SIKU 100 TAMU ZA GOMES SIMBA

Muktasari:

ITAKAPOFIKA Mei 4, rasmi kocha wa Simba, Mfaransa Didier Gomes atafikisha siku 100, tangu alipoanza kazi ya kuwafundisha mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara.

ITAKAPOFIKA Mei 4, rasmi kocha wa Simba, Mfaransa Didier Gomes atafikisha siku 100, tangu alipoanza kazi ya kuwafundisha mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara.

Gomes alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Mbelgiji Sven Vandenbroeck ambaye aliondoka bila kutarajiwa kutokana na mafanikio ambayo aliipa timu hiyo ikiwemo kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwanaspoti limefuatilia Gomes katika siku hizo 100, ambazo amekuwa hapa nchini kuna rekodi mbalimbali ambazo ameziweka katika ligi, Ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano mengine ya ndani.

Makala haya yanakuletea mafanikio mbalimbali ambayo Gomes ameyapata katika muda huo akiwa na kikosi cha Simba ambacho bado kina kiu ya kufanya vizuri zaidi.


UJIO WAKE SIMBA

Gomes alikuja nchini siku chache baada ya Sven kuachana na vigogo hao Januari 7, kisha kutimkia FAR Rabat ya Morocco, saa chache tu baada ya kuiongoza Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwafunga FC Platinum ya Zimbabwe.

Gomes ambaye ni raia wa Ufaransa akakabidhiwa mikoba ya kuwanoa wababe hao wa Msimbazi na kilichofuata ni historia na rekodi ‘baab-kubwa’ ndani na nje ya nchi akiwa na chama hilo ambalo linawatisha hata vigogo wa Afrika kwa sasa.


ALIPOANZIA

Kibarua cha kwanza kwa Gomes kilikuwa ni kuhakikisha anabeba ubingwa wa michuano mipya ya kirafiki ya Simba Super Cup iliyoandaliwa na klabu hiyo kwa lengo la kuweka utimamu kwa wachezaji wake kuelekea katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gomes alitwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kushinda mechi ya kwanza mabao 4-0, dhidi ya Al Hilal ya Sudan kisha mchezo wa mwisho akatoka suluhu na miamba ya soka la Afrika TP Mazembe ya DR Congo.


LIGI KUU NI MOTO

Gomes hadi sasa ameiongoza Simba kwenye mechi kumi za ligi hajapoteza hata mchezo mmoja, ameshinda nane na kutoka sare mbili ambazo zilikuwa dhidi ya Azam na Tanzania Prisons zote zilichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.


Matokeo

Dodoma 1 - 2 Simba

Simba 2 - 2 Azam

Biashara United 0 - 1 Simba

Simba 3 - 0 JKT Tanzania

Simba 1 - 1 Tanzania Prisons

Simba 5 - 0 Mtibwa Sugar

Mwadui 0 - 1 Simba

Kagera Sugar 0 - 2 Simba

Gwambina 0 - 1 Simba

Simba 3 - 1 Dodoma Jiji


REKODI KIMATAIFA

Gomes ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuiongoza timu kutoka Tazania kupata ushindi mbele ya AS Vita ikiwa kwenye ardhi yao nchini DR Congo baada ya kuwafunga bao 1-0 lililofungwa na Chris Mugalu.

Mfaransa huyo aliweka rekodi nyingine akiwa na Simba alimaliza nafasi ya kwanza katika kundi ‘A’ mbele ya vigogo wa soka la Afrika, Al Ahly waliokuwa nafasi ya pili, AS Vita ya tatu wakati Al Merrikh wakiburuza mkia.

Katika michezo sita ya hatua hiyo Gomes alishinda minne akiwachapa AS Vita mara mbili 1-0, ugenini na 4-1 kwa Mkapa, akawatandika mabingwa mara tisa wa Afrika, Ahly 1-0 nyumbani na kuwachakaza Merrikh 3-0 nyumbani huku akitoa suluhu (0-0) na Merrikh ugenini na kufungwa 1-0 ugenini Misri dhidi ya Ahly.

Kutokana na matokeo hayo wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, walimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi A wakiwa na pointi 13.

KILA KOMBE ANALITAKA

Simba wapo katika mashindano matatu mpaka sasa ligi, Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho ambalo (Jumamosi), walicheza mechi ya hatua ya 16, bora dhidi ya Kagera Sugar.

Kwenye Ligi Kuu Bara, Simba ndio wanaongoza wakiwa na pointi 61, katika Ligi ya Mabingwa Afrika wapo robo fainali na kwenye Kombe la Shirikisho (ASFC), wapo katika hatua ya 16 bora.


MASHINE YA MABAO

Rekodi zinaonyesha Simba chini ya Gomes katika ligi wamecheza mechi kumi, wamefunga mabao 17 na wao kuruhusu matano.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ya makundi Simba wamefunga mabao tisa na kufungwa moja huku, mshambuliaji, Luis Miquissone akiibuka kuwa kinara wa ufungaji katika hatua hiyo akifunga mabao matatu.

Kwenye Kombe la Shirikisho (ASFC), Gomes ameingoza timu hiyo katika mechi moja dhidi ya African Lyon ambayo walishinda mabao 3-0, ambayo yalifungwa na Ibrahim Ajibu mawili pamoja na Parfect Chikwende.

Wakati huo huo, leo Gomes atakuwa na mtihani mwingine katika Kombe la ASFC, kwenye hatua ya 16 bora kucheza dhidi ya Kagera Sugar.

MSIKIE MWENYEWE

Gomes anasema mafanikio hayo aliyoyapata ndani ya Simba kwa kipindi ni kutokana na ushirikiano ambayo unaonyeshwa na wachezaji katika kutimiza majukumu yao katika kila mechi.

Anasema mara nyingi anawafuatilia wapinzani vile ambavyo wanacheza na kufahamu ubora na udhaifu wao kisha huenda kwa wachezaji kuwachorea ramani kamili ya vile ambavyo wanatakiwa kufanya.

“Jambo ninalojivunia ni kukutana na wachezaji wenye uelewa hapa Simba. Kama binadamu kuna makosa ambayo huyafanya lakini kwa kiasi kikubwa hufanya vizuri ndio maana mpaka wakati huu nimepata mafanikio hayo na nina imani nitakuwa na mafanikio mengine zaidi,” anasema Gomes na kuongezea;

“Najisikia vizuri kuwa Simba, ni timu iliyokamilika kuanzia uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na hata mashabiki jambo ambalo ni gumu kulipata kwenye timu nyingi za ukanda huu wa Afrika.

“Siri kubwa ya mafanikio haya ni umoja, ubora na kujitoa kwaajili ya timu, kila mtu wa Simba anatimiza majukumu yake kwa mapenzi makubwa ya klabu ndiyo maana tunafanikiwa na naamini tutaendelea kufanikiwa zaidi ya hapa.”