SABABU ZA ERIKSEN KUZIMIA UWANJANI

Muktasari:

KIUNGO wa kimataifa wa Denmark, Christian Eriksen aliushtua ulimwengu wa soka, baada ya kuanguka ghafla dakika 43 akiwa uwanjani na kuleta simanzi, ikidhaniwa labda kapoteza maisha.

KIUNGO wa kimataifa wa Denmark, Christian Eriksen aliushtua ulimwengu wa soka, baada ya kuanguka ghafla dakika 43 akiwa uwanjani na kuleta simanzi, ikidhaniwa labda kapoteza maisha.

Nyota huyo anayekipiga Inter Milan alikumbwa na tukio hilo kwenye mchezo wao wa fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2020 dhidi ya Finland uliochezwa Jumamosi usiku.

Kiungo huyo alionekana akienda kupokea mpira wa kurushwa kutokea kwenye wingi ya kushoto, lakini hakuweza, alianguka chini na kulalia upande wa kulia.

Tukio hilo lilisababisha jopo la madaktari pamoja na watu wa huduma ya kwanza uwanjani hapo kuingia kumpa huduma ya dharura ikiwamo ile muhimu ya uokozi wa maisha.

Utomasaji wa moyo ni moja ya huduma muhimu sana kwa ajili ya ufufuaji wa moyo na upumuaji pale mwanadamu anapopata tishio la mshtuko wa moyo au moyo kusimama ghafla.

Huduma hii hujulikana kama Cardiopulmonary Resuscitation (CPR) ambapo mifumo nyeti ya mwili ambayo ni mzunguko wa damu na moyo na upumuaji hupata usaidizi kutoka kwa wataalam wa afya na vifaa tiba ikiwamo mashine ya umeme ya kuustua moyo.

Huduma hii ya dharura ndiyo iliyochangia kumwokoa kiungo huyu aloyewahi kutesa akiwa na klabu ya Tottenham ya Ligi Kuu ya England na kumfanya kurudiwa na fahamu hapo baadaye.

Ingawa hadi anatolewa aliendelea kupata upumuaji kwa usaidizi wa mashine, taarifa za baadaye zilieleza aliweza kuongea na kocha wake akiwa anapelekwa katika huduma za juu za matibabu.

Mechi hiyo ilisimama kwa saa 1 na dakika 45 ili kupisha jopo la madaktari na watoa huduma ya kwanza kumhudumia kiungo huyo.

Baadaye mechi hiyo iliendelea na Denmark walipoteza kwa bao 1-0, kocha wa nchi hiyo Kasper Hjulmand alieleza kuwa matokeo hayo hayana umuhimu kama ilivyo uhai wa Eriksen.


MAMBO YANAYOSABABISHA WATU KUZIMIA

Kuzimia ni hali ya mwili kuzima mawasiliano ya nje ghafla kwa muda mfupi hatimaye mwili huendelea kuwajibika na mawasiliano ya ndani ya mwili tu ili kusahihisha dosari inayoweza kutishia uhai.

Lakini wengi wanauliza kulikoni hali ile imempata mchezaji wa kulipwa ambaye suala la utimamu wa afya yake ni jambo muhimu sana.

Ieleweke kuwa unaweza kuwa timamu kiafya mara baada ya kupima lakini kumbe hapo baadaye matatizo ya kiafya huweza kuibuka ghafla wakati unafanya majukumu mbalimbali ikiwamo kucheza.

Mara nyingi sababu kubwa inayoweza kuchangia wanadamu kuzimia ni ubongo kukosa hewa ya oksijeni kunakoweza kuchangiwa na matatizo ya mapafu, moyo na mishipa ya damu na pia kuvuta hewa yenye sumu ya carbon monoxide.

Kwa upande wa matatizo ya moyo yanayoweza kusababisha mtu kuanguka ghafla na kuzimia ni pamoja na moyo kusimama ghafla au shambulizi la moyo au matatizo ya mishipa ya damu.

Kuzimia ni moja ya njia za kujihami kwa mwili kutoa nafasi rasilimali zake ambazo ni damu na oksijeni kutumika katika maeneo nyeti ya mwili na kunyima zile sehemu ambazo hazina umuhimu kwa uhai wa mwili.

Maeneo nyeti ya mwili kwa ajili ya uhai wa mwili ni pamoja na ubongo, moyo, mapafu, ini na figo.

Dalili ambazo mara kwa mara ni ishara ya kuzimia ni pamoja na hisia za uzito miguuni, kukosa nguvu, kuona giza, kizunguzungu, kupata hali ya kichefu chefu, kupiga miayo mara nyingi bila sababu, kuweweseka au kuchanganyikiwa na kuhisi joto au moto.

Yapo mambo mengine yanayoweza kusababisha mwanadamu kuzimia ni pamoja na mwili kupata mstuko, sukari ya mwili kushuka au kupanda sana, upungufu mkali wa maji mwilini, kunywa sumu au usumu wa vimelea, upungufu wa damu, vichochezi na dawa za matibabu.


KUZIMIA KUNAZUILIKA?

Hakuna njia ya moja kwa moja inayoweza kuzuia mwanadamu kuzimia ingawa pale unapopata dalili za kuzimia ni vyema kujisogeza eneo ambalo litakuwa salama endapo utazimia na kuanguka.

Kwa mtu aliyezimia atahitaji kutathiminiwa kama anapumua au hapumui.

Eriksen alifanyiwa huduma ya CPR mara baada ya kuonyesha kuwa hapumui vyema na mapigo ya moyo yalikuwa chini.

Inashauriwa kama upo jirani na mtu aliyezimia na atakuwa anapumua ni vyema haraka mlaze mahala salama, nyanyua miguu yake na uitikise tikise ili damu nyingi iende maeneo nyeti, mfungue mkanda au legeza mavazi aliyovaa na ondoa vizuizi vya mavazi na kisha mlaze ulalo wa uponaj.

Kama atakua anapumua vizuri basi msikilizie kwa dakika moja na ita msaada wa watoa huduma au mkimbize katika huduma za afya.

Ikiwa atakua hapumui, haraka tathmini upumuaji wake na tazama njia ya hewa kama ina mkwamo au kizuizi. Kama atakuwa hapumui na hakuna mapigo ya moyo anza huduma ya ufufuaji wa moyo na upumuaji yaani CPR. Endelea kufanya CPR mpaka pale msaada utakapokuja.

Umuhimu wa CPR ndiyo unafanya elimu yake kutolewa tangu elimu ya msingi kwa lengo la kuikuza jamii iwe na ufahamu wa huduma hii inayoweza kuokoa maisha ya mgonjwa.

Huduma hii ndiyo iliyofufua moyo na upumuaji CPR ndiyo imetajwa kuwa mwokozi wa maisha ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29.