama na Luis Miquissone kuuzwa. Wachezaji wapya wa mstari wa mbele, Kibu Denis, Pape Sakho na Duncun Nyoni hawakuweza kuirudisha timu katika ubora wake pamoja na kutajwa kuwa ni bora.

Kwanza, Sakho alisajiliwa kama namba 10 lakini Pablo hakumtumia kwenye nafasi hiyo kwa kuwa ni mfupi. Makocha wengi wa Ulaya huwa wanawaamini sana wachezaji warefu kucheza katikati.

Kibu hakuwa na ubora ule aliokuwa nao alipokuwa Mbeya City. Huu ni ugonjwa wa wachezaji wengi wa ‘Kitanzania’ huwa wanafanya vizuri wanapokuwa na timu ndogo lakini presha ya mashabiki wa Simba na Yanga huwa zinawatesa wanapohamia Kariakoo.

Viongozi wa Simba wanasema, wanaachana na Pablo na wanatafuta kocha mwenye uzoefu wa soka la Afrika. Hii ni propaganda tu. Pablo ni kocha mwenye uwezo wa kufundisha sio kama kocha wa Ulaya hawezi kufundisha Afrika. Hii ni sawa na kumpa jina baya mbwa ili upate nafasi ya kumuua.

Viongozi wa Simba walitakiwa kukaa chini na Pablo na kuanza kujenga upya kikosi kwa ajili ya msimu ujao kwa kuwa ameshapata uzoefu na anajua udhaifu wa timu aliyokuwa nao. Leo hii Yanga isingekuwa katika ubora huu kama ingemfukuza Kocha Nabi ilipofungwa na Simba kule Kigoma katika fainali ya ASFC. Viongozi hao walikiona kitu ambacho Simba hawakukiona kwa Pablo.


UBORA WA YANGA

Kingine ambacho kimeifanya Simba kufeli ni ubora wa kikosi cha Yanga. Timu hiyo yenye masikani yake Jangwani ilitengeneza timu na kuleta wachezaji walioizimua timu na kuifanya iwe na kasi katika idara zote.

Wachezaji kama Yanick Bangala, Khalid Aucho, Djuma Shaban, Fiston Mayale, Sadio Ntibanzikiza, Jesus Moloko na kipa Djigui Diarra waliweza kuunganisha nguvu na kuifanya Yanga kuwa bora.


Advertisement