Rais Samia, Dk Mwigulu wameupiga mwingi kazi kwako Chongolo

Muktasari:

Yapo matukio ambayo yamenishtua michezoni nyakati hizi ambayo yameniacha na furaha na wakati mwingine kunikera inawezekana nimechukizwa na sarakasi za uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinazoendelea.

Yapo matukio ambayo yamenishtua michezoni nyakati hizi ambayo yameniacha na furaha na wakati mwingine kunikera inawezekana nimechukizwa na sarakasi za uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinazoendelea.

Inawezekana yakawa ni matukio yaliyonifurahisha ya Simba kuendeleza ubabe wake nyumbani msimu huu wakampiga yeyote aliyekuja mbele yao na wakauheshimisha uwanja wao wa nyumbani na kwamba hatoki mtu salama.

Hayo ni baadhi tu lakini yote kwa yote hakuna ambalo linaweza kuzidi hili la Rais Samia Suluhu Hassan ambayo kwangu mimi imekuja katika nyakati ambazo ni kama nimelala na kuota ndoto ambayo baadaye inakuja kuwa kweli.

Kauli ya Rais Samia kuhusu kukigeukia Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimsingi ndio chama tawala kuhusu viwanja vyake vya michezo inavyomiliki ibaki kuwa kauli ya kishujaa katika michezo kuliko nyingine zozote ambazo nimezisikia hivi karibuni.

Rais Samia ameigeukia CCM akiwataka sasa kuanza kuviangalia viwanja wanavyomiliki na kuvikarabati na kuwa katika sura ya ubora wa matumizi ya watu wa michezo, kauli ambayo ameitoa pale Jijini Mwanza alipokutana na vijana wa Tanzania katika ziara yake ya siku tatu jijini humo.

Hakuna kiongozi wa nyuma yake aliwahi kuigeukia CCM kwa sura ya namna hii ikichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha michezo nchini kwa ubovu wa viwanja mbalimbali ambavyo viko katika miliki yake vikihudumu michezo mbalimbali kwa hali ya uchovu.

Haya yanatokea katika nyakati ambazo viwanja hivi vimekuwa vikiingiza fedha nyingi katika matamasha na hata mechi mbalimbali za soka lakini maingizo hayo yamekuwa hayaendani na uwekezaji wa kuhudumia viwanja hivyo.

Hata wakubwa wa chama walipowahi kuulizwa huko nyuma wamekuwa na majibu ya kisiasa zaidi kwamba lini wanafikiria kuvikumbuka viwanja hivyo na kuvikarabati na inaonekana walikuwa wanahofia kauli ya watu wa juu yao hasa mwenyekiti wa chama ana dira gani.

Kauli ya Rais Samia imekuja kama pale mgonjwa wa maradhi sugu yaliyokosa tiba anaposikia kwamba sasa dawa ya maradhi yake imepatikana anaweza kujikuta anapona ghafla kwa furaha hiyo akisikia kilio chake sasa hatimaye kimesikika.

Uamuzi huu wa Rais Samia umekuja wakati muafaka hasa zikiwa zimepita siku chache tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba naye awasilishe bajeti kuu ya nchi akicheza vyema karata yake kwa kuondoa kodi katika uingizaji wa nyasi za viwanjani.

Uamuzi katika haya mawili una afya kubwa katika michezo kwani sasa ukiongeza na uamuzi wa kurudisha michezo shuleni kutakuwa na uhakika wa kuzalisha vipaji sahihi kutoka katika mazingira yenye afya bora.

Unawezaje kuzalisha wachezaji bora katika miundombinu mibovu? Ni Lazima uwe na mazingira sahihi yatakayosaidia yule anayefundisha na mfundishwaji kufanya kitu katika ubora mkubwa ambao unatarajiwa.

Uhakika ni kwamba uamuzi wa haya sasa unaashiria kwamba serikali ya Awamu ya Sita imeamua kwa dhati kugeukia michezo na kuhakikisha wanaweka nguvu ambayo itakuwa ni suluhisho la kuonyesha kuna hatua inapigwa.

Uamuzi wa haya sasa uwe kama chachu ya kuhakikisha kwamba hata klabu mbalimbali sasa zinaamka na kuwa na viwanja vyao katika ile sera ya kila timu kuwa na leseni yake kama maagizo ya vyombo vya juu ya TFF inavyoagiza.

Hakuna tena sababu ya klabu kusota kuwa na uwanja wake wakati suala lililopo ni kuamua kujenga uwanja na kuagiza nyasi tu bila kuwa na kodi na kuondoa msoto kama ule wa klabu ya Simba jinsi nyasi zake zilivyokwama pale bandarini Dar es Salaam.

Endapo kila klabu na hata taasisi binafsi zitachangamkia hili kuna uwezekano mkubwa baada ya miaka michache tutakuwa na matunda makubwa katika michezo kupitia uzalishaji wa mastaa wengi watakaotokana na sera hizi ambazo nimeanza kuziona katika serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia na serikali yake.

Hizi sio nyakati tena za kuona watu wanarudishana nyuma na kushindwa kutumia fursa hii adhimu ambayo itakuja kuwa muarobaini wa kututoa hapa tulipokwama kwa muda mrefu tukishindwa kuwa na mfumo mzuri wa kuzalisha wanamichezo.

Imani yangu kwamba sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu, Daniel Chongolo sasa wataamka na kutengeneza utaratibu wa haraka katika kuvifufua viwanja hivi, niseme tu Rais Samia kwangu ni mchezaji bora wa muda wote na Mwigulu ni nahodha wangu wa muda wote hawana baya.