Sanogo kutoka Arsenal hadi uvumi wa Zamalek

UNAKUWA mbabe kadri unavyoweza. Mwishowe unanyoosha mikono juu. Inakadiriwa kwa jumla mpaka alipokuwa akimaliza ngumi mbabe Muhammad Ali alikuwa amepigwa ngumi zaidi ya 200,000.

Haishangazi kuona aliondoka katika mchezo huo akiwa na ugonjwa wa Kiharusi. Sawa, alikuwa chuma, mbabe, nyuki, kipepeo. Mwishowe alipokea ngumi zaidi ya 200,000 katika mwili wake. Wababe ukafika mwisho.

Pambano lake la mwisho alipigana katika visiwa vya Bahamas mwaka 1981 na bondia mchovu aliyeitwa, Trevor Berbick na bado Ali alidundwa raundi ya 10. Huo ulikuwa mwisho wake. Alinyoosha mikono.

Nilikumbuka niliposoma mahala kuwa wakala wa mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Yaya Sanogo alikuwa ameipa ofa klabu ya Zamalek kumnasa mshambuliaji huyo.

Nimwite staa? Hapana. Wakati mwingine tunalitumia vibaya hili neno staa.

Nakukumbusha Sanogo ana miaka 27 tu. Hajadanganya miaka kwa sababu alizaliwa nje kidogo ya Jiji la Paris eneo la Massy Januari kama hii mwaka 1993. Bado ni kijana mdogo. Anakujaje Zamalek akiwa na miaka 27?

Kuna mastaa wachache wakubwa waliotamba Ulaya waliwahi kuja kucheza Afrika. Wengi ni Waafrika wenyewe lakini kama kuna mfano wa staa wa nje basi ni Rivaldo. Lakini huyu alikwenda Angola akiwa na umri wa zaidi miaka 37. Si umri wa miaka 27 wa Sanogo.

Hawa kina Sanogo ndio miongoni mwa vijana wa mtu anayeitwa, Arsene Wenger aliowapeleka Arsenal akijaribu kufanya maajabu ambayo aliwahi kuyafanya awali.

Wakati dunia ikiwa inabadilika Arsene Wenger aliendelea kubakia yule yule tu huku akipokea ngumi nyingi kama Muhammad Ali licha ya ukweli kuna wakati alikuwa mbabe.

Wenger aliamini Sanogo angekuwa Thierry Henry mwingine. Wakati ule Henry alikuwa akisuasua pale Juventus lakini Wenger alifanikiwa kumbadili na kumfanya awe staa mkubwa duniani.

Wenger pia aliwahi kufanya maajabu hayo kwa Patrick Vieira. Alikuwa anasuasua AC Milan akisugua benchi akiwa kijana mdogo, lakini Wenger akambadili kuwa staa mkubwa duniani.

Wenger pia aliwahi kumgeuza Cesc Fabregas kuwa staa mkubwa duniani baada ya kuwa kinda pale Barcelona. Wenger alichukia matumizi makubwa ya pesa. Kwa sababu aliwahi kufanya maajabu haya, basi aliamini angefanya tena hata wakati huo dunia ikiwa inazama katika matumizi makubwa ya pesa katika soka.

Kitu ambacho kiliashiria mwisho wa Wenger katika soka ni namna ambavyo baadaye katika maisha yake ya Arsenal alikuwa analamba magalasa mengi kuliko zamani. Kila nafasi alikuwa anajaribu kumleta mrithi Kinda ambaye amemtoa daraja la pili Ufaransa, Uswisi au kwingineko. Hata hivyo waliishia kuwa magalasa.

Alienda Uswisi akawachukua Philippe Sendoros na Johan Djourou kwa ajili ya kuchukua nafasi za kina Martin Keown na Sol Campbell. Wote tulishuhudia jinsi walivyoangukia kuwa magalasa ambao hawakustahili kuchezea timu kama Arsenal.

Kina Kieran Gibbs wakapelekwa kwenda kuchukua nafasi za akina Ashley Cole. Huyu Sanogo ndio alikuwa ameandaliwa kuwa Thierry Henry mpya.

Alikuwa amechukuliwa katika klabu ya Auxerre iliyokuwa Daraja la Kwanza Ufaransa. Eti awe Henry mpya. Huo ulikuwa ni mwaka 2013.

Kumbuka mwaka huo Manchester City walikuwa na mtu kama Sergio Aguero. Liverpool walikuwa na mtu kama Luis Suarez. Chelsea walikuwa na mtu kama Diego Costa.

Wenger alikuwa anajaribu kufanya maajabu kwa kumchukua Yaya Sanogo kutoka klabu ya madaraja ya chini Ufaransa.

Leo ukisikia wakala wa Sanogo anaipa klabu kama Zamalek kumchukua ujue sio kwa bahati mbaya kwamba mchezaji huyu amefikia hadhi hiyo.

Hakuwa na hadhi ya Arsenal achilia mbali timu nyingine za juu. Kwa mfano. Baada ya hapo alienda Charlton Athletic na kisha akaenda kwao Ufaransa kucheza Toulouse.

Mkataba wake umefikia ukingoni Januari hii na sasa wakala wake anataka kumtupa Afrika. Wakati huo huo mshambuliaji namba moja wa Zamalek, Mostafa Mohmmed anatakiwa na klabu ya St Ettiene ya Ufaransa. Ina maana Mostafa anayecheza Afrika ni bora kuliko Sanogo. Ina maana Mostafa ni bora kuliko Sanogo hata kama bado yuko Afrika. kwa nini St Etienne wasiende kwa Sanogo?

Kila mara nilikuwa nasisitiza anguko la Wenger lakini wakati mwingine inakuwa ngumu kueleweka. Siku za mwisho za maisha ya Wenger Arsenal alijikuta akikabiliwa na maanguko mawili makubwa. Kwanza ni anguko la namna ya kunasa mastaa wapya, pili ni mbinu zake za uwanjani.

Kitu kigumu zaidi kwake ni namna ambavyo dunia ilikuwa imeingiliwa na mambo mawili. Kwanza ni pesa zilizoingia katika soka kuanzia ujio wa Roman Abramovich, kisha Waarabu wa Man City na Warusi. Pia kulikuwa na ujio wa makocha ambao waliweza kutuonyesha mbinu mpya zaidi uwanjani. Hawa ndio kina Pep Guardiola.

Wenger hakutaka kubadilika. Aliendelea kujaribu kufanya maajabu kwa akina Sanogo lakini uwanjani pia Arsenal ilikuwa ni ile ile ambayo ilikuwa inapiga pasi nyingi uwanjani huku ikiwa haina ubunifu katika ukabaji.

Sanogo ni alama ya siku za mwisho za Wenger. Sanogo ni alama ya ngumi ambazo Wenger alipigwa katika maisha yake ya soka kama vile ambavyo Muhammad Ali licha ya ubabe wake alikuwa anapigwa.

Rafiki yake Sir Alex Ferguson hakuwahi kujaribu maajabu haya. Sawa, kuna wakati alikuwa ana wachezaji wa kawaida lakini hakuwahi kufanya mzaha katika kupandikiza mchezaji mahiri katika nafasi ambayo mchezaji mahiri ameondoka au umri umemtupa mkono.

Sir Alex alijua namna ya kutumia pesa. Hakuwa na muda sana wa kusubiri maajabu. Maajabu yake makubwa yalikuwa kukipandisha kikosi cha vijana cha Manchester United kilichotwaa ubingwa wa FA mwaka 1992. Ndio hawa akina David Beckham, Paul Scholes, Phil Neville, Gary Neville na Nicky Butt.


Imeandikwa na Eddo Kumwembe