Prince Dube duh!

Prince Dube duh!

Muktasari:

KAIMU Kocha Mkuu wa Azam FC, Vivier Bahati amewaambia mashabiki wao watulie kwani straika wao Prince Dube anakamiwa sana na mabeki, lakini msemaji wa timu akagusia kitu kuhusu afya yake.

KAIMU Kocha Mkuu wa Azam FC, Vivier Bahati amewaambia mashabiki wao watulie kwani straika wao Prince Dube anakamiwa sana na mabeki, lakini msemaji wa timu akagusia kitu kuhusu afya yake.

Thabit Zakaria alisema: “Baada ya kufika Afrika Kusini na kufanyiwa vipimo ndipo tutajua atakaa nje ya uwanja kwa muda gani ingawa tatizo kama lake huwa linaweza kumuweka nje si chini ya wiki sita.”

Dube ambaye anatibia mfupa wa mbele wa mkono wa kushoto unaoitwa Ulnar hajafunga katika mechi sita zilizopita jambo lililosababisha mashabiki kuanza kumnyooshea kidole na kuona ilikuwa nguvu ya soda.

Mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe alianza ligi kwa kasi akifunga mabao sita katika mechi nne dhidi ya Coastal Union aliyofunga mabao mawili sawa na alivyofunga katika mechi dhidi ya Kagera Sugar, huku akifunga bao moja katika mechi dhidi ya Prisons na Mwadui.

Pia, alitoa pasi nne za mabao katika mechi ambazo alifunga na ambazo hakufunga, jambo lililosababisha aongoze msimamo wa wafungaji bora tangu kuanza kwa ligi kabla ya kushushwa wiki iliyopita na John Bocco mwenye mabao saba.

Kasi yake uwanjani, chenga na jinsi anavyojua kukaa katika nafasi sahihi anapolikaribia goli ndivyo vitu ambavyo viliwavutia mashabiki wengi na kuanza kumfuatilia, lakini ghafla upepo umekata.

Tangu alipotoa pasi safi ya bao lililofungwa na Ayoub Lyanga, Oktoba 20 kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Ihefu, Dube hajafunga tena wala kutoka pasi katika mechi tano zilizofuata dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam ilipochapwa bao 1-0, ilipotoka sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania, iliposhinda mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji na ilipochapwa bao 1-0 na KMC na Yanga.

Hali hiyo ya ukame wa mabao ilisababisha kupitwa na mshambuliaji wa Simba, Bocco ambaye kwa sasa ana mabao saba na anaongoza chati ya ufungaji bora huku pia akifikiwa na kinda wa Gwambina, Meshack Abraham mwenye mabao sita.

Kocha Bahati alisema si kwamba Dube amefulia ila anapambana sana, lakini bahati ya kufunga haipo upande wake kwa siku za karibuni hivyo watu wasubiri kuona akirejea kwa nguvu kubwa atakapopona majeraha yake.

“Bado ni mshambuliaji mzuri na tegemeo katika kikosi chetu, lakini nafikiri ni upepo tu mbaya umemkumba na hajafunga mechi tano zilizopita ila naamini bado ana uwezo wa kuonyesha maajabu na akafunga mabao mengi msimu huu.

“Katika mechi hizo tano zilizopita amekuwa akipambana sana kutafuta mabao, lakini inashindikana kwani licha ya kwamba baadhi ya mechi tulipoteza ikiwemo dhidi ya KMC alipambana na kupata nafasi kama mbili nzuri lakini hakufanikiwa kufunga.

Lakini pia kwa sababu ni mshambuliaji mzuri na alionyesha makali mechi za mwanzo mabeki wa timu pinzani wanakuwa wanamuangalia zaidi na kumkamia,” alisema Bahati.

Dube yupo Afrika Kusini akitibiwa katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town chini ya daktari bingwa wa mifupa, Robert Nicolas.

Mchezaji huyo alilazimika kutolewa uwanjani dakika ya 17 katika mchezo dhidi ya Yanga uliofanyika Novemba 25 baada ya kuumia kwa kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wa kushoto unaoitwa Ulnar (huu ni mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho) kutokana na kutua vibaya wakati wakiruka juu kuwania mpira na beki Bakari Mwamnyeto.

...............

Na OLIVER ALBERT