Okrah: Eti Yanga? subirini

STRAIKA mpya wa Simba, Augustine Okrah amezungumza mambo mbalimbali huku akiitaja Yanga kwa mara ya kwanza, na kuitumia salamu kwamba “dabi ndiyo itaamua”, ingawa hana hofu na wababe hao wa Jangwani

Okrah ni mmoja wa wachezaji anayesubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Simba kumuona akifanya vitu uwanjani, ni straika aliyesajiliwa dirisha hili akitokea Bechem United ya Ligi Kuu Ghana.

Mchezaji huyo amekuwa akizungumziwa kama mmoja wa mastraika hatari katika kufumania nyavu, lakini anadaiwa pia kuwa mmoja wa nyota walioing’arisha ligi ya nchi hiyo msimu uliopita.

Mwanaspoti limeweka kambi hapa Ismalia, Misri ilipo kambi ya Simba na kushuhudia jinsi mastaa wapya na waliokuwepo Msimbazi msimu uliopita wakipikwa akiwamo Okrah, ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya vizuri na kama ataendelea hivyo hadi katika mashindano yanayoikabili timu hiyo atakuwa mmoja ya nyota wa kuchungwa ndani ya kikosi msimu ujao.

Ili kujua mengi juu ya Okrah, Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalumu mjini hapa na kufunguka mengi kuhusu maisha ya soka ndani ya Simba kwa muda mfupi aliopo pamoja na timu nyingine alizowahi kucheza.


AWAGUSA YANGA

Okrah anasema kabla ya kutua Tanzania hakuifahamu Yanga, lakini baada ya kufika alianza kusikia habari zake hasa mechi ya Ngao ya Jamii ambayo itapigwa siku 10 zijazo yaani Agosti 13 kati yao na watani wao hao wa jadi.

Anasema kama wachezaji wamepanga kupambana kuhakikisha wanapata ushindi ili kufikia malengo ya kutwaa taji la kwanza msimu.

“Hakuna mchezo wowote wa dabi katika nchi zote nilizopita ambao ni rahisi. (Dabi) haikuwahi kuwa rahisi, nafahamu Tanzania siku hiyo mashabiki wanakuwa wengi uwanjani, ila wale wa kwetu wanatakiwa wafahamu wachezaji wao tunakwenda kupambana na kuvunja rekodi mbaya ya mechi kama hiyo msimu uliopita,” anasema Okrah.

“Nimewaona Yanga kidogo na kutokana tunacheza nao baada ya kumalizana na kilele cha Wiki ya Simba ndio nitawaelezea zaidi kwani nitakuwa nawafahamu, lakini kwa sasa tunaendelea na maandalizi ikiwemo michezo ya kirafiki iliyobaki.

“Kama Yanga ni timu kubwa, basi zinakwenda kukutana timu kubwa mbili, ila kwetu hatutaki kuanza kwa rekodi mbaya. Nieleze tu hili taji tunalitaka na kuweka kabatini taji letu la kwanza msimu ujao, kwani utakuwa mwanzo mzuri kwetu.”


NAFASI ANAYOPENDA

Okrah anasema kila kocha huwa na mifumo anayopenda kuitumia na wakati akiwa Ghana kabla ya kujiunga na Simba timu yake na benchi la ufundi lilikuwa likitumia zaidi mfumo wa 4-3-3 na alikuwa akitumika kama namba kumi nyuma ya mshambuliaji wa kati.

“Binafsi napendra kucheza nyuma ya mshambuliaji namba kumi, kwani nakuwa nikicheza kama mchezaji huru jambo ambalo linanipa nafasi ya kutengeneza mabao kwa wachezaji wengine na muda mwingine kufunga mwenyewe. Naelewa nina uwezo wa kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara,” anasema.

“Muda mwingine nafurahi zaidi kutumika kama winga nikitokea upande wowote kati ya kushoto au kulia, kwangu naona ni sawa hakuna shida yoyote, ila kama kutakuwa na mabadiliko kutokana na benchi la ufundi ambavyo litahitaji kwangu sawa wala haina shida.”

Okrah anasema: “Unaweza kuona nimeeleza hivyo, nafasi ambazo napenda kucheza kumbe kwa benchi la ufundi linaona linaweza kunitumia vingine, hilo wala sio shida kwangu kwani hata huko nitafanya vizuri na malengo makubwa ni kuhakikisha Simba tunafanya vizuri na kutoa mchango katika michezo yote.”


USHINDANI WA NAFASI

Katika nafasi ambazo Okrah anacheza kuna wachezaji wengine wenye viwango bora kamą Clatous Chama, Moses Phiri, Pape Sakho, Kibu Denis na wengineo ikionyesha kwamba kutakuwa na ushindani wa kuwania namba kutumika mara kwa mara.

Okrah anasema uamuzi wa kuwatumia wachezaji katika michezo mfululizo unategemea na vile ambavyo benchi la ufundi linaamua, kwa maana hiyo licha ya ubora wa wachezaji waliopo ikitokea akipata nafasi atafanya kilicho bora kwa ajili ya kuhakikisha kwamba malengo ya timu yanafikiwa.

“Ushindani lazima utakuwa mkubwa ndani ya timu yetu kwa jinsi ambavyo wachezaji wapya tumeingia na wale waliokuwa kwenye timue msimu uliopita, ila kwangu nitapambana na kushindana katika mazoezi ili kufanya kilicho bora na kupewa nafasi ya kucheza mechi, na nikiwa uwanjani wakati wa mchezo kufanya na kuonyesha kiwango bora ili kuendelea kuaminiwa na kupewa nafasi zaidi,” anasema.


MABAO JE?

Katika timu ambazo Okrah amepita alionyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya aina mbalimbali pamoja na kuhusika kutengeneza nafasi nyingi za wazi kwa wengine ili wafunge hasa mpira unapokuwa katika mguu wake wa kushoto.

Straika huyo anasema ana uwezo wa kufunga mabao kutokana na mipira iliyokufa kama faulo, penalti na aina nyingine mbalimbali na ni faida ya kuandaliwa vizuri tangu akiwa mdogo katika timu za vijana nchidi kwao.

“Ikitokea nikapewa nafasi hiyo nikiwa Tanzania nina imani nitakuwa nafanya pengine zaidi ya maeneo mengine niliyopita nikiwa nacheza soka la ushindani,” anasema Okrah.


KWA NINI SIMBA?

Okrah anasema kabla ya kufanya uamuzi wa kutua Simba kulikuwa na ofa nyingi kutoka katika timu tofauti, lakini alishindwa kukubaliana nazo kutokana na mambo mawili.

Kwanza, anasema Simba ilimpatia pesa nzuri za usajili pamoja na mshahara ambao atakuwa analipwa kila mwisho wa mwezi wakati akitimiza malengo ya kucheza klabu hiyo kubwa yenye mafanikio.

“Mara ya kwanza baada ya kusikia Simba inanihitaji nilishtuka na sikutaka kuamini kama ni kweli kwani ni moja ya timu kubwa na yenye mafanikio katika mashindano ya ndani na ya kimataifa. Wamekuwa kwenye ushindani wa kutosha,” anasema.

“Siyo rahisi timu kama Simba yenye mafanikio makubwa kuhitaji huduma yangu, ndio maana baada ya kusikia hivyo wala sikutaka kusikia lingine lolote zaidi ya kukubali na kukamilisha haraka usajili wangu wa kufika katika timu kubwa na yenye mafanikio kama hii.

“Lakini pia kila mchezaji anatamani kucheza timu kubwa kama Simba ndio maana nilifanya uamuzi ya kuja hapa na naamini nitapambana vya kutosha ili kupata nafasi ya kucheza na kufanya kila kilicho bora ili timu iweze kufanikiwa.”

Mchezaji huyo anasema: “Kabla ya kufika Simba nilikuwa nikifuatilia mambo mawili, kwanza niliambiwa Ligi (Kuu Bara) ni kubwa na yenye ushindani, lakini wapo marafiki kama James Kotei, Nicholas Gyan, Benard Morrison na Pascal Wawa waliowahi kupita, na kila mmoja kwa nafasi yake alinieleza Simba ni mahala salama kucheza na kutimiza ndoto zangu.”


KUMBE AZAM ILIMTAKA

Okrah anasema kabla ya kufanya uamuzi wa kujiunga na Simba aliyokubaliana nayo kila kitu hadi kusaini mkataba wa kucheza Msimbazi, Azam iliingia katika mbio za kuhitaji saini yake ingawa iliishia njiani.

“Nakumbuka wakati Azam wanaendelea kujipanga na mazungumzo pamoja na wakala wangu hata sielewi kitu gani kilitokea Simba walikuja kwa nguvu zote wakiwa na kila kitu ambacho nahitaji na kunisainisha. Wakati Azam wanarudi nilikuwa nimekamilisha kiła kitu tayari (Simba) kwa hiyo ilishindikana kwenda kwao,” anasema Okrah.

“Simba ni timu kubwa kama nilivyoeleza hapo awali na walikuja na kiła kitu ambacho nilikuwa nahitaji katika maslahi yangu tena yaliyo bora. Ilikuwa ngumu kuachana nao na kuanza kufikiria kwenda kwingine ambapo bado kulikuwa hakujakamilika.

“Hata baada ya kumalizana na Simba nilipata ofa nyingine kubwa Ulaya na Afrika, (lakini) ilikuwa ngumu kwangu kwani wakati huo nilishasaini mkataba na akili yangu ilikuwa ni kuanza maisha mapya kwenye klabu hii kubwa yenye mafanikio.”


MAISHA YA MPIRA

Okrah anasema alianza kucheza soka katika timu za vijana akiwa kwao, Ghana, ikiwemo timu ya Taifa kabla ya kuanza kucheza soka la ushindani nchini humu na hapa anasema, soka la ushindani alianza msimu wa 2012/13 katika timu ya RB Ghana kabla ya msimu huohuo kutua Asante Kotoko kisha akatua Liberty Prof kama mchezaji huru.

“Baada ya hapo nikaenda tena Asante Kotoko, kisha 2013/14 nikajiunga kwa mara ya kwanza na Bechem United ambayo msimu uliofuata walinitoa kwa mkopo kwenda Hacken ambayo nayo msimu wa 2014/15 walinirudisha klabu yangu Bechem,” anasema Okrah.

“Msimu wa 2014/15 nilijiunga na Al Merreikh ambayo nayo nilicheza kwa msimu mmoja, nao walifanya biashara nyingine ya kuniuza Al Hilal ya Sudan ilikuwa msimu wa 2016/17 na nilicheza kwa msimu mmoja kabla nao kuniuza Smouha nilikocheza msimu wa 2017/18.

“Msimu wa 2018/19 nilitu North East United kwa mkataba wa mwaka mmoja kisha 2019/20 nilisajiliwa tena na Asante Kotoko ya nyumbani kwetu Ghana kabla ya msimu wa 2021/22 kufanya biashara ya kuniuza Bechem United baada ya kuonyesha kiwango bora na Simba ilivutiwa na kiwango changu hadi kunisajili na hiyo ndiyo historia yangu ya soka tangu nilivyoanza.”


GHANA FRESHI

Miongoni mwa wachezaji waliokuwa kivutio katika Ligi Kuu ya Ghana, Okrah ni miongoni mwao na hiyo inatokana na kiwango bora alichoonyesha hasa katika misimu miwili iliyopita, akisema ni kutokana na kujituma kwake katika kila mechi kiasi cha kuwafurahisha mashabiki wa soka na ameweka malengo kama hayo katika maisha yake Simba.

Anasema kikubwa ambacho mashabiki wanapenda kutoka kwa kila mchezaji ni uwezo wa kutimiza majukumu uwanjani katika kila mechi na hilo amepanga kulifanya Simba ili kuwafurahisha Msimbazi na kuhakikisha timu inafanya vizuri.

“Nikiangalia aina ya maandalizi ya huku Misri wachezaji, benchi la ufundi pamoja na uongozi najiona kwenda kufanya vizuri kwa ushirikiano katika maeneo yote na hata Tanzania nitakuwa kipenzi cha mashabiki kama nyumbani kwetu Ghana,” anasema Okrah.

“Unajua hawa mashabiki wa soka duniani kote hakuna ambacho wanahitaji zaidi ya kuona timu yao inafanya vizuri kushinda kila mechi pamoja na kuchukua mataji, huku wachezaji wao wakionyesha viwango bora.

“Umeona hawa wachezaji wa Simba msimu ujao watakuwa vipenzi vya mashabiki wa timu yao kwani kila mmoja amekuwa akionyesha kiwango bora naamini watafanya hivyo hadi katika michezo ya mashindano yanayoanza muda mfupi ndani ya mwezi huu.”


MASHABIKI SIMBA

Okrah ana mengi kwa mashabikiwa wa Simba, lakini kutokana na kutajwa sana wakati wa usajili wake Msimbazi anachukulia kama deni ambalo linamsumbua zaidi akilini ili kuhakikisha kwamba anakwenda kulilipa uwanjani, kwani hata mitandaoni kaongeza mashabiki wengi wanaomfuatilia, licha ya kwamba hataji idadi yao.

“Mashabiki wa Simba nafahamu kama wananipenda, kwani tangu nimefika nimeongeza wafuasi wengi katika mitandao yangu yote ya kijamii tofauti na nilivyokuwa nacheza kwenye timu nyingine huko nyuma,” anasema Okrah

“Hata nikiweka picha katika mitandao yangu ya kijamii nimekuwa nikipokea ujumbe mwingi kwa Kiswahili na wote wakijieleza kuwa ni mashabiki wa Simba na wanategemea makubwa kutoka kwangu, nami niwaeleze tu wala siwezi kuwaangusha.”

Kuhusu familia yake, anasema inafurahia uwepo wake Msimbazi na mapokezi aliyoyapata klabuni.

“Familia yangu ina furaha tangu ijue nimejiunga na Simba. Nimefurahia mazingira ya timu hii. Kimsingi nimeamua hadi kuweka kitu kwenye simu yangu (mtu) akiongea au kuandika Kiswahili inaniletea kwa lugha ya Ghana ambayo naelewa haraka ili kuweza kumjibu, lakini chumbani kwangu kambini naishi na Victor Akpan ambaye naye anaelewa Kiswahili ananifundisha kila siku.”


UONGOZI SIMBA

Okrah anasema uongozi wa Simba upo makini na unataka kuona timu inafanikiwa, kwani ndani ya muda mfupi imefanya mambo makubwa ya msingi akishukuru viongozi wa juu wawili wa klabu hiyo kutumia muda wao kumfuata hadi Ghana kukamilisha usajili wake.

Anasema katika kambi Ismalia wanapata kila kitu cha msingi wanachotaka tena kwa wakati jambo ambalo linawafanya wachezaji na benchi la fundi kufikiria kazi zaidi kuliko kitu kingine chochote.

“Timu yoyote yenye mafanikio duniani kote lazima viongozi waonyeshe kutimiza majukumu na kufanya yote ya kiutawala kama ilivyo kwa Simba. Ushirikiano kama huu ukiendelea hadi katika mashindano wachezaji watakuwa na deni kubwa la kuhakikisha wanafanya vizuri na hilo linawezekana kutokana na malengo yalivyo,” anasema.


MENGINEYO

Kuna mambo ambayo Okrah anaeleza kupenda ikiwamo staili ya kushangilia huku akiwa ameweka vidole vyake viwili juu kwa maana ya kuishukuru familia yake, aliyemtengenezea nafasi ya kufunga na Mungu aliyemwezesha kufanya hivyo.

Anasema anapenda muziki, lakini mingi ni ya Ghana kutokana na kuwa Tanzania bado hajaanza kuelewa Kiswahili, lakini anafurahia kula chakula cha Kitanzania kama kuku, samaki na wali na anatamani kujifunza kupika ili siku moja akiwa amekaa nyumbani ajipikie.

Pia anapenda maisha ya Watanzania kwani ndani ya muda mfupi wamemuonyesha upendo na ukarimu, jambo ambalo hakuwa analitegemea kutokana na ugeni wake. Akiwa nyumbani tofauti na majukumu ya kazini muda mwingi anapenda kupumzika pamoja na kusoma vitabu bila kusahau kuangalia runinga ikiwamo mechi mbalimbali alizowahi kucheza.

Kuna baadhi ya mechi huangalia mahala alipokuwa na kipi aliharibu ili apambane kurekebisha mwenyewe kabla ya kuelekezwa na kocha, huku pia akipenda kuangalia michezo ya timu pinzani ikiwemo kufuatilia soka la Ulaya.


MALENGO SASA

Okrah anasema lengo lake la kwanza ni kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza Simba kutokana na mchango mkubwa ambao atakuwa akiutoa kwenye kila mechi ambayo atakuwa akipewa nafasi ya kucheza hata kama ni muda mfupi.

“Simba msimu uliopita haikufanya vizuri kwa maana ya kupoteza mataji matatu katika mashindano ya ndani, tumeelezwa hilo na nimepanga kupambana ili kutoa mchango ili kuhakikisha msimu ujao tunachukua mataji yote katika mashindano ya ndani yaliyopotea msimu uliopita,” anasema.

“Nahitaji kuonyesha kiwango bora hadi mashindano ya kimataifa, kwani Simba inahitaji kufanya vizuri huku ikiwemo malengo ya muda mrefu kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, naamini kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu pamoja na benchi la ufundi tunaweza kufikia malengo.”