Rekodi Simba zaitikisa Kaizer

Monday May 03 2021
ROBO FULL SIMBA
By Charles Abel

HISTORIA ya Simba dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika zinaipa jeuri na kuiweka katika hali nzuri kisaikolojia kupata matokeo mazuri katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika.

Katika droo ya robo fainali ya mashindano hayo iliyochezeshwa juzi jijini Cairo - Misri, Simba walioongoza kundi A walipangwa kukutana na Kaizer Chiefs walioshika nafasi ya pili katika kundi C, ambapo mechi ya kwanza itachezwa nchini Afrika Kusini kati ya Mei 14 na 15 na kisha timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam kati ya Mei 21 na 22.

robo kaiza

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Simba wamekuwa hawapati wakati mgumu pindi wanapokutana na timu za Kusini mwa Afrika katika hatua za mtoano za mashindano ya klabu barani Afrika na mara nyingi imekuwa ikipenya kwenda hatua inayofuata, huku mara chache tu ndio ikishindwa kufanya hivyo.

Katika mashindano tofauti ya klabu Afrika, Simba imekutana na klabu zinazotoka katika nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (Cosafa) mara 26 na kati ya hizo imefuzu mara 19 huku ikikwama mara saba tu.

Jumla ya mechi za mashindano ya klabu Afrika ambazo imecheza dhidi ya klabu kutoka nchi wanachama wa Cosafa ni 50 ambapo kati ya hizo, imeibuka na ushindi mara 26, kutoka sare 11 na kupoteza mechi 13, ikifunga jumla ya mabao 77 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50.

Advertisement

Katika mechi hizo 50 ilizokutana na timu kutoka nchi wanachama wa Cosafa, michezo 25 walicheza ugenini ambapo wameibuka na ushindi mara nane, kutoka sare nane na wamepoteza jumla ya mechi tisa wakati katika mechi 25 walizocheza uwanja wa nyumbani wameibuka na ushindi mara 18, kutoka sare tatu na kupoteza mechi nne tu.

Simba imekutana na timu kutoka Afrika Kusini mara moja ambapo ilikuwa ni mwaka 2003 katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika walipocheza na Santos ya huko na kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 8-9 baada ya mechi mbili baina yao zilizomalizika kwa sare tasa.

Ti-mu za Zambia ndizo zinaonekana kuisumbua zaidi Simba na sio nchi nyingine wanachama wa ukanda huo kwani katika mara saba ambazo Simba ilitupwa nje na timu kutoka ukanda huo, mara nne ilitolewa na timu kutoka nchi hiyo ambazo ni Nkana, Zanaco na Green Buffaloes huku ikitolewa na timu kutoka Msumbiji mara mbili na mara moja dhidi ya timu kutoka Angola.

Mara ya kwanza kwa Simba kupangwa na timu kutoka Kusini mwa Afrika ilikuwa ni 1974 walipokutanishwa na Linare ya Lesotho katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na wakaibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-2, wakishinda mabao 3-1 ugenini na mechi ya marudiano Dar es Salaam wakaibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mwaka huohuo wakakutana na Green Buffaloes ya Zambia katika hatua ya pili ya mashindano hayo na kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 3-1, wakishinda mabao 2-1 ugenini na walipokuja kucheza marudiano hapa nchini wakaibuka na ushindi wa bao 1-0.

Simba sio tu imekuwa na uwezo wa kupata ushindi ugenini dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika, bali mara kadhaa imekuwa ikipata ushindi wa idadi kubwa ya mabao ambayo huyaweka katika nafasi nzuri kufuzu.


Mwaka 1979 iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini dhidi ya Mufulila Wanderers ya Zambia, licha ya kufungwa mabao 4-0 nyumbani lakini msimu wa 2018/2019 iliichapa Mbabane Swallows ya Eswatini kwa mabao 4-0 ugenini.

Iliwahi kuichapa Lengthens ya Zimbabwe kwa mabao 3-0 ugenini mwaka 2010 na mwaka 2003 iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Botswana Defence Force XI ya Botswana

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema pamoja na ugumu wa Kaizer Chiefs anaamini timu yake itafika mbali katika mashindano hayo msimu huu

“Tunataka kufika mbali kwenye haya mashindano na tupo tayari kucheza vizuri dhidi ya Kaizer Chiefs kwenye mechi zote.

Haitakuwa rahisi lakini nina uhakika huu msimu Simba inaweza kwenda mbali zaidi,” alisema Gomes.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji alisema kuwa ana imani timu yake itapenya mbele ya Kaizer Chiefs.

“Hongera Simba kwa kupangwa kucheza na Kaizer Chiefs kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Nina imani kubwa kwamba tutafanya vizuri kwenye mechi hii,” alisema Dewji.

Advertisement