NYUMA YA PAZIA: Timothy George Weah nyumbani ni wapi hasa?

MMAREKANI mmoja mjivuni akiwa katika ubora wake aliwahi kutuambia ‘New York sio jiji, ni dunia’. Ndivyo Wamarekani walivyo. Wajivuni. Wanajipenda. Hawaamini kama kuna dunia nyingine nje ya Marekani. Huyu alikwenda mbali zaidi kwa kuamini kwamba hakuna dunia nyingine nje ya Jiji la New York.

Miongoni mwa watu waliozaliwa katika jiji hilo ni Jay-z, Mike Tyson na Donald Trump. Subiri kwanza. Na Timothy Weah, mtoto wa staa wa zamani wa timu ya taifa ya Liberia, George Opong Weah. Na hapohapo subiri kwanza. Tuseme tu kwamba ni mtoto wa Rais wa Liberia, George Weah. Kwa Weah siku hizi cheo cha ‘mwanasoka wa zamani’ kinapotea kwa kasi na badala yake cheo cha rais wa Liberia kinatambulika zaidi na kumheshimisha zaidi kuliko hali ilivyokuwa zamani. Na sio ajabu majuzi ukazuka utata mkubwa kuhusu mwanaye Timothy pindi alipoonekana uwanjani akiwa na jezi ya taifa la Marekani.

Majuzi nilikuwa nasoma mahala katika maoni ya watu. ‘mtoto wa rais wa taifa fulani inakuwaje mwanao aichezee timu ya taifa jingine?” Ilikuwa ni mara ya baada ya kumuona Timothy akiichezea timu ya taifa ya Marekani, halafu zaidi akatangaza jina baada ya kufunga bao katika pambano dhidi ya Wales.

Suala la uzalendo likaibuka. Nadhani kilikuwa kipimo cha juu cha uzalendo kati ya baba na mtoto. Kwanza baba ni rais wa taifa fulani lakini mwanaye anachezea taifa jingine. Inaweza ikawa ni utata wa kwanza katika soka.

Tunaona mastaa wa nchi fulani wakipata watoto ughaibuni halafu watoto wanacheza katika nchi hizo badala ya kucheza nyumbani. Ni kama mtoto wa staa wa zamani wa Brazil, Mazinho, Thiago Alcantara ambaye aliamua kuchezea Hispania ingawa baba yake ni Mbrazili. Tatizo la Weah ni rais wa nchi. Tena ni rais aliye madarakani. Wananchi wa Liberia wamekuwa wakilalamika kwamba Weah ametumia pesa za walipakodi kwenda kumtazama mwanaye Qatar akicheza Kombe la Dunia. Sijaenda mbali zaidi kujua kama wana tatizo jingine zaidi ya kodi zao. kwamba labda na wao wanaamini kwamba Timothy alistahili kuchezea Liberia na sio Marekani.

Suala la Timothy limenikumbusha swali maarufu ambalo nimekuwa nikiuliza hapa. Nyumbani ni wapi? Ndiyo, nyumbani kwa Timothy ni wapi? Mtu mmoja mhenga aliwahi kutuambia ‘nyumbani ni pale moyo wako ulipo’.

Kwa hiyo kama ambavyo Jay-Z anavyojisikia na Umarekani wake ndivyo ambavyo Timothy anavyojisikia na Umarekani wake. Alizaliwa mwaka 2000 na akaondoka kwa mara ya kwanza kwenda Ufaransa kucheza soka akiwa na miaka 14. Ndani ya miaka hii Timothy aliupata Umarekani na akawa Mmarekani. Ndani ya miaka hii Timothy alikuwa miongoni mwa watoto waliozaliwa na kuzurura katika mitaa ya New York na kisha Florida. Kumwambia kwamba nyumbani ni Monrovia inabidi umueleweshe mambo mengi. Kitu cha msingi ambacho unaweza kufanya ni kumwambia tu kwamba Liberia ni asili yake.

Wanadamu wengi tunajikuta nyumbani katika maeneo ambayo kiasili sio nyumbani. Hata hivyo moyo wako unajikuta ukiwa na amani katika eneo hilo na katika hali halisi hapo ndipo nyumbani. Unawafahamu watu wote, mitaa yote, tamaduni zote na unakuwa miongoni mwao.

Timothy ukimpeleka Monrovia hawezi kujisikia yupo nyumbani. Nyumbani kwake ni New York na hajisingizii. Ndivyo ilivyo. Wanaotaka ajisikie kuwa nyumbani ni Liberia huwa wananichekesha kidogo. Na wengine ni wale ambao hawajawahi kufika hata katika vijiji vyao au katika mikoa yao na sisi hatuwezi kuwalaumu.

Lakini katika nchi ambayo amezaliwa na kukulia, sidhani kama kuna vipaji vikubwa vya kumfanya akumbuke asili yao na kwenda kucheza katika taifa ambalo baba yake amezaliwa. Timothy kwa kipaji alichonacho ilikuwa rahisi tu kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Marekani. Tukumbuke Timothy ni mmoja kati ya Wamarekani wachache ambao wanacheza katika ligi kubwa tano barani Ulaya. Ligi ambazo zimeiacha Ligi Kuu ya Marekani kwa mbali. Anakipiga katika klabu ya Lille ya Ufaransa na huwa anacheza kila wikiendi. Sio wachezaji wengi wa Marekani wamepata fursa hii.

Lakini kuthibitisha kwamba hachezi katika kikosi cha kwanza kwa sababu baba yake ni rais tumeona alichofanya katika pambano dhidi ya Wales. Na hapana shaka jana alitazamiwa kucheza katika pambano dhidi ya England.

Kuna rafiki zetu ambao wana unafiki zaidi. Wanaposhindwa kucheza katika mataifa makubwa ndio huwa wanakimbilia kwetu na kujifanya wazalendo. Hawa ni kina Inaki Williams. Ameona ameshindwa kucheza katika kikosi cha Hispania ameamua kukimbilia Ghana. Alijua kwamba Ghana inampa nafasi ya kucheza Kombe la Dunia. Asingeweza kuipata nafasi hiyo kama angesubiri Hispania.

Mdogo wake, Nico Williams kwa sababu ana uwezo mkubwa yeye ameitwa na kocha Luis Enrique Martinez. Huyu Inaki anatudanganya kwamba nyumbani ni Ghana wakati mdogo wake anatuambia ukweli kwamba nyumbani ni Hispania.

Hawa sio wa kwanza kufanya hivi. Kumbuka stori ya Jerome Boateng na kaka yake Kevin-Prince Boateng. Jerome alifanikiwa kupata nafasi katika kikosi cha Ujerumani. Nadhani ni kwa sababu wakati huo nafasi ya beki haikuwa na ushindani mkubwa au tufanye Jerome alikuwa na uwezo mkubwa.

Kelvin-Prince akaamua kuchezea kikosi cha Ghana. Nadhani ni kwa sababu eneo la kiungo la Ujerumani lilikuwa na ushindani mkubwa na Kelvin alijua kwamba asingeweza kuitwa hata kama angekimbilia kwa waganga.

Timothy amechukua uamuzi sahihi. Angeweza kurudi kucheza Liberia kama angekuwa amezaliwa na kukulia Ufaransa. Ushindani ni mkubwa katika baadhi ya mataifa. Lakini kwa kuchagua kucheza Marekani naamini amefanya uamuzi sahihi zaidi katika kila njia. Amechagua kucheza nyumbani. Ametujibu vyema swali la ‘nyumbani ni wapi?’ Kwake yeye nyumbani ni Marekani na hapana shaka anafunga mjadala wetu kuhusu uamuzi wake.