Pablo akiweza hapa tu ametoboa

Pablo akiweza hapa tu ametoboa

HIVI karibuni uongozi wa Simba umemwajiri Mhispania Pablo Franco aliyepewa mkataba wa miaka miwili ambayo ndani yake una vipengele mbalimbali vya kuhakikisha kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kinafanikiwa.

Simba katika kipindi cha miaka minne iliyopita walikuwa kwenye kilele cha mafanikio ya mashindano ya ndani na nje ya nchi kutokana na ubora waliokuwa nao.

Katika kipindi hicho chote mbali ya mafanikio hayo wameachana na makocha wanne kwasababu mbalimbali ambao ni Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck na Didier Gomes.

Pablo anatakiwa kuhakikisha anakirudisha kikosi kwenye ubora na kufikia mafanikio. Makala hii inakuletea mambo matano ambayo Mhispania huyo akitoboa atafanya vizuri na kudumu ndani ya timu hiyo, akishindwa naye safari itamkumba kama waliomtangulia.


NIDHAMU

Kati ya maeneo anayotakiwa kuanza kuyafanyia kazi ni kusimamia nidhamu kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji bila ya kuangalia ukubwa wa jina la mtu.

Ikumbukwe kati ya sababu zilizomuondoa Aussems ni kushindwa kusimamia nidhamu kwa baadhi ya wachezaji hasa wale walioonekana kuwa na mikasa mingi ya utovu wa nidhamu.

Sven alifanikiwa na kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika huku kati ya silaha zake ni ukali aliokuwa nao katika kusimamia na kuongoza nidhamu.

Katika kuhakikisha nidhamu inakuwapo ndani ya Simba kuna wakati staa, Ibrahim Ajibu alichelewa kufika kambini alimrudisha nyumbani huku pia akimtoza faini ya Sh200,000.

Kutokana na mifano ya namna hiyo, Pablo ili afanikiwe anatakiwa kuwa mkali na mstari wa mbele kuongoza nidhamu kwa kila mchezaji, benchi la ufundi na wengineo wanatakiwa kuifuata.


PIRA BIRIANI

Msimu huu timu hiyo imewapoteza wachezaji wake wawili muhimu waliokuwa kikosi cha kwanza, Clatous Chama aliyeuzwa kwa RS Berkane ya Morocco na Luis Miquissone aliyekwenda Al Ahly ya Misri.

Baada ya kuuzwa wachezaji hao na kusajiliwa wengine wapya 12, kikosi hicho kimeshindwa kucheza vizuri pengine kama ambavyo kilikuwa misimu minne nyuma waliyochukua ubingwa wa ligi mfululizo.

Simba hawachezi soka la kuvutia, kumiliki mpira muda mrefu, kupiga pasi za chini na wakati huu wanacheza zaidi mipira mirefu ya juu jambo ambalo linawawia ugumu kucheza kama walivyozoeleka.

Mbali na kuonekana kuwa imara safu ya ulinzi hadi sasa kucheza mechi tano bila kuruhusu bao lakini Pablo anatakiwa kuiboresha safu ya ushambuliaji irudi kwenye makali yake sababu kufikia sasa mechi tano za ligi imefunga mabao matatu tu na pia arudishe ubora na aina ya uchezaji wa soka la kuvutia, upambanaji na utawala wa mechi kama mashabiki walivyoizoea Simba yao ikipiga ‘pira biriani’.


DIRISHA DOGO

Dirisha kubwa la usajili msimu huu wameongeza wachezaji wapya 12, ambao pengine hawakutegewa na wengi kufikia idadi hiyo kutokana na ubora waliouonyesha msimu uliopita.

Katika orodha ya wachezaji hao wengi wao wameshindwa kuonyesha makali tofauti na Inonga Baka, ambaye amekuwa nguzo imara ya safu ya ulinzi na mchezaji muhimu.

Wengine wote 11, waliobaki wamekuwa wachezaji wa daraja la kawaida ingawa siku zijazo pengine huenda wakaonyesha makali yao ila hadi sasa wameshindwa kulifanya hilo jambo.

Kutokana na hilo kwenye dirisha dogo ambalo litafunguliwa Desemba 16, Pablo atakuwa na kazi ya kuongeza wachezaji si chini ya watatu ambao wataimarisha zaidi kikosi chake.


VIKOMBE VITATU

Simba waliachana na Gomes kutokana na kuanza vibaya kwake msimu alipopoteza ubingwa wa Ngao ya Jamii pamoja na kuondolewa hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pablo atakuwa na kibarua kizito ambacho kitamfanya kuwa na uhakika wa kudumu ndani ya misimu miwili kama ambavyo mkataba wake unaeleza endapo atafanikiwa.

Kibarua cha kwanza kwa Pablo anatakiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao Simba wamechukua kwa mara nne mfululizo lakini ndio utawapa tiketi ya uhakika kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Baada ya hapo atakuwa na kibarua kingine cha kutetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ambao msimu uliopita walichukua kwa kuifunga Yanga bao 1-0 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanganyika, Kigoma.

Mtihani wa mwisho kwake utakuwa ni kuchukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ambalo msimu uliopita walilipoteza kwa kufungwa na Yanga huko Zanzibar.


KOMBE LA SHIRIKISHO

Simba baada ya kuondolewa katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika nguvu zao wamezihamishia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambalo nalo wataanzia hatua ya mtoano dhidi ya Red Arrows ya Zambia.

Baada ya kuondolewa kwenye CL, halitakuwa jambo rahisi kwao kupoteza nafasi hiyo kwani kila mmoja kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wataunganisha nguvu ili kufanya vizuri.

Kocha huyo kama atakiongoza kikosi hicho kufanya vizuri mechi hizo mbili dhidi ya Red Arrows nyumbani na ugenini maana yake watakwenda hatua ya makundi, jambo ambalo kila Mwanasimba anatamani kuona linatokea.


WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema kitu cha kwanza Pablo anatakiwa kuwauliza wasaidizi wake kila ambacho anahitaji ili kuona namna gani atafanya kazi ikiwemo nidhamu za wachezaji.

“Anatakiwa kusimamia nidhamu, kupata matokeo mazuri kupunguza presha iliyopo Simba pamoja na kutengeneza timu bora ya kwake kwani hii ya sasa ameikuta,” alisema Kibadeni.

Aliyewahi kuwa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: “Hakuna sehemu ambayo utafanya kazi bila changamoto, ambacho naamini tumpe muda na kuona namna gani Simba itatengenezwa na ile mitihani iliyokuwepo namna gani ataitatua,” alisema Kamwaga.